Monday, April 28, 2014

Hotuba ya DC-Angeline Mabula 50 ya Muungano



HOTUBA YA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR WILAYA YA BUTIAMA ILIYOTOLEWA NA DC-ANGELINE MABULA 26/4/2014

Mhe. Mwenyekiti wa CCM (W),
Wahe. Wenyeviti wa Halmashauri,
Viongozi wa Madhehebu ya Dini,
Viongozi wa vyama vya Siasa,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.

Bwana ni mwema.

Ndugu Wananchi, Awali ya yote napenda kuungana na watanzania wote kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutufanya kuendelea kuwa na amani na utulivu pamoja chokochoko nyingi zinazofanywa na wachache. Tumekuwa na mafanikio makubwa katika Nyanja za kiuchumi na Huduma za jamii tukiwa ndani ya Muungano. Hatuna budi sote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Baraka na ukarimu wake. Aidha niwashukuru nyote mlioacha shughuli zenu nakuja kuungana nasi katika siku hii muhimu katika taifa la Tanzania, nasema asanteni sana.
Ndugu wananchi, tunapoadhimisha Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kauli mbiu inasema “Utanzania wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha” kitaifa maadhimisho yanafanyika jijini Dar es Salaam, Mgeni rasmi ni Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutafakari kwa kina kauli mbiu hii nakuiweka katika matendo.
Ndugu wananchi, Kwetu sisi wanabutiama, hatuna budi kutafakari namna ambayo tunapaswa kujipambanua katika kuonyesha kuwa, tunayo dhamana kubwa yakuendelea kutunza heshima katika kuenzi fikra za waasisi wa muungano, hayati baba wa Taifa Mwl. J.K Nyerere aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume. Je tunawaenzi waasisi hawa kwa namna gani, ukizingatia kuwa mmoja wao anatokana na wanabutiama.

Takwimu za idadi ya watu zinaonyesha kuwa 91% ya watanzania wamezaliwa baada ya Muungano, hivyo ni wazi wengi wao hawaujui kwa undani Muungano huu. Ni jukumu la wazee wetu sasa kama ambavyo leo wametukumbusha na kutuasa masuala muhimu juu ya muungano wetu. Wapi tulikotoka, tulipo na wapi tunakwenda Nijukumu la kila mmoja wetu, kuhakikisha vijana wanajikita katika uzalendo zaidi. Mfano mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambayo yamerejeshwa tena baada yakusitishwa kwa muda mrefu, ni chuo tosha kwa vijana kuwajengea uzalendo wa nchi yao.

Ndugu Wananchi, tukumbuke kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu kadhaa, nitataja chache tu;

1. Kuwepo kwa mahusiano ya karibu kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususani baina TANU na ASP.


2. Moyo wa kuwa na Muungano wa Afrika hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania utaifa katika ukanda wa Afrika Mashariki walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika.

3. Mwingiliano wa kijamii ambapo wengi wameoleana bara na visiwani, ushirikiano wa kibiashara watanzania wanaendesha biashara zao pande zote za muungano bila hofu, kwa uhuru zaidi pasipo hofu yoyote.

4. Kuimarisha mshikamano na umoja ili kulinda uhuru na mapinduzi kwa kuhakikisha usalama wan chi yetu, nakutoruhusu tena wakoloni kurudi.

Ndugu Wananchi, sote ni mashuhuda kuwa, kuna baadhi ya watanzania wenzetu wameanza kulewa amani, utulivu na demokrasia tuliyo nayo. Vijana wasomi tunaowategemea kuwa dira ya taifa hili wanafanya uchambuzi usio na manufaa kwa taifa hili. Kauli zao zinaonyesha wazi huenda kuna msukumo wanaoupata kutoka nje ya nchi ili kuvuruga amani. Wapo baadhi ya watanzania wanaoubeza muungano wetu, kikao cha bunge maalumu la katiba kilichokuwa kinafanyika mkoani Dodoma, yaliyojiri huko ni aibu tupu hata huwezi kuyataja hadharani.


Suala la kuwa na Serikali mbili, tatu au moja siyo kipau mbele cha watanzania walio wengi. Watanzania wanahitaji huduma za uhakika za jamii na kiuchumi, usalama wa mali zao, maisha yao na pia kuwa na umoja, amani na utulivu endelevu.

Aidha ni vyema tujiulize katika dunia ya leo ni muungano wa nchi gani ambao umedumu kwa muda mrefu zaidi na una utulivu kama tulivyo watanzania! Ukiacha mataifa makubwa kama marekani na kwingineko.


Nitoe mifano michache tu kwa nchi zilizojaribu kuungana na baadae kusambaratika; Mfano ni Muungano wa Senegal na Gambia (SENEGAMBIA) muungano ulidumu kwa miaka 7 tu ulianza Julai, 1982 ukavunjwa mwaka 1989. Muungano wa Syria na Misri ambao haukufika mbali, Marehemu Gadaffi alikuwa anahitaji muungano lakini ilishindikana, vilevile Muungano wa Kisovieti ambao ulisambaratika na mingine mingi. Watanzania tuna lulu ambayo ikituponyoka katu hatutaipata tena.


