Monday, November 5, 2012

HATA INGEKUWA SERIKALI YA CHADEMA

Na: Gabriel Athumani.
DODOMA.



Mwanafalsafa wa zamani nchini Ugiriki, Plato, ni miongoni mwa binadamu waliojaliwa kuwa na uwezo wa kufikiri, lakini akitumia zaidi nadharia za mwalimu wake, Socrates.
Alipokuwa anaangalia juu ya dola wakati ule, aliamini kuwa dola ambayo inaweza kufanya mambo yake vizuri, inaweza kupatikana kama wakiwapo watu makini wa kuingoza.
Akaendelea kusema; na kwa kuwa njia kuu ya mafanikio ni hekima ya kiongozi ambaye anafanya maamuzi kwa ajili ya jamii nzima, basi jamii nzuri itapatikana tu pale Wafalme watakapokuwa Wanafalsafa au Wanafalsafa wamefanywa kuwa Wafalme.

Nimetumia nukuu hii ikiwa ni mwendelezo wa mjadala wangu wa wiki iliyopita nilipojadili kuhusu baadhi ya wanasiasa kujiona wanajua kila kitu kuliko wengine. Kujiona ni wababe wasioweza kuguswa na yeyote na kwamba wanaweza hata kuropoka chochote na wasihojiwe.

Nimetumia maneo hayo ya Plato kuelezea umuhimu wa hekima katika kuongoza watu, umakini wa viongozi ili uwe na Taifa zuri na uwezo wa kiongozi kuchambua mambo kwa kutumia elimu na ufahamu wake.

Katika wiki iliyomalizika tumeshuhudia mambo yanayofanana kidogo na mjadala wangu wa wiki iliyopita, na yanayolandana na muono wa mwanafalsafa, Plato. Katika habari za magazeti ya hapa nchini, moja wapo iliyokuwa imebeba uzito ni ile Chadema kumwandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete. Kuna magazeti yalikuwa na kichwa cha habari “Chadema ‘wamlima’ barua JK”.

Habari nyingine, ni ile ya Chadema kumsusia Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na ile ya Chadema kuhamasisha maandamano Iringa. Lakini kubwa kuliko yote ni pale Mchumba wa Dk. Wilbroad Slaa, Katibu Mkuu wa Chadema, Josephine Mushumbusi alipoibua tuhuma nzito akidai kuna mpango wa kumuua mumewe kwa sumu au uchawi!

Habari hizo zote, ukisoma kwa umakini, utagundua  jambo moja linalofanana na umuhimu wa maneno ya Plato niliyoyagusia hapo juu.

Tukianza na ile ya Chadema kumwandikia barua Rais. Unachoweza kukiona haraka haraka ni kukosekana kwa hekima, na umakini katika kufikia uamuzi na kutoa tamko kama lile. Angalia lugha ya kibabe inayotumika kumtisha na kumwamrisha Rais, angalia mambo yaliyosababisha tamko lile.

Unaweza kujiuliza, wao ni akina nani mpaka wafikie hatua ya kumtaka Rais afanye watakavyo na si watakavyo Watanzania au atakavyo yeye aliyepewa mamlaka na Katiba kufanya uteuzi na kufukuza. Mbaya zaidi, amri zote hizo kwa Rais zinaishia kwa masharti ya kumtisha ati; “Iwapo Serikali haitazingatia, Chadema kitawaongoza   wananchi kwa njia ya kidemokrasia ikiwamo maandamano kuishinikiza”. Ni kukosa hekima na umakini.

Kama hiyo, haitoshi Chadema hao hao, wiki iliyopita walisusia semina iliyokuwa imeandaliwa na John Tendwa, Msajili wa Vyama vya Siasa iliyovishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine. Wameapa kutoshirikiana naye mpaka pale Rais atakapomuondoa katika nafasi aliyonayo.

