MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara),Pius Mswekwa na Mlezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara anatarajia kufanya ziara ya wiki moja katika Mkoa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na katibu Mwenezi wa Mkoa wa Mara, Maximillian Ngesi alisema ziara hiyo ina lengo la kuangalia uhai wa Chama na kuzungumza na wanachama paomoja na kuratibu maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.
Alisema kuwa kama ulivyo utaratibu wa chama cha Mapinduzi kuwa na walezi kila Mkoa nchini,Mlezi wa kila Mkoa hana budi kutembelea Mkoa wake na wilaya zote.
Ziara hiyo inatarajia kuanza juni 11-17 ambapo atatembelea wilaya za Tarime, Rorya, Serengeti, Bunda, Musoma Mjini na Musoma Vijijini.
Aidha ziara hizi ni za walezi wa nchi nzima kwa mujibu wa taratibu na kanuni za Chama.
Mlezi wa awali alikuwa Mheshimiwa Samweli Sitta.
MUSOMA
JUMLA ya kadi 550 za CCM zimekamatwa na kukabidhiwa katika ofisi ya CCM wilaya ya Musoma Mjini na kurudishwa Makao Makuu.
Akizungumza na waandishi wa habari hii ofisini kwake jana Katibu Msaidizi Wilaya ya Musoma Mjini, Hamisi Mkaluka alisema kuwa kadi hizo zilikamatwa hivi karibuni na makatibu wa matawi ambapo baadhi ya wagombea wamesambaza kadi hizo.
Alisema kuwa baada ya makatibu tawi kupelekewa kadi hizo ili kuingiza wanachama wapya katika daftari la wanachama wa CCM Tawini bila kufuata utaratibu makatibu hao waliamua kurejesha kadi hizo wilayani.
"Mwanachama kama anataka kuingia kwenye chama anapaswa kutuma maombi ama kwenda kwa katibu na baada ya hapo inakaa kamati ya siasa tawi kupitia maombi yote ya wanachama wapya waliokubaliwa na muhtasari kupelekwa kwenye kata na Wilaya ambapo utaratibu huu ni wa kikatiba lakini ulisahaulika"Alisema Mkaluka.
Aliongeza kuwa "Kuna baadhi ya wagombea wanazo kadi zao ambazo hatutambui wamezitoa wapi ili kuzitumia kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi lakini wameshidwa kuzitumia na makatibu wa matawi wamegundua na kusababisha kuwepo malumbano na kutumia baadhi ya vyombo vya habari kutaka kupaka matope Chama na uongozi wa Mkoa kwa ujumla kwa kuandika habari za uzushi".
Alifafanua kuwa wagombea ambao walitaka kuingia kwa njia za panya wamedhibitiwa na kwamba utoaji wa kadi unatolewa kulingana na idadi ya wanachama walioomba na kukubaliwa kuingia katika chama.
Alisema kuwa hakuna mtu aliyezuiliwa kuingia katika chama bali afuate utaratibu wa kikatiba kwa kulipia kadi sh.500 na ada 1,200 na baadaye kuingizwa kwenye daftali la wanachama kufuatia agizo kutoka Makao Makuu na kwamba ni zoezi ambalo linaendela kwa wanachama wapya hadi Juni 30 mwaka huu ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kuingiza wanachama wapya katika daftari hilo.
Kadi hizo zilikamatwa katika kata ya Nyakato, Kigera na Rwarulimi.