Monday, November 5, 2012

MAELEZO YA KIUTENDAJI YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU,TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAAHAWA GHASIA





MAELEZO YA KIUTENDAJI YA MHESHIMIWA HAWA ABDUL RAHMANI GHASIA (MB), WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA KUHUSU MAPITIO YA KAZI MWAKA WA FEDHA 2011/12 NA MWELEKEO
 WA KAZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/13

1.            Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nguvu na kuniwezesha leo kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia, nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyoionesha kwangu kwa kuniteua katika nafasi hii ya kuwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili nishughulikie Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Naahidi kufanya kazi kwa uwezo wangu kadri mungu atakavyonijalia.

2.            Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii pia kumshukuru Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba nzuri ya Mwelekeo na Malengo ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa fedha 2012/13. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Stephen Masato Wasira (Mb), kwa hotuba ya Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2011/12 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13.     Pia   nampongeza  Mheshimiwa  Dk. William Mgimwa (Mb), Waziri wa Fedha kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na nimpongeze vilevile kwa hotuba aliyotoa kuhusu Mapendekezo ya Serikali ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/13.  Hotuba zote zilizotangulia zimeonesha mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2012/2013.

3.            Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Naibu wa Spika kwa uongozi imara na madhubuti katika Bunge hili.  Aidha, namshukuru kwa namna ya pekee Naibu Waziri Mheshimiwa Aggrey D. J. Mwanri (Mb) wa Siha, anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Majaliwa Kasimu Majaliwa (Mb) wa Ruangwa,  anayeshughulikia  Elimu  chini ya  OWM-TAMISEMI,   Katibu   Mkuu   Bw. Hussein A.  Kattanga,  Naibu  Makatibu  Wakuu               Bw. Jumanne A. Sagini, Bw. Alphayo J. Kidata, Wakurugenzi na Watumishi wa OWM-TAMISEMI ambao kwa kipindi kifupi nilichofanya nao kazi wamenipa ushirikiano wa kutosha hivyo, ni imani yangu tutafanikisha kuyatekeleza majukumu ya ofisi kwa manufaa ya Watanzania wote. Niwashukuru Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wote wa Mikoa na Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Mabaraza ya Madiwani, wote kwa pamoja nawaahidi ushirikiano.

4.            Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mawaziri kama ifuatavyo: Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb); Mhe. Dkt. Fenella Ephraim Mukangara (Mb); Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb); Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (Mb); Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb); Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb). 

5.            Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mawaziri katika Wizara mbalimbali, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb); Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb); Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb); Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb); Mhe. January Yusuf Makamba (Mb); Mhe. Dkt. Charles John Tizeba (Mb); Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb); Mhe. Angela Jasmine Kairuki (Mb); Mhe. Stephen Julius Maselle (Mb); na Mhe. Mhandisi Dkt. Binilith Satano Mahenge (Mb.). 

6.            Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mhe. Musa Azan Zungu (Mb) wa Ilala kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Kadhalika, nampongeza Mhe. James Mbatia (Mb) kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge, na Waheshimiwa Dkt. Dalali Kafumu, Joshua Nasari kuchaguliwa kuwa Wabunge katika Majimbo yao na Mhe. Cesilia Pareso kuwa Mbunge wa Viti Maalum.

7.            Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kutoa pole kwa familia za Wabunge wenzetu waliopoteza maisha baada Bunge la Bajeti la mwaka 2011/2012.  Wabunge hao ni Marehemu Jeremiah Sumari aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki na Marehemu Regia Mtema aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum. Tunaomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi na awajalie ndugu jamaa na marafiki wa marehemu moyo wa subira.

8.            Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala chini ya Uongozi wa Mwenyekiti Mheshimiwa Pindi Hazara Chana (Mbunge wa Viti Maalum - CCM) na Makamu Mwenyekiti Mhe. John Paul Lwanji (Mbunge wa Manyoni Magharibi) kwa kuichambua bajeti ya ofisi yetu na kutupa maoni na ushauri ambao unaendelea kutujenga katika utendaji wetu wa kazi, nawashukuru sana. Tutayachukua maoni na ushauri walioutoa kwa uzito unaostahili na kuufanyia kazi.

9.            Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wananchi wa Mtwara Vijijini kwa mshikamano na ushirikiano wanaonipatia katika majukumu yangu ya ubunge na uwaziri wa Nchi, OWM-TAMISEMI.  Naahidi kuendelea kuwatumikia kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijalia ili kwa pamoja tufanikishe shughuli za kujiletea maendeleo katika Jimbo letu.

Utekelezaji wa Majukumu kwa Mwaka wa Fedha 2011/12 na Mwelekeo kwa Mwaka wa Fedha 2012/13

Utawala Bora

10.       Mheshimiwa Spika, Serikali za Mitaa ndio mhimili mkubwa wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika lengo zima la kuhakikisha yanakuwepo maendeleo endelevu katika nchi yetu. Upelekaji wa madaraka kwa wananchi unapitia katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na ndiyo maana Serikali za Mitaa na ushirikishwaji wa Wananchi katika mchakato wa maendeleo vimetambuliwa katika Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ufafanuzi wa dhana ya kupeleka madaraka kwa wananchi umeelezwa kwa kina zaidi katika Sera ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1998 (The Policy Paper on Local Government Reform of 1998). Katika Sera hii, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapewa uhuru (autonomy) wa kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu utoaji wa huduma kwa wananchi walio katika mamlaka hizo kwa kuwashirikisha wananchi katika kujiletea maendeleo na ustawi wao kwa ujumla. Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatakiwa kuutumia uhuru huo kwa kuzingatia Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na endapo zitakwenda kinyume chake, Serikali Kuu inao wajibu wa Kikatiba na Kisheria kuingilia kati (intervene) na kuchukua hatua dhidi ya mamlaka hizo.

11.       Mheshimiwa Spika, Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa umetekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya Kwanza ilianza kutekelezwa mwaka 1998 hadi 2008 na Awamu ya Pili imeanza kutekelezwa mwaka 2009 na utakamilika mwaka 2014. Katika awamu ya pili Mikoa yote imepatiwa Wataalam Washauri watakaosaidia kujenga uwezo wa ngazi hii ili kuweza kuzishauri na kuzisimamia kwa karibu Mamlaka za Serikali za Mitaa. Wataalam hawa watafanya kazi kwa karibu na Makatibu Tawala Wasaidizi katika Sekretarieti za Mikoa katika kuimarisha masuala ya fedha na rasilimali watu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ni matarajio yetu kwamba baada ya muda, wataalam wote walio katika Sekretarieti za Mikoa watakuwa wamejengewa uwezo wa kusimamia shughuli hizo.