Hivi, kama kweli busara ilitumika, kumsusia Tendwa ambaye ndiye anayefahamika kisheria, halafu wakati huo huo, wanadai wataendelea kuiheshimu Sheria ya Vyama vya Siasa, akili ya kawaida inaonyesha kuna mapungufu makubwa katika safu ya uongozi ya Chadema. Msajili wa Vyama vya Siasa anatajwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa ingawa si kwa jina la Tendwa, lakini aliyepo kwa mujibu wa Sheria hiyo ndiyo huyo. Sasa wanaiheshimu sheria ipi. Hekima ni muhimu katika uongozi.

Aidha, mchumba wa Dk. Slaa, Josephine naye amekuja na kali nyingine kama iliyowahi kutolewa na Kamati Kuu ya Chadema hivi karibuni. Josephine ambaye katika habari hiyo inadaiwa yupo nje ya nchi, amenukuliwa akiandika kuwa kuna vikao vya watu ndani ya Serikali vyenye lengo la kutaka kummaliza Dk. Slaa kwa njia yoyote ile.

Amenukuliwa “Wanaamini kwamba Dk. Slaa ndiye mzizi wa Chadema na anaweza kuiangusha CCM 2015. Wameona mazingira ya kuchakachua 2015 ni magumu sana”. Pia katika taarifa yake hiyo, Josephine anahusisha sumu na uchawi kuwa vitatumika katika harakati hizo za kummaliza ‘mumewe’.

Anasema; “Kwenye kikao chao cha kidhalimu, mmoja wao akapendekeza matumizi ama ya uchawi au sumu inayoua taratibu. Huyu aliyependekeza anahofia kuwa njia yoyote itakayofanana na nyingine italeta kelele na dunia nzima itagundua. Anajaribu kuwashawishi wenziwe waachane na hiyo, isipokuwa watumie njia hizi mbadala; sumu au uchawi.”

Habari zote hizo hapo juu kwa muhtasari utagundua jinsi watu hao walivyokosa hekima na umakini katika matamshi yao. Kwa wenzangu kutoka makundi mbalimbali kati jamii hii ya Kitanzania, tulisaidie kundi hili la Chadema!

Nasema tulisaidie kwa sababu pamoja na wengi wao kuwa na umri kama wangu, wenye akili isiyochoka, lakini wanaonekana stamina za kisiasa hazipo. Hakuna wanachowaza ni kuitishia Serikali kwa maandamano. Mara Mbunge wa Iringa Mjini anahamasisha wananchi waandamane, kumshinikiza Rais kumuondoa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Michael Kamuhanda!

Haiwezekani kila kukicha, habari ni za kumtishia Rais, Waziri Mkuu, Waziri,  Mkuu wa Mkoa kisa, demokrasia ya upinzani. Hapana. Hakuna nchi wala Serikali ambayo kuanzia Januari mpaka Desemba kundi fulani lipo kuiyumbisha ili ishindwe kufanya kazi zake. Hakuna Serikali inayoweza kufanya kazi kwa matamko ya kuiamrisha kutoka vyama vya siasa.

Hakuna Rais anayefanya kazi kwa kuamrishwa na Kiongozi au Kamati Kuu ya chama asichokiwakilisha. Hata kama Serikali hii ingekuwa ya Chadema, isingefanya kama inavyotaka sasa viongozi wa Serikali ya CCM wafanye.

Tuwasaidie akina Freeman Mbowe, Dk. Slaa, John Mnyika na wengine ndani ya Chadema kuwa “ukitaka mbio, agana na nyonga”. Wasijidanganye kwa malengo ya muda mfupi ya kutaka tu kuingia Ikulu. Mikakati inayofanyika sasa inajionyesha wazi si ya kutaka kuongoza nchi bali kuingia Ikulu, wakifika huko ndiyo watajua wenyewe biashara watakayoifanya.

Nasema haya kwa sababu mbili kubwa, mosi; Viongozi wa Chadema wanatumia raslimali nyingi za chama na nje ya chama kuliunda kundi la Watanzania wabishi, wapenda maandamano, wapinga kila kitu hata kama ni kizuri na wakaidi wa amri halali za Serikali na dola. Pili wanategeneza kundi la Watanzania waongo, wanafiki, wazushi, na waropokaji.

