Chama cha Mapinduzi ( CCM) kinatarajia kufanya Mkutano wake
wa kawaida Novemba 11 hadi 13 mwaka huu.
Maandalizi kwa ajili ya Mkutano Mkuu huo ambao utafanyika
katika ukumbi wa Kizota Mjini Dodoma yamekamilika na wajumbe wa Halmashauri Kuu
ya CCM,watatakiwa kuwasili Novemba 9 kwa kikao cha NEC kitakachofanyika Novemba
10.
Wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa Taifa watawasili Mjini Dodoma Novemba 10 kwa ajili ya Mkutano Mkuu
utakaoanza Novemba 11.
Mkutano Mkuu wa CCM utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu ya
CCM na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa vitakavyofanyika Novemba 10.
Mkutano Mkuu wa CCM, Pamoja na mambo mengine unatarajiwa
kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM, Makamu Wenyeviti wa CCM Tanzania Bara na
Tanzania Zanzibar.
Pia Mkutano Mkuu wa CCM Taifa utafanya uchaguzi wa wajumbe
wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa viti 10 Bara na Tanzania Zanzibar pamoja na
kufanya marekebisho ya Katiba wa CCM ya Mwaka 1977 Toleo la 2010.
Aidha ili kukidhi matakwa ya wakati wa sasa, wajumbe wa
Mkutano Mkuu watapokea taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
Mwaka 2010/2015 kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na kuijadili.
Mjadala wa Taarifa hizo utafanyika kwa makundi ili kutoa
nafasi kwa wajumbe kuchangia mawazo yao
na baadae mawazo ya kila kundi kuwasilishwa mbele ya wajumbe wote wa
Mkutano Mkuu na kutoa maazimio ya jumla ya namna bora ya kuendelea mbele.
Taarifa hii imetolewa kwa waandishi wa habari katika kikao na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye Mchana katika ukumbi
wa white house katika ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM Makao Makuu ya CCM, na Tanzania Dodoma.
No comments:
Post a Comment