12.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Halmashauri 62 zimepatiwa magari ili kuwezesha vitengo vya Ukaguzi wa Ndani kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Nyenzo hii ya usafiri itawawezesha kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika ngazi za chini za Halmashauri na hivyo kubaini thamani ya fedha katika miradi inayotekelezwa. Aidha, Mikoa yote imepatiwa magari ambayo yatatumiwa na Wataalam waliopelekwa katika ngazi hiyo pamoja na wale wa sehemu ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa ili kuwawezesha kuzifuatilia kwa karibu Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizo katika Mikoa yao.

13.       Mheshimiwa Spika, ili Madiwani waweze kutekeleza majukumu yao vema umeandaliwa utaratibu wa kuwakopesha vyombo vya usafiri kupitia Benki. Tayari makubaliano yameshafikiwa kati ya Serikali na NMB ili kuwawezesha Madiwani kupata vyombo vya usafiri. Baadhi ya Madiwani wameanza kufaidika na utaratibu huu.   

14.       Mheshimiwa Spika, Waweka Hazina katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wamejengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo ya viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (International Public Sector Accounting Standards (IPSAS)).  Hivyo, ni mategemeo yetu kwamba mfumo huu utawasaidia katika kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa ya kusimamia vizuri fedha za Serikali na kutoa taarifa zilizo sahihi kwa wakati unaotakiwa.

15.       Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza shughuli zinazohusiana na uboreshaji wa uendeshaji wa Mabaraza ya Kata, OWM-TAMISEMI ilimteua Mtaalam Mshauri ambaye alipewa kazi ya kupitia Sheria na nyaraka mbalimbali zinazohusu uendeshaji wa Mabaraza ya Kata na kupendekeza namna bora ya kuboresha utendaji kazi wa Mabaraza hayo kwa kuzingatia mabadiliko yaliyotokea hadi sasa. Baadhi ya matatizo yaliyoibuliwa na Mtaalam Mshauri katika taarifa yake ni pamoja na malipo na posho kwa Wajumbe wa Baraza la Kata; uwezo na sifa za Wajumbe wa Mabaraza ya Kata; mafunzo kwa wajumbe wa Baraza la Kata; ukosefu wa vitendea kazi; kutekeleza majukumu ya Kimahakama zaidi kuliko ya usuluhishi; Mabaraza hayo kuwepo chini ya Mamlaka tatu tofauti yaani chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ambalo lipo chini ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Mahakama Kuu.

16.       Mheshimiwa Spika, Changamoto zilizojitokeza katika taarifa hiyo zilijadiliwa na wadau mbalimbali na hatimaye maoni na mapendekezo ambayo yaliwasilishwa Serikalini. Maoni na mapendekezo hayo yanafanyiwa kazi na Serikali kwa kushirikiana na Tume ya Kurekebisha Sheria.
           
Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa

17.       Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha utendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali imekuwa ikichukua hatua kwa watumishi wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali. Kuanzia mwaka 2009/10 hadi Machi, 2011/12, Wakurugenzi wa Halmashauri wapatao 24 walichukuliwa hatua za kinidhamu, kati yao 8 walivuliwa madaraka, 11 walipewa onyo, 3 wamepumzishwa kazi na 2 wamesimamishwa kazi na kesi ziko mahakamani.  Aidha, Wakuu wa Idara 74 wa Halmashauri mbalimbali wamechukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na tuhuma zinazowakabili.  

Kujenga Uwezo wa Sekretarieti za Mikoa

18.       Mheshimiwa Spika, Ofisi yangu imetoa mafunzo kwa viongozi wa Sekretarieti za Mikoa ili kuwakumbusha majukumu yao kwa lengo la kuboresha utendaji wa kazi.  Mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na Maandalizi ya Mipango na Bajeti kwa Makatibu Tawala Wasaidizi 75 kutoka Mikoa 21.  Mafunzo hayo yalilenga kuwapa uelewa zaidi katika kuandaa Mipango, Bajeti na Taarifa za Mikoa yao.  Makatibu Tawala wa Mikoa 21 walipata mafunzo hayo katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo ambapo dhumuni kubwa lilikuwa ni kuwajengea uwezo wa kiutendaji ili kuwawezesha kuzisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa katika maeneo yao.

19.       Mheshimiwa Spika, kujenga uwezo wa Sekretarieti za Mikoa ni pamoja na kuimarisha utendaji wa Maafisa Tarafa.  Mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa Maafisa Tarafa wanapata vitendea kazi hususan vyombo vya usafiri na ofisi.  Aidha, nafasi wazi za Maafisa Tarafa 145 tayari zimepata kibali cha ajira na mchakato wa kuwaajiri unaendelea.

20.       Mheshimiwa Spika, Ofisi yangu imeendelea kuzifanyia mapitio Sheria mbalimbali ili ziweze kuendana na mabadiliko yanayojitokeza katika uendeshaji wa shughuli za Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sheria ya Tawala za Mikoa namba 19 ya mwaka 1997. Mapitio yatakapokamilika yatawasilishwa mbele ya Bunge lako tukufu. Lengo kubwa ni kuimarisha utendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na  Sekretarieti za Mikoa.
           
Mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa

21.        Mheshimiwa Spika, makisio ya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2010/11 makadirio yalikuwa shilingi bilioni 173.1 na makusanyo halisi yalikuwa shilingi bilioni 158.3 sawa na asilimia 92.  Aidha, kwa mwaka wa fedha 2011/12 makadirio yalikuwa shilingi bilioni 350.5. Hadi kufikia Machi 2012 zimekusanywa shilingi bilioni 142 .8 sawa na asilimia 40.7. 