Makundi hayo hapo juu yanaundwa kwa kiasi kikubwa na vijana. Vijana ambao tayari wameiva kwa yote niliyoyaorodhesha. Wajue kuwa, hakuna namna Serikali itakayoundwa na Chadema kama ikitokea, inaweza kuyabadilisha makundi hayo mawili. Haitawezekana kwa sababu, vijana hawa na wengine hawawashabikii viongozi wa Chadema kwa sababu wao handsome, au warembo.

Hasira waliyoijaza kwa makundi haya haitakwisha wakiingia madarakani, kwani wameziwekeza katika matarajio ya kesho. Kama leo anaichukia CCM kwa sababu umemwambia hakuna ajira, kesho ukiingia madarakani, bado kukawa hakuna ajira, unatulizaje hasira yake!

Kwa jinsi walivyofuzu somo la kuandamana kwa alama za juu, utawazuia vipi kufanya maandamano kudai kima cha chini cha mshahara kuwa milioni mbili? Jamii iliyofuzu yote yanayofundishwa sasa na viongozi wa Chadema ni ya Watanzania. Hatutegemei Chadema ikiingia madarakani, itakwenda kuchukua Wachina ndio wawatawale.

Ni Watanzania wale wale ambao vijana wengi wako mijini wakifanya biashara ndog ndogo (Machinga) ambao Chadema imewafundisha kuzomea viongozi hata pale wanaposhauriwa mambo yenye manufaa kwao.

Ni vijana wale wale wanaosoma katika shule zetu za Sekondari za Kata mnazoziponda leo, ambazo hawatazitaka tena kwani mlishawaambia hazifai. Ni watanzania wale wale, watakaougua, ambao watataka kila zahanati iwe na mashine ya X-Ray, kwa sababu mlisema inawezekana.

Ni watanzania wale wale, wanaonunua mfuko mmoja wa sementi kwa Sh 20,000 leo, ambao Chadema ikiingia madarakani hawataelewa kama haitauzwa kwa Sh.5,000, lazima wataandamana. Wamefuzu shughuli hiyo. Na ni Polisi wale wale wanaotuhumiwa kuua kwenye mikutano ya Chadema ndiyo watalinda maandamano.

Baadhi ya wanaharakati, wasomi, waandishi wa habari na vyombo vya habari wanaoshabikia yanayoandaliwa sasa na Chadema, wasaidieni viongozi wake kwani, ukipanda bangi utavuna bangi.

Wasaidieni wajue kuwa wao si wajuzi wa kila kitu, wasikilize na wajifunze namna ya kuwaanda wananchi kupokea utawala wao wakiwa wavumilivu, wamoja, na wenye subira. Wasaidieni kuwaambia kuwa wasitengeneze njia za mkato kuingia madarakani, bali wajipange kujua namna ya kuingia madarakani.

Wasaidieni kujua kuwa, wakiingia madarakani hawatashangiliwa kila wapitako, watazomewa na kurushiwa mawe kama walivyowafundisha kufanya hivi sasa. Watafanyiwa vurugu, watatukanwa, wataandikwa vibaya, kupingwa kama wafanyavyo wao.

Chadema kama cha siasa kinachoipa changamoto CCM kwa staili ya kuidhoofisha kwa mbinu chafu, zikiwamo zile za uzushi kama unaofanywa sasa wa kusingizia viongozi wa Serikali na vyombo vya dola kupanga mikakati ya kuwadhuru, kinajitengenezea hatima watakayokuja kuijutia.

Watakwenda vijijini kwa chopa, wananchi watazishangaa, watawashangaa pia akina Dk. Slaa, watagawa kadi mithili ya vipeperushi vya maelezo ya waganga wa kienyeji, watawatukana viongozi wao, watapata burudani ya uongo na uzushi, lakini mwisho wa siku, kila mmoja anatafakuri juu ya maisha yake.

