Wednesday, May 18, 2016

ASKARI AUA

MKAZI Mmoja wa Kijiji cha Nyambono Wilaya ya Butiama katika halmashauri ya Musoma,Thanael Maganira (60) amefariki dunia kwa madai ya kupigwa na askari Mgambo katika kituo cha Polisi cha Saragana.


Kaka wa Marehemu Masunu Kuyenga amesema kuwa ndugu yake alifika kituoni kwa lengo la Kutoa taarifa ya kulipa deni la sh 30,000 alilokuwa anadaiwa na Christina Katuma ambaye alikuwa mpenzi wake kwa madai ya kuwa alitaka kumbaka.


Inadaiwa kuwa baada ya marehemu kufika katika kituo hicho alidai kuwa bado hajafanikiwa kupata sh.15,000 zilizosalia kulipa deni ambapo Mkuu wa kituo koplo Mtui alimwagiza constable Jacob amweke lumande, ndipo vurugu zilipoanzia baina ya askari mgambo na marehemu na muda mchache alitolewa nje akiwa katika hali ya kutojitambua akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.


Majeruhi alipelekwa katika hospitali ya Manyamanyama Wilaya ya Bunda na kupewa matibabu na baada ya muda mchache alifariki dunia,ambapo mwili wake ulipelekwa katika hospitali ya rufaa ya Musoma kufanyiwa uchunguzi.

Katika uchunguzi uliofanywa katika hospitali hiyo na Dk. Regina Msonge unaonyesha kuwa marehemu alipigwa na kuvunjwa bandama.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Ramadhani Ng’anzi amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba watu wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi,akiwemo aliyekuwa mpenzi wake, Christina Katuma na askari Mgambo Burilo Musimu(39)ambapo askari mgambo mmoja anatafutwa.


Tukio hilo lilitokea mnamo mei 15 saa 4 asubuhi ambapo pia kuna madai ambayo hayajathibitishwa yanadai kuwa huyu ni mtu wa nne kupigwa na mgambo pamoja na askari polisi na kupoteza maisha katika vijiji vya Bugoji,Kabhulabula na Nyambono kwa kupigwa katika kituo hicho na kupoteza maisha.