22.       Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa katika Halmashauri ni kujiwekea makadirio kidogo katika ukusanyaji mapato. Ili kuondoa tatizo hili Ofisi yangu  imeanza kuandaa mikakati ya kusaidia kuimarisha ukusanyaji wa mapato.  Vikao vya kitaalamu vya uchambuzi wa mipango na bajeti za kila chanzo na ushahidi wa takwimu za walipa kodi na vitu vinavyolipiwa kodi (Tax Payers na Tax Objects) vimefanyika. Taarifa hizo muhimu zitatumika pamoja na taarifa za utafiti unaotarajiwa kufanywa na wataalamu washauri katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali

23.       Mheshimiwa Spika, taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2011 iliwasilishwa Bungeni tarehe 12 Aprili 2012. Kwa mara ya tatu mfululizo, hesabu hizi ziliandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uhasibu kwa Sekta ya Umma (IPSAS).  Kwa ujumla, matokeo ya ukaguzi wa hesabu hizo yanaonesha kuwa bado kuna kazi ya ziada ya kufanya ili kuwa na utendaji ulioimarika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. 

24.       Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha kuwa kiwango cha utendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kinaendelea kuimarika. Hii inatokana na ukweli kwamba; kumekuwa na ongezeko la Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopata hati zinazoridhisha (safi) kutoka 66 (48.9%) mwaka 2009/10 mpaka hati 72 (54%) mwaka 2010/11. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopata hati zenye shaka zimepungua kutoka 64 (48.1%) mwaka 2009/10 mpaka hati 56 (42%) Mwaka 2010/11. Vilevile, kumekuwa na ongezeko la Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopata hati zisizoridhisha (chafu) kutoka 4 (3%) mwaka 2009/10 mpaka 5 (4%) mwaka 2010/11.

25.       Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya ukaguzi huo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amebainisha sababu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kupata hati zenye shaka au zisizoridhisha kama ifuatavyo;  Kutotolewa kwa mafunzo ya kutosha ya kuandaa taarifa za fedha kwa kutumia viwango vya kimataifa vya uhasibu kwa Sekta ya Umma (IPSASs) na hivyo kuandaliwa kwa taarifa za fedha zisizo sahihi; Kuwepo kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa  wanaokiuka maadili ya kazi zao na kujihusisha na ubadhirifu wa fedha za Halmashauri na hata kula njama na watumishi wa Benki na udhaifu wa mifumo ya udhibiti wa ndani.

26.       Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kuainisha vyanzo vya mapungufu yaliyoonekana wakati wa ukaguzi. Hii imetusaidia kuanza kuyafanyia kazi ili kuzuia kujirudia kwa hali hii. Eneo tunalolipa kipaumbele ni kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani na usimamizi kwenye ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa.

27.       Mheshimiwa Spika, ili kuzipa uwezo Halmashauri kusimamia fedha kwa ufanisi, matumizi ya mfumo wa Epicor 9.05 katika mfumo wa “Intergrated Financial Management System (IFMS)” utaanza kutumika kwa Halmashauri zote nchini mwaka wa fedha 2012/13. Aidha, mwezi Mei, 2012 Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI imefanya Mkutano wa kazi uliowashirikisha Makatibu Tawala wa Mikoa yote, Wakurugenzi wa Halmashauri zote, Waweka Hazina wa Halmashauri zote pamoja na wataalam wengine kutoka ngazi ya Mkoa kwa ajili ya kutafuta suluhisho la kudumu la dosari na mapungufu yanayoendelea kujitokeza katika taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali. Moja ya maazimio muhimu ya Mkutano huo ni kwamba kuanzia sasa makosa yanayotokana na uzembe na uwezo mdogo wa kusimamia kazi hautavumiliwa. Kila Katibu Tawala wa Mkoa atawajibika kwa kutokuchukua hatua zinazolenga kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika Halmashauri chini ya Mkoa anaoongoza. Kadhalika Mkurugenzi wa Halmashauri atapimwa kwa kigezo cha uwajibikaji kutokana na tathmini mbalimbali ikiwemo taarifa ya ukaguzi, kuweka kwenye mbao za matangazo taarifa za miradi inayotekelezwa katika Halmashauri pamoja na fedha zote zilizopokelewa kwa ajili ya miradi hiyo.  

28.       Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kunakuwa na uzingatiaji wa viwango vya kimataifa vya uhasibu kwa Sekta ya Umma (IPSASs) na kunakuwa na usahihi wa taarifa za hesabu zinazoandaliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali itaendelea kutoa mafunzo yanayotakiwa kwa wahasibu katika ngazi zote zinazohusika. Aidha, Serikali itahakikisha kuwa watumishi wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu, wizi na kuzisababishia hasara Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kutowajibika ipasavyo, wanachukuliwa hatua ..kwa mujibu wa kanuni,sheria na taratibu.

29.       Mheshimiwa Spika, pamoja na taarifa hizo napenda kuzipongeza Halmashauri 11 ambazo zimeendelea kupata hati zinazoridhisha (hati safi) kwa kipindi cha miaka minne (4) mfululizo; Halmashauri hizo ni za Wilaya za Mufindi, Biharamulo, Missenyi, Siha, Nachingwea, Serengeti, Kyela, Maswa, Singida na Manispaa ya Shinyanga.  Vilevile, napenda kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Mtwara kutokana na Halmashauri zote za Mkoa huo kupata hati zinazoridhisha.

Mfuko wa Barabara za Serikali za Mitaa

30.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 kiasi cha shilingi bilioni 94.02 kutoka katika Mfuko wa barabara zilitengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Halmashauri. Hadi kufikia mwezi Machi, 2012 jumla ya shilingi bilioni 73.7 zilikuwa zimepokelewa na kupelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara, pamoja na miradi mikubwa kupitia fedha za maendeleo ambazo ni asilimia 10 ya bajeti ya Mfuko wa Barabara zinazotolewa kwa OWM-TAMISEMI.

31.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 kiasi cha shilingi bilioni 128.9 kinategemewa kutoka kwenye Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali.
           

Mfumo wa Kupeleka Ruzuku ya Maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGDG)


32.       Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Kuzipatia Mamlaka za Serikali za Mitaa ruzuku ya maendeleo ulianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2004/05. Mfumo huu ndio unaotumika katika kugawa ruzuku ya maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia uwazi na usawa. Kupitia Mfumo huu, tathmini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kila mwaka na ruzuku ya maendeleo hupelekwa katika Mamlaka hizo kulingana na jinsi zilivyofuzu vigezo vilivyowekwa. Ruzuku ya kujenga uwezo hutolewa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zote kwa ajili ya kujiimarisha kiujuzi na maarifa kwenye maeneo ambayo Mamlaka hizo zitakuwa zimebaini kuwa na upungufu.