Kutokana na kukosa hekima inayosaidia kujenga jamii nzuri, tumesikia jinsi ufisadi wa kutisha katika Halamsahauri ya Manispaa ya Moshi inayoongozwa na Chadema, ulivyofichuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama. Na kwa kudhirisha jinsi wasivyo makini, Meya wa Manispaa hiyo, anatamka kutoshirikiana na Mkuu wa Mkoa kwa madai ati anatumika kisiasa.

Hivi kweli, msafara wa watu 58 mnakwenda kujifunza Kigali kwa kutumia Sh. 200 milioni kuna tija kweli hapo? Katika hali ya kawaida na haiingii akilini kuwa watu 58 wanakwenda mafunzoni kwa mpigo, huo ni wizi wa fedha za walipa kodi tu na hakuna maelezo mengine.

Na jambo hili, kama lingefichuliwa kwenye Halmashauri inayoongozwa na CCM, albamu nyingine ya ufisadi ingekuwa inauzwa nchini. Ungeimbwa majukwaani, kwenye magazeti, midahalo isiyo na tija na mitandao ya kijamii. Hongera sana Mkuu wa Mkoa, kaza uzi hawana namna ya kuendesha mambo yao bila Serikali kujua kwani fedha ulizookoa si za Chadema, ni za umma.
 
Nafahamu Waafrika tuna hulka ya kudandia mambo bila ya kuyapima na hasa tukihamasishwa na nguvu kutoka nje. Tukiambiwa tufanye mabadiliko, hata kama hatupewi sababu za msingi, tumo! Tunashabikia mambo ambayo hatuyajui kabisa. Mfano ni kama ule wa Uganda, pale Idd Amin alipoipindua Serikali ya Milton Obote.

Waganda wakiamini kuwa Idd Amin ni mkombozi, walimpongeza na waliyashangilia mapinduzi yale ambayo Mganda yoyote, ukimuuliza leo kama yalikuwa na ulazima wowote, ataishia kusikitikia yaliyokuja kutokea baada ya hapo.

Libya yamefanyika mapinduzi yaliyomuua Kanali Muammar Gaddaf, Misri yametokea mapinduzi yaliyomg’oa Hosni Mubarak, Tunisia kadhalika. Mapinduzi haya yote barani Afrika yameshabikiwa hata hapa nchini kwetu, lakini chanzo chake na kufanikiwa kwake ni kutokana na nguvu za nje ya nchi hizo.

Tumeshuhudia jinsi majeshi ya NATO yalivyoshiriki kule Libya. Lakini Waafrika hatujiulizi kulikoni NATO na Gaddaf. Yalitaka kutokea kule Zimbabwe, Rais Robert Mugabe alivyowekewa vikwazo na nchi za Wazungu kulazimishwa akubaliane wanachotaka kuhusu kibaraka wao.

Chadema kama chama cha siasa kina muda na nafasi ya kufanya siasa za kistaarabu. Si uhodari wala sifa kiongozi kuwa muongo, mzushi kwa sababu tu unataka umaarufu. Kujisingizia kutaka kuuawa kisha hutaki kutoa taarifa zako kwenye vyombo vya dola ni kutafuta umaarufu wa kitoto.

Kama viongozi hawatashituka na kuendelea kucheza “CD ya ufisadi” ambayo imechuja, chama kitajikuta kikija na sababu za vichekesho kwa wanachama wake pale watakapokuwa wanashindwa kwenye uchaguzi. 

Watanzania wanataka kusikia au kuona mikakati ya kuwaletea maendeleo na kuondosha kero zao. Hawahitaji kuongezewa kero ya maandamano, wala kusikiliza hadithi za kutunga. Kama nilivyosema Chadema wana muda na nafasi waachane na kutengeneza mabomu ambayo yanaweza kuwalipukia wenyewe. Hata kama wao wangekuwa madarakani, wanayoyafanya sasa ndiyo watakayofanyiwa.

Mungu Ibariki Tanzania.

                     
   

No comments:

Post a Comment