Hali ya Nishati ya Mafuta ya Petroli na mafuta ya taa imezidi kuwa mbaya katika Manispaa ya Musoma, Mkoani Mara ambapo katika visima vyot vya mjini hapo kufungwa kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo muhimu.
Bei ya mafuta kwa sasa mjini hapo yanauzwa kati ya sh.7,000 hadi sh. 10,000 kwa lita moja kutoka kwa walanguzi wa mitaani huku mafuta ya taa kuadimika kabisa hali iliyomlazimu mbunge wa jimbo hilo, Vicent Nyerere (CHADEMA) kufanya ziara na kuona hali halisi ya ukosefu wa bidhaa hiyo ya mafuta.
Baadhi ya vituo ambavyo alitembelea na kukutana na uongozi wa vituo walisema kuwa mafuta yamewaishia tangu siku ya jumatano na wengine siku ya alhamisi na kudai kuwa bidhaa hiyo itapatikiana kuanzia jumanne mwaka ujao wa 2012 kutokana na ukosefu katika maghala wanayochukulia.
Meneja wa kituo cha kampuni ya White Said Fundikira alisema kuwa wao huagiza mafuta jijini Mwanza katika kituo cha GAPCO na kudai kuwa wamew3asiliana kwa njia ya simu na kuambiwa kuwa anaweza kupata mafuta siku ya jumanne au jumatano mwakani.
“Najitahidi tuone tunanusuru upungufu huu lakini jitihada zinagonga mwamba kwani tumeshaambiwa hadi mwakani na hakuna jinsi tunasubiria hadi watakapotuletea na akiba yetu imeisha jana (juzi),”alisema Fundikira.
Naye mkurugenzi wa kituo cha Kiraba Kampani Shamsa Kiraba alimeioma EWURA kujipanga na kujidhatiti ili kuona hali haiwi mbaya nchini kutokana na ukosefu huu ambao unaendelea sehemu mbalimbali nchini na kusababisha kushuka kwa uchumi wa nchi na maisha kupanda.
“EWURA ijipange vizuri na kuona ni jinsi gani wanaweza kutatua tatizo hilo kubwa la uhaba wa mafuta nchini lakini ingiwa kuna tuhuma nyingi zinaelekezwa kwetu sisi wauzaji naweza kusema katika kituo chetu sisi hata kama bei wa bidhaa tumenunua kwa bei ya juu na siku ya pili bei inashuka hatujali tunauza kwa bei hiyo mpya elekezi na sio kuficha mafuta,” Kiraba.
Pia ziara hiyo ya mbunge ilifika hadi kwa baadhi ya watumiaji wakubwa wa bidhaa hiyo waendesha pikipiki maarufu bodaboda katika kituo cha Nyasho ambapo hawakusita kueleza hasira zao na kupaza sauti kwa wauzaji wa mafuta mjini hapo kilichosababisha pikipiki kubakia tatu badala ya 27.
Mmoja wa dereva wa bodaboda Bakari Bega alisema kuwa wanapata usumbufu mkubwa kutoka kwa wauzaji hao kwani wanatumia mwanya huo wa upungufu wa mafuta kuuza kwa bei ya juu hasa kuwapa kuwapa walanguzi na kuuza kwa bei ya juu.
“Hapa kwanza kazi hakuna hata pesa imeshakosekana kwetu pamoja na hilo tunaomba serikali ya Manispaa ya Musoma ikakague baadhi ya vituo vya mafuta watakuta kuna mafuta yapo ila ndio hivyo wanataka kupata faida kubwa kwani jioni wanafungua kwa wizi na kuuza bei ya s. 3,000 kwa lita,”alisema Bega.
Madereva hao hawakusita kutaja kituo kimojawapo ambacho kinauza mafuta kwa siri kinachojulikana kwa jina la Petrolux kinachomilikiwa na Zembwela ambapo mbunge Nyerere hakusita kwenda kujionea ambapo msemaji wa kituo hicho Justine Dida alikanusha ingawa alionekana kujikanyaga kwa kusema kuwa kituo hicho kiliishiwa mafuta tangu siku ya jumatano saa 9 jioni wiki hii huku mmoja wa wateja wake alipouliza alisema kuwa mafuta yameisha jana asubuhi.
“Huo ni uongo hatuna mafuta je? Wewe mwandishi unajua mafuta ya petrol twende nikakuoneshe kama utayaona maana naona mnanilazimisha kuwa yapo mimi nimesema hakuna mafuta hakuna jingine,”alisema kwa jaziba baada ya kuona amebanwa kwa maswali.
Wakati huo huo wakati tupo katika kituo hicho dereva wa gari lenye namba T 726 BMT, Christopher Paulo alikutwa akiweka mafuta katika gari lake ambayo yalikuwa yamehidhadhiwa kwenye dumu na alipoulizwa alisema kuwa mafuta hayo ameyatoa Buhemba Musoma Vijijini ambako alinunua kwa sh. 3,000 kwa lita.
Nao madereva wa Bajaji walisema kuwa hali kwao ni ngumu kwani katika kituo chao kuna jumla ya bajaji 25 lakini kwa sasa kuna bajaji nne tu ndizo zinazofanya kazi kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo ya mafuta.
“Hapa kuna jumla ya bajaji 25 lakini kwa sasa kuna bajaji nne tu zinazofanya kazi kwa maana hiyo maisha yameshaanza kuwa magumu kutokana na kukosekana kwa mafuta ya petroli kwa hivyo hata bei ya kusafirisha mizigo imepanda nayo kwa kilometa 8 tunatoza kati ya sh. 20,000 hadi 25,000 hali inayofanya kugombana na wateja wetu,”alisema Lazaro Kumburu mmoja wa madereva wa bajaji.
Baada ya ziara hiyo Mbunge Nyerere alisema kuwa EWURA inabidi itoe tamko kama bei ya mafuta imepanda kabla ya mwakani kwani tetesi nyingi zinasema kuwa bei ya mafuta itapanda kwa kiwango Fulani hivyo kwa hali hii wananchi wetu watapata shida kwa kipindi hiki chote.
“EWURA inabidi itoe tamko haraka iwezekanavyo kunusuru hali mbaya ya mji wetu kwani hata usafiri wa watu wa chini wanaotumia pikipiki utakuwa wa taabu sana na watalipa nauli kubwa hivyo tamko lao ndio ukombozi wa wana Musoma,”alisema Nyerere.
Gazeti hili wiki iliyopita iliandika habari ya ukosefu wa nishati hiyo kuanzia siku ya mkesha wa Krismasi ambapowakazi wa mji huo wamelazimikakusheherekea sikukuu ya Krismasi huku mji huo ukighubikwa na uhabamkubwa wa nishati ya mafuta ya Petroli ambayo imesababisha kupanda beina kuuzwa kwa walanguzi tu.
Wiki hiyo bei ya mafuta ilipanda kutoka sh. 2,199 bei halali iliyopangwa na EWURA hadi sh. 5,000 kwa lita lakini kwa wiki hii imepanda na kuuzwa kati ya sh. 7,000 hadi 10,000 kutokana kuadimika kwa nishati hiyo hali iliyiosababisha hadi bei yausafiri wa pikipiki maarufu bodaboda kupanda 2,000 kwa masafa ya mjini na nje ya mji kufikia hadi 5,000.