33.       Mheshimiwa Spika, Mfumo huu ulifanyiwa tathmini mwezi Septemba 2011. Mojawapo ya mapendekezo yaliyotolewa katika tathmini hii ni kufanya mapitio ya vigezo vya tathmini, kiwango cha ruzuku na namna ya kupata ruzuku ya maendeleo na ya kujenga uwezo. Kutokana na mapendekezo haya, utaratibu mbadala unaandaliwa ambao utatumika kupima Mamlaka za Serikali za Mitaa. Utaratibu mbadala unaopendekezwa ni wa kuzitumia Sekretarieti za Mikoa katika upimaji wa awali wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.  Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zitakuwa zimeshindwa kufuzu, ufuatiliaji utafanywa na timu ya wataalam ili kubaini chanzo cha mapungufu pamoja na mbinu za kuondokana na mapungufu hayo.  Hata hivyo, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali huzingatiwa wakati wa kufanya maamuzi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakazopata Ruzuku ya Maendeleo na Kujenga Uwezo.

34.       Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2012, jumla ya shilingi bilioni 106.6 zimepelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Mfumo huo zikiwa ni ruzuku isiyo na masharti.  Aidha, kwa upande wa Sekta ya Kilimo jumla ya shilingi bilioni 59.8 zilikuwa zimepelekwa kwa ajili ya ruzuku ya maendeleo ya kilimo na shilingi bilioni 43.3 zilipelekwa kwa ajili ya ruzuku ya maendeleo ya maji vijijini.  Vilevile shilingi bilioni 80.9 za Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Afya ambazo ni asilimia 100 zimetolewa na kupelekwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TSCP)

35.       Mheshimiwa Spika, Mradi wa uboreshaji wa miundombinu katika Miji Tanzania ni matokeo ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia na Serikali ya Denmark. Mradi ulizinduliwa rasmi Oktoba, 2010 na umepangwa kutekelezwa hadi mwaka 2014/15. Madhumuni ya mradi huu ni kuziwezesha Halmashauri nane (8) zinazohusika na utekelezaji wa mradi huu, kuboresha miundombinu na utoaji wa huduma za jamii katika Miji. Mamlaka hizi ni Jiji la Mwanza, Tanga na Mbeya; Manispaa za Arusha, Dodoma, Kigoma Ujiji, Mtwara Mikindani na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma. Hadi Machi, 2012, shilingi 21,520,034,150.00 (Kati ya shilingi 49,807,534,150.00 zilizotengwa) zilikuwa zimetolewa kwenye Halmashauri na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali.  Kiasi kilichobakia kitaendelea kutolewa kadri utekelezaji unavyoendelea.

36.       Mheshimiwa Spika, mbali ya fedha za ujenzi wa miundombinu, kiasi cha shilingi 4,068,292,750.00 kimeshapelekwa kwenye Mamlaka zinazotekeleza mradi huu kwa ajili ya kujenga uwezo katika maeneo mbalimbali katika Mamlaka hizo. Maeneo hayo ni kama vile Idara za Mipango Miji ambapo yamefanyika mafunzo ya Geographical Information Systems (ARC–GIS) pamoja na ununuzi wa mfumo huo (ARC–GIS software). Vilevile, Wizara ya Ardhi imepewa kandarasi ya kurekebisha picha za Satelite (Rectification and Digitization of satelite image) na kazi hiyo inaendelea kutekelezwa katika maeneo ya mradi.

Mradi wa Kuimarisha Halmashauri za Manispaa 11 na Miji 7

37.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 Serikali itaanza utekelezaji wa Mradi wa kuimarisha miundombinu pamoja na uwezo wa kutoa huduma za jamii katika Halmashauri za Manispaa 11 na Miji 7 (Urban Local Government Strengthening Programme). Manispaa zinazohusika ni Morogoro, Moshi, Iringa, Bukoba, Shinyanga, Singida, Musoma, Sumbawanga, Songea, Lindi na Tabora. Miji inayohusika ni Babati, Njombe, Korogwe, Mpanda, Kibaha, Geita na Bariadi. Mradi utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2012/13 hadi 2016/17. Mradi utagharimu kiasi cha dola za kimarekani milioni 175 ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.  Kati ya fedha hizo, dola milioni 160 zitagawiwa katika Halmashauri husika kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya aina mbalimbali kulingana na mipango ya Halmashauri hizo. Fedha zinazobaki yaani dola milioni 15 ni kwa ajili ya uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa mradi huo.

TEHAMA

38.       Mheshimiwa Spika, Ofisi yangu imeendelea kuhakikisha kuwa taarifa sahihi zinapatikana katika ngazi zote za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuwezesha utoaji wa huduma kupitia Serikali Mtandao.  Miundo ya Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa imetengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya TEHAMA na hivi sasa vimeanzishwa vitengo vya TEHAMA katika ngazi hizo.

39.       Mheshimiwa Spika, ili kuboresha mawasiliano tumefunga vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya “video conferencing” katika kila Sekretarieti ya Mkoa. Ofisi inaendelea kujenga uwezo kwa kutoa msaada wa kiufundi ili Mikoa iweze kutoa huduma ya kiufundi ya TEHAMA katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yaani Dawati la Usaidizi la TEHAMA. Aidha, Ofisi imeanzisha “Computer Laboratory” kwa ajili ya kufundisha watumishi wake katika ngazi zote kuhusu mifumo mbalimbali inayotumika katika utendaji wa kazi.

40.       Mheshimiwa Spika, mifumo ambayo imeshafanyiwa kazi katika ngazi zote za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni ifuatayo:- Tovuti za Sekretarieti za Mikoa, mfumo wa barua pepe, mfumo wa “Intergrated Financial Management System,” “Planrep” na Mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGHRIS) ambao ulitengenezwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa Ufadhili wa “Intra-Health International”.  Zoezi la uingizaji takwimu za rasilimali watu linaendelea katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 89 na Sekretarieti za Mikoa 13 ambako mfumo umewekwa.  Vifaa vya TEHAMA na mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huu vitaendelea kufungwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizosalia kupitia Programu ya Kuboresha Mfumo wa Serikali za Mitaa Awamu ya Pili (LGRP II).

Uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari Nchini

41.       Mheshimiwa Spika, OWM-TAMISEMI imeendelea kutekeleza jukumu la kusimamia utoaji wa elimu ya Msingi na Sekondari kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa.  Ofisi iliziagiza Halmashauri kupitia Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha kwamba watoto wenye umri stahiki wanaandikishwa na kuhudhuria Shule za Msingi bila kukosa kama inavyoelekezwa na Sera ya Elimu na Mafunzo.  Aidha, Halmashauri zilitakiwa zisimamie uwepo wa madarasa ya elimu ya awali kwenye Shule za Msingi ili watoto wengi zaidi wapate fursa ya kuhudhuria elimu ya awali kabla ya kuanza darasa la kwanza.  Ofisi ilishirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za ‘Capitation’ katika Halmashauri zake ikiwa ni pamoja na fedha nyingine zinazopelekwa katika Halmashauri husika.  Aidha, Halmashauri zimetakiwa kutumia fedha wanazopata kwa uadilifu ili kuepuka madeni hasa ya chakula na vifaa vya kujifunzia.

42.       Mheshimiwa Spika, iko changamoto ya maeneo ya shule hasa mijini kuvamiwa au kwa kutumia mikataba isiyo halali wafanyabiashara kujenga vibanda vya biashara kuzunguka eneo la shule.  Matumizi ya maeneo ya shule yamefafanuliwa katika Gazeti la Serikali Na. 298 la mwaka 2002 kuwa ni  kinyume cha sheria, kanuni na taratibu kufanya biashara katika maeneo ya shule au kutumia majengo ya shule kwa shughuli za biashara. Kupitia Bunge lako Tukufu nawaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa yote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali tarehe 15 Januari, 2010 kuhusu kudhibiti biashara katika maeneo ya Shule. Aidha, Wakuu wa Mikoa wanatakiwa kufuatilia suala hili kwa karibu kuhakikisha kuwa biashara hizo zinasitishwa katika maeneo ya shule.  Hata hivyo, suala la kuwepo kwa vibanda vya chakula, Ofisi yangu kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kulifanyia kazi ili kupata utaratibu utakaoonekana unafaa katika kutoa huduma ya chakula katika shule kwa ajili ya walimu na wanafunzi bila kuathiri maadili ya msingi ya Shule zetu.

43.       Mheshimiwa Spika, vilevile, viko vibali vya biashara vinavyotolewa na Halmashauri ambavyo vinasababisha kujengwa kwa majengo ya biashara za nyumba za kulala wageni na baa karibu na viwanja vya shule. Napenda kutumia fursa hii kupitia Bunge lako tukufu kuziagiza Halmashauri zote hususan za mijini kusitisha vibali vyote vilivyotolewa vya kufanya biashara za nyumba za kulala wageni na uendeshaji wa baa katika viwanja vinavyopakana na maeneo yaliyojengwa shule. Aidha, liko suala ambalo linajitokeza la maeneo ya shule za Msingi na Sekondari kutokuwa na hati miliki kwa viwanja ambavyo vimejengwa shule hizo.  Hali hii inachangia uvamizi wa ujenzi wa makazi na biashara katika viwanja vya shule. Halmashauri zote nchini zinatakiwa kupima viwanja vya shule zilizo katika maeneo yao na kuzipatia hati miliki.

44.       Mheshimiwa Spika, ili kuratibu na kusimamia upatikanaji wa maslahi ya walimu wa shule za msingi na  sekondari kwa kuyaboresha, jumla ya walimu 23,167 waliwasilisha madai yao Serikalini na  kati ya hao 17,682 ni wa shule za msingi ambao  walipelekewa shilingi 13,040,096,775.00 na walimu 5,485 ni walimu wa shule za sekondari ambao walipelekewa shilingi 6,169,789,992.00.  Walimu waliopo katika Sekretarieti za Mikoa walipelekewa shilingi 22,789,680.00 na kufanya jumla ya fedha zilizopelekwa kufikia jumla ya shilingi 19,232,676,447.00. Madai ya malimbikizo ya mishahara ya kiasi cha shilingi 25,643,594,545.43.00 yanalipwa kwenye mishahara ya walimu husika kupitia mfumo wa malipo ya mishahara ya watumishi wa Umma.  Hadi Aprili 2012 jumla ya shilingi 16,567,655,437.34 zilikuwa zimelipwa. Aidha, jumla ya shilingi 2,642,231,329.78 zilikuwa zimebaki.

45.       Mheshimiwa Spika, OWM-TAMISEMI kwa miaka miwili mfululizo iliendelea kuratibu uendeshaji wa mashindano ya michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari (UMISSETA). Michezo iliyoshindaniwa ni riadha, mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa pete, mpira wa wavu, bao, meza, mpira wa kikapu. Aidha, kulikuwepo mashindano ya taaluma na ubunifu kwa Shule za Msingi.  Mashindano ya UMITASHUMTA yanahusisha wanafunzi kutoka Tanzania Bara pekee wakati UMISSETA iliwahusisha wanafunzi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM)

46.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, ruzuku ya uendeshaji shule (Capitation grant) iliyotengwa kwa elimu ya msingi ni shilingi bilioni 50. Hadi kufikia mwezi Mei, 2012 kiasi cha shilingi bilioni 10.1 kimetolewa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Fedha hizo zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ukarabati wa majengo ya shule, kuendesha mitihani ya ndani na uendeshaji wa shule za msingi. Aidha, shilingi bilioni 30 ambazo ni sehemu ya CAPITATION zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu vya kiada kwa ajili ya Shule za Msingi.


