MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara, imemhukumu Mkazi wa kijiji cha Bwai kata ya Bukoko Tarafa ya Mayani, Fugo Makubi(25) kifungo cha miaka sita jela na viboko sita, baada ya kukiri kosa la kumchoma binti yake (9) jina linahifadhiwa katika sehemu zake za siri kwa kiginga cha moto na kumsababishia maumivu makali na majeraha.
Akisoma shitaki lake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mara, Emmanuel Ngingwana, Mwendesha Mashitaka Inspekta wa Polisi, Eradius Kakoki alisema mnamo Tarehe 19 Disemba 2011 katika kijiji cha Mayani Bwai Musoma Vijijini alisababisha majeraha kwa kumchoma sehemu zake za siri na kiginga cha moto kwa kumwingizia ukeni mlalamikaji.
Mwendesha Mashitaka aliendelea kudai kuwa Makubi alimtuma binti yake kuteka maji na ndipo alipochelewa kwenda na kuanza kumchapa viboko na kuweka kamba kwenye shingo yake kwa nia ya kumnyonga lakini baadae aliacha na kuamua kuchukua kiginga cha moto na kumchoma ukeni madai ambayo mshitakiwa hakuyakiri.
Mara baada ya kusomewa shitaka hilo Mshitakiwa aliulizwa swali la kutenda kosa na Hakimu Mkazi na kukiri kuwa alitenda kosa na kwamba aliingiliwa na shetani na hajawahi kuugua ugonjwa wowote zaidi ya Malaria.
Baada ya mshitakiwa kukiri kosa ilimchukua dakika 10 Hakimu Ngingwana kuandaa hukumu kwa kusoma vifungu vya sheria.
Akisoma hukumu hiyo na kuzingatia upande wa Jamhuri unaosema kwamba Jamhuri haipendi makosa kutendeka alisema kuwa anatoa hukumu hii ili iwe fundisho kwa wazazi wanaowanyanyasa watoto wao badala ya kuwatunza na kuwalea kwa mujibu wa sheria za nchi na kwamba hawajaandika barua kuja duniani ama kuzaliwa nchi Fulani.
Alisema kuwa mtoto anatakiwa aione dunia hii ni salama si kujuta kwamba kwa nini alikuja duniani na mzazi pia aanapaswa kumlinda kuasaidia ama endapo kama amekosea anapaswa kupewa adhabu zingine kama kuchapwa viboko.
“Unafikia hatua ya kumfunua mtoto sehemu zake za siri? kitendo hicho ni aibu na ni manyanyaso makubwa kwa mzazi wa kiume. Watu kama hawa hawafai kurudi katika jamii wanapaswa kuishi sehemu ambayo watapata mafunzo zaidi hafai kuwa mzazi na hastahili kuwepo katika kundi la wazazi.
Alipoulizwa juu ya utetezi wake alisema kuwa anaomba asamehewe kwani shetani alimwingilia.