Fedha za Chenji ya Rada

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipokea fedha za fidia ya ununuzi wa Rada kiasi cha Paundi milioni 29.5 kutoka Serikali ya Uingereza sawa na shilingi bilioni 72.3 za Kitanzania ambazo zitatumika kuimarisha Elimu ya Msingi Nchini.  Kati ya kiasi hicho, ilikubalika shilingi bilioni 54.2 sawa na asilimia 75 zitumike kununua vitabu vya kiada kwa shule za msingi na shilingi bilioni 18.1 sawa na asilimia 25 itumike kutengeneza madawati kwa shule za msingi.  Ununuzi wa vitabu vya kiada utazingatia vitabu ambavyo viliainishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwaka 2009 hata kabla ya fedha za fidia ya rada hazijajulikana kuletwa nchini ambapo vitabu viwili viwili vya kiada viliteuliwa kwa kila somo. Kila shule ya msingi nchini itapata vitabu hivyo.  Mazungumzo yamefanyika ili kila Mchapishaji atakayepewa zabuni awajibike kufikisha vitabu hivyo kwenye shule.  Ili kuimarisha uwazi vitabu vitapokelewa shuleni na Kamati ya Shule mbele ya wanafunzi, wazazi na Serikali ya Kijiji/Mtaa.  Mahali kamili kwa wachapishaji yatatolewa baada ya kupata uthibitisho toka Mikoa na Halmashauti zote kwamba vitabu vimepokelewa kwa ubora na idadi iliyokubalika.

Mheshimiwa Spika, shilingi bilioni 18.1 zitatumika kutengeneza madawati kwa shule za msingi. Kiasi cha madawati yatakayopatikana hakitatosha lakini kitasaidia kupunguza tatizo kubwa la madawati linalozikabili shule zetu za msingi nchini.  Awali ilipendekezwa kuwa madawati hayo yanunuliwe na kusambazwa kwenye Halmashauri zilizokuwa na upungufu mkubwa wa madawati yaani upungufu unaofikia madawati 100,000 au zaidi.  Hata hivyo, Serikali imetafakari tena na kuona kwamba kigezo cha upungufu mkubwa pekee si kigezo bora cha kutumia katika kugawa madawati.  Kutokana na uamuzi huu, kila Halmashauri itapata mgao wa madawati.




Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES)

47.       Mheshimiwa Spika, kazi za Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari Awamu ya Pili (MMES II) zilizotekelezwa katika mwaka 2011/12 ni kufanya uchambuzi yakinifu wa shule 264 ambazo zitafanyiwa ukarabati mwaka 2012/13; kuandaa moduli za mafunzo ya Bodi za Shule na Waratibu Elimu Kata ili kusimamia uendeshaji na uratibu wa  elimu ya Sekondari. Mafunzo yataanza katika mwaka wa fedha 2012/13. Maafisa  Elimu wa Mikoa 25, Maafisa  Elimu Taaluma wa Mikoa 25, Maafisa Elimu wa Sekondari wa Halmashauri 133, Maafisa Elimu Taaluma 133 wa Halmashauri na Wakuu wa Shule 3,435 wa shule za Serikali na zisizo za Serikali walipata mafunzo kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari Awamu ya II (MMES II).

48.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 22.9 kwa ajili ya uendeshaji wa Shule za Sekondari. Hadi kufikia Machi, 2012 jumla ya shilingi bilioni 7.6 zimetolewa na kupelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya Capitation ya shule ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vitabu vya kiada na vifaa vya maabara.

49.       Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mwaka 2012/2013 ni kufanya ukarabati wa shule 264 zilizoanishwa; Kutoa mafunzo kwa Bodi za Shule, kuendesha michezo ya UMISSETA; Kushiriki katika kufuatilia utoaji wa elimu ya Sekondari katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuchukua hatua stahiki.

Programu ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu na Ardhi Oevu

50.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 Programu ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu (PFM) ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kuendeleza usimamizi shirikishi wa misitu katika baadhi ya Halmashauri za Mikoa ya Morogoro, Iringa Njombe, Mbeya, Lindi Tanga, Ruvuma, Rukwa, Lindi, Kigoma, Mtwara, Mara, Shinyanga, Dodoma, Pwani na Kagera chini ya ufadhili wa DANIDA na Finland. Kiasi cha fedha kilichotolewa hadi Machi 2012 ni shilingi 490,493,000.00. Fedha hizo zimetumika kuratibu utoaji wa elimu kwa jamii kuhusiana na hifadhi ya misitu na mazingira. 

51.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 Programu Shirikishi ya Usimamizi wa Ardhi Oevu iliidhinishiwa shilingi 758,600,000.00. Kati ya fedha hizo shilingi 158,600,000.00 ni kwa ajili ya uratibu na shilingi 600,000,000.00 zimepelekwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa zinazotekeleza Programu.  Programu hiyo inatekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mikoa ya Arusha, Iringa, Njombe, na Mbeya. Kazi zilizotekelezwa katika Mamlaka hizo ni pamoja na kufanya mapitio ya mwongozo wa usimamizi wa fedha na utekelezaji wa programu na kuandaa mafunzo kuhusu mwongozo kwa watendaji wa Mamlaka. 

Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP)

52.       Mheshimiwa Spika, kwa kutumia bakaa ya fedha ya mwaka 2010/11 na fedha za 2011/12, Halmashauri zimeendelea na uboreshaji wa miundombinu ya masoko ya mazao kwa kujenga jumla ya masoko 84 kwa wanufaika 197,750, barabara za maeneo ya Vijijini (feeder roads) zenye urefu wa km. 263 na madaraja madogo 25 kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa mazao na pembejeo yamefanyiwa ukarabati. Aidha, kwa upande wa miundombinu ya mifugo, jumla ya malambo 27 yamejengwa kwa wanufaika 47,837.  Vilevile Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kuvijengea uwezo vikundi mbalimbali vya wakulima kiuchumi katika maeneo yao na jumla ya wanufaika 17,315 wamepatiwa mafunzo ya uboreshaji wa bidhaa zinazotokana na kilimo ili kuwa na uhakika wa masoko. Pia jumla ya mashamba darasa 4,542 na vikundi 14 vya watumia maji (Water User Association) vimepatiwa mafunzo ya mbinu bora za uzalishaji mazao ya kilimo na mifugo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. 

Mkakati wa Kufufua na Kuendeleza Sekta na Viwanda vya Ngozi

53.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 Jumla ya shilingi 677,000,000.00  zimepelekwa  katika  Mamlaka za Serikali za Mitaa 65 kwa ajili ya kutekeleza mkakati wa kufufua na kuendeleza Sekta ya Viwanda vya Ngozi. Kila Halmashauri imepangiwa kutumia jumla ya shilingi 10,415,384.00 zinazotekeleza mkakati huo. Vikao vya uhamasishaji, mafunzo, warsha na ziara za mafunzo vilifanyika kwa wadau wa zao la ngozi ikiwa ni pamoja na  Wafugaji, Wachunaji, Wawambaji, Wasindikaji, Wachambuzi wa Madaraja na Wafanyabiashara, Madiwani, Maafisa Ugani, Wakuu wa Idara, Viongozi wa Vijiji na Vitongoji.  Uhamasishaji huu umeleta ufahamu juu ya umuhimu wa zao la ngozi na umechangia katika ongezeko la ubora na biashara ya zao la Ngozi. Vilevile, vimeanzishwa  vikundi vya ujasiriamali katika usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za  zao la Ngozi na uundaji wa vyama vya wadau wa zao la ngozi unaoendelea kufanyika katika Halmashauri zote zinazotekeleza Mkakati .

54.       Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2012 jumla ya ngozi za Ng’ombe zilizokusanywa zilikuwa ni  475,639, ngozi za Kondoo ni 94,166 na ngozi za Mbuzi ni  322,249.  Katika mwaka wa fedha 2012/13 jumla ya shilingi 855,900,000.00   zimetengwa  kwa ajili ya Mamlaka za Serikali za Mitaa 65 Tanzania Bara zinazotekeleza Mkakati huu na jumla ya shilingi 25,000,000.00 zimetengwa kwa ajili ya uratibu.

Programu ya Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund)

Mheshimiwa Spika,  Serikali kupitia Mfuko wa pamoja wa Afya katika kipindi cha fedha cha mwaka 2011/2012 imepeleka jumla ya Shs 80.99 bilioni katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa huduma katika zahanati 4,105, vituo vya afya 457 na hospital 112 zinazomilikiwa na serikali ili kuimarisha huduma za tiba na Afya kwa ujumla. Aidha, kupitia mfuko huu shughuli zifuatazo zimetekelezwa: ununuzi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi, kujenga uwezo kwa watumishi wa sekta ya afya wa ngazi zote, usimamizi, ufuatiliaji na uratibu na kuimarisha muundo wa sekta ya afya. Vile vile mfuko huu umesaidia kuimarisha utaratibu wa rufaa kutoka vituo vya afya/zahanati kwenda Hospitali za Wilaya na usambazaji dawa, chanjo na vitendanishi. Mfuko huu pia umetumika kuhakikisha watumishi wanakuwepo katika vituo vya kutolea huduma masaa yote na upatikanaji wa maji, umeme na usafi wa mazingira

Taasisi na Mashirika
Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo

55.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Chuo cha Serikali za Mitaa HOMBOLO kimeendelea na mipango yake ya kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi. Katika kipindi hicho Chuo kiliweza kuanzisha kozi mpya nne hivyo kufanya jumla ya kozi zinazotolewa mpaka sasa kuwa nane kutoka nne za awali. Kozi mpya zilizoanzishwa zinalenga kuongeza wataalamu wa fani ambazo zitasaidia kuimarisha utendaji wa kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kozi hizo ni:-  Astashada ya Maendeleo ya Jamii, Astashahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu, Stashahada ya Maendeleo ya Jamii na Stashahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu.

56.       Mheshimiwa Spika, udahili wa wanafunzi pia uliongezeka kutoka wanafunzi 1,389 mwaka 2010/11 hadi kufikia wanafunzi 2,286 katika mwaka wa masomo 2011/12. Idadi hii ni ongezeko la wanafunzi 897 sawa na asilimia 65 ya wanafunzi waliodahiliwa mwaka wa masomo 2010/11. Chuo kiliendesha mafunzo ya muda mfupi kwa Wenyeviti wa Vijiji 32 vya Halmashauri za Mbinga na Maafisa Watendaji wa Vijiji 20 wa Halmashauri za Misenyi, Magu, Karagwe na Ukerewe, Wakuu wa Idara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Maafisa 6) na Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi.

57.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12 Chuo kilipewa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ikiwa ni ruzuku ya miradi ya maendeleo. Kiasi cha shilingi 426 milioni kimetumika kulipia sehemu ya fidia ya eneo lililochukuliwa na Chuo kwa ajili ya upanuzi, shilingi milioni 300 zitatumika kujenga nyumba mbili (2) za watumishi, shilingi 700 zitatumika katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya na sehemu ya kiasi kilichobakia shilingi 75 milioni kimetumika kuweka samani katika nyumba mpya 15 za watumishi (daraja la A na B).

58.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Chuo kimetenga shilingi milioni 650 kwa ajili ya kulipa fidia. Serikali itaendelea kukiimarisha Chuo kwa kuongeza idadi ya wataalamu mbalimbali ili kiweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Wakala wa Usafiri wa Haraka (Dar es Salaam Rapid Transit - DART)

59.       Mheshimiwa Spika, usafiri wa haraka Dar es Salaam (DART) ni Mkakati wa Serikali wa muda mrefu utakaotumia mabasi makubwa kupitia njia maalum katika Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano. Usanifu wa kina wa mradi awamu ya pili (Kilwa Road) na ya tatu (Nyerere Road) umekamilika. Ujenzi wa Miundombinu awamu ya kwanza katika barabara ya Morogoro umeanza kutekelezwa. Wakala unakamilisha usanifu wa kina wa mfumo wa DART awamu ya 2 na 3 yenye urefu wa kilomita 42.3.

60.       Mheshimiwa Spika, gharama za ujenzi wa mfumo huu awamu ya kwanza kupitia Benki ya Dunia ni dola za Marekani milioni 225.37 na Serikali ya Tanzania hadi sasa imechangia shilingi bilioni 11.5. Sekta Binafsi inatarajiwa kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 40.9. Aidha, hivi sasa mradi umefikia hatua muhimu ya utekelezaji baada ya kusainiwa kwa mkataba kati ya Kampuni ya Ujenzi ya STRABAG kutoka Ujerumani na Serikali tarehe 22 Desemba 2011. Wakala pia umelipa fidia awamu ya kwanza katika kituo cha mabasi Ubungo kwa kutumia shilingi milioni 500 zilizokuwa zimetengwa mwaka 2011/12. Matarajio kwa sasa ni kwamba ifikapo mwaka 2014 sehemu kubwa ya mradi itakuwa imekamilika na kuanza kutumika.



Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF)

61.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2011/12, Mfuko uliandikisha wanachama wapya 10,195 kati ya lengo la kuandikisha wanachama 10,216. Hadi Machi 2012, Mfuko ulikusanya michango ya wanachama shilingi bilioni 66 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 87.5.  Katika lengo la uwekezaji, Mfuko uliwekeza shilingi bilioni 111.46 kati ya lengo la kuwekeza shilingi bilioni 163.83. Vilevile, katika kipindi hicho Mfuko ulipata shilingi bilioni 20.37 kutokana na uwekezaji uliokuwepo kati ya matarajio ya kupata shilingi bilioni 43.81 kwa mwaka.

62.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 Mfuko unategemea kuandikisha wanachama wapya 11,591 na kufanya idadi ya Wanachama kuongezeka kutoka 92,269 Juni 2012 hadi  103,860 ifikapo Juni  2013. Mfuko umelenga kukusanya shilingi bilioni 107.66 kutokana na Michango ya wanachama na kuwekeza shilingi bilioni 196.74 kwenye vitega uchumi mbalimbali na kulipatia Shirika mapato ya shilingi bilioni 42.67. Pia Mfuko unategemea kutumia kiasi cha shilingi bilioni 35.27 kwa ajili ya malipo ya mafao.  Aidha, Mfuko katika kutekeleza Sheria mpya ya Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii, umepanga kuendelea na utafiti wa kubainisha utaratibu bora wa kutoa mafao ya elimu na njia mwafaka ya kupanua wigo kwa sekta isiyo rasmi.

Shirika la Elimu Kibaha

63.       Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza malengo yake, Shirika la Elimu Kibaha kwa mwaka 2011/12 limeweza kutoa Elimu na malezi bora kwa wanafunzi 2,920. Wanafunzi 915 walipata elimu ya msingi (wavulana 447 na wasichana 468), Wanafunzi 1,532 walipata Elimu ya Sekondari Kidato cha Kwanza hadi cha Nne (Wavulana 855 na Wasichana 677) na wanafunzi 373 ambao wote ni Wavulana walipata Elimu ya Sekondari Kidato cha Tano na Sita. Aidha, vitabu  914  vilinunuliwa, Walimu 126 walilipwa posho ya nauli wakati wa likizo, walimu  26  walikuwa wakiendelea na masomo katika ngazi ya Shahada na Walimu  11 waliajiriwa. Shirika lilitoa huduma ya Maktaba kwa wadau 34,112, wanaume 27,706 na wanawake 7,406.

64.       Mheshimiwa Spika, Elimu ya nadharia na vitendo kupitia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi ilitolewa kwa wanachuo 408 (wavulana 245 na wasichana 163). Mafunzo yaliyotolewa ni Kilimo na Mifugo, Ujenzi na Useremala, Ushonaji na Upishi, Ufundi wa Magari, Uundaji na Ufuaji Vyuma na Umeme wa Majumbani.  Mafunzo ya muda mfupi yalitolewa kwa wadau 255.  Mafunzo hayo yalikuwa ni udereva, ujasiriamali, kilimo cha bustani, kilimo cha uyoga, kutengeneza tofali na kuchakata ngozi.

65.       Mheshimiwa Spika elimu ya kinga na tiba kupitia Hospitali Teule ya Tumbi ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ilitolewa kwa wagonjwa 247,985.  Kati yao waliolazwa ni 50,949 (wanawake 33,798 na wanaume 17,151) na wa nje walikuwa 197,036 (wanawake 105,246 na wanaume 91,790). Pia hospitali ilihudumia majeruhi wa ajali za barabarani 2,724.

66.       Mheshimiwa Spika, Shirika pia liliendelea kupambana na janga la UKIMWI. Katika mwaka wa fedha 2011/12, wagonjwa 6,168 (wanaume 2,845 na wanawake 3,323) walipewa ushauri  nasaha na  kupimwa UKIMWI. Wagonjwa 1,051 walisajiliwa katika Kliniki ya kutoa huduma kwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI (CTC). Ujenzi wa upanuzi wa Hospitali ya Tumbi awamu ya pili inayojumuisha ujenzi wa vyumba vya upasuaji, ofisi na sehemu ya mapokezi uliendelea.  

Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa

67.       Mheshimiwa Spika, jukumu la Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ni kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa  kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.  Hadi Aprili, 2012 mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 1.028 imetolewa kwenye Halmashauri tatu za Lushoto, Mbinga na Mtwara Mikindani na kufanya mikopo yote iliyotolewa kufikia jumla ya shilingi bilioni 5.5 ikilinganishwa na maombi yaliyowasilishwa ya jumla ya shilingi bilioni 25.1 tangu Bodi ianzishwe.

68.       Mheshimiwa Spika,  katika kipindi hicho michango ya Akiba ya jumla ya shilingi milioni 322.4  imewasilishwa kati ya shilingi bilioni 1.1 zilizokadiriwa na kufanya michango yote ya Akiba kufikia jumla ya shilingi bilioni 4.9 ikilinganishwa na kiasi kilichopaswa kuchangwa cha jumla ya shilingi bilioni 5.6. Kuhusu Mikopo na riba, jumla ya shilingi milioni 279.7 zimerejeshwa na kulipwa kati ya shilingi milioni 958 zilizokadiriwa. Uwasilishaji wa Michango na marejesho ya mikopo umekuwa siyo wa kuridhisha. Hadi tarehe 15 Aprili, 2012, Bodi inazidai Halmashauri 64 jumla ya shilingi bilioni 3.1 kwa viwango tofauti kutokana na Michango ya Akiba (MCR) na Mikopo pamoja na Riba.

69.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuchukua hatua za kuufanyia marekebisho muundo wa Bodi. Matarajio ya marekebisho haya ni kuwa na chombo cha fedha cha Serikali za Mitaa kilichoimarika na  kinachojitegemea kwa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuendesha shughuli zake kwa asilimia 100 katika nyanja zote za utumishi, kifedha, na tekinolojia ya habari na mawasiliano.

HITIMISHO

70.       Mheshimiwa Spika, OWM-TAMISEMI inapenda kuwashukuru wadau wote ilioshirikiana nao katika kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2011/12 na inatoa rai waendelee kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya mwaka 2012/13.

No comments:

Post a Comment