Ndugu Wananchi, Awali wakati muungano unaanzishwa kulikuwa na mambo 11yaliyokuwa yameanishwa katika makubaliano. Kutokana na mahitaji ya ndani ya wananchi yaliyolenga kuunganika kwa mambo mengi zaidi pamoja na mabadiliko yaliyokuwa yanaendelea kutokea ulimwenguni baada ya Muungano, ikiwemo kuundwa kwa “EAC” 1967, kuvunjika kwa “EAC” 1977, na hivyo kukasimiwa kwa Serikali ya Muungano mambo yote yaliyokuwa yanasimamiwa na “EAC”.
Aidha uwepo kwa mfumo wa vyama vingi 1992, mambo ya muungano yaliongezeka kufikia 22.
Mambo hayo kwa kuyataja kwa uchache ni; Katiba na Serikali ya Muungano, Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka juu ya mambo yanohusika na hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji, Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje, Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha, Bandari mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.


Ndugu wananchi, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 – 2015, Ibara ya 183, imeanisha masuala ya muungano yenye lengo la kuimarisha Muungano, Serikali imeelekezwa kujenga mazingira endelevu na kuimarisha fursa za kiuchumi miongoni mwa Wananchi wa kila upande, ili waone na kuamini kwamba, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar siyo tu ni ngao madhubuti ya Umoja, Amani na Mshikamano wao, bali pia ni daraja la kuwafikisha katika azma yao ya kuondokana na umaskini na kuharakisha maendeleo yao na Taifa kwa jumla.
Ndugu Wananchi, pamoja na baadhi ya watu kubeza muungano wetu, Serikali imeweza kutekeleza mambo mengi ndani ya Serikali ya muungano, miongoni mwa mambo hayo ni:-

• Kuimarisha utendaji wa Kamati ya Pamoja ya kutatua changamoto za Muungano kwa kuandaa utaratibu madhubuti wa vikao vya Kamati na utekelezaji wa haraka wa maamuzi yanayofikiwa; mfano hoja za marekebisho ya Sheria za Kodi, Sheria za Usajili wa Vyombo vya Moto, hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu.
• Kuboresha uchangiaji na mgawanyo wa mapato ya Muungano; Tume ya Pamoja ya Fedha imekamilisha mchakato wa kitaalamu wa kuchambua na kupendekeza vigezo vya mgawanyo wa mapato na uchangiaji wa gharama za Muungano.
• Kuzifanyia mapitio na uboreshaji Sheria na Kanuni za Fedha zinazotawala ukusanyaji wa mapato chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), upande wa Tanzania Zanzibar, kwa lengo la kukuza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato hayo;
• Kuboresha Sheria, Kanuni na taratibu za ajira ya Watumishi katika Taasisi za Muungano ili utumishi huo uwe na sura mwafaka ya ki-Muungano;
• Kuimarisha utaratibu wa kuandaa na kutekeleza mikakati na mbinu za pamoja zenye lengo la kuinua uchumi wa pande zote mbili za Muungano;
Mikakati na mbinu za pamoja zimeandaliwa ili kuinua uchumi wa pande zote mbili za Muungano. Mikakati ya MKUKUTA na MKUZA imeandaliwa na kutekelezwa na pande zote mbili za Muungano.
• Miradi ya Maendeleo imeendelea kutekelezwa na kunufaisha pande zote za Muungano. Mfano wa Miradi ya Maendeleo iliyoandaliwa na kutekelezwa pande zote mbili ni Mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani ya Tanzania (MACEMP).
Ndugu Wananchi, Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza masuala ya Muungano, zimejitokeza changamoto mbalimbali zikiwemo za kuuelimisha umma kuhusu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Aidha, Serikali inatambua kuwa zipo changamoto katika kumaliza vikwazo vinavyokwamisha shughuli za Muungano kwa mfano; Suala la ajira, suala la wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili, kuangalia uwezekano wa kuondoa kodi ya ziada ya asilimia mbili inayotozwa kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi na kuimarisha ushirikiano katika suala la vipimo na mizani ambako kumejadiliwa changamoto zinazojitokeza na namna ya kukabiliana nazo na kuainisha maeneo ya ushirikiano ambayo ni mikataba ya kimataifa, mikutano, mafunzo na Miradi ya pamoja. Dhamira ya Serikali zetu mbili ni kuondoa vikwazo hivyo kwa kuhakikisha kwamba, vinatatuliwa ipasavyo ili Muungano uendelee kuwa imara. Dawa si kuongeza Serikali nyingine
Ndugu Wananchi, Kama ilivyo kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano “Utanzania wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha” tukumbuke kwamba hakuna kitakacho dumu bila kuwa na amani na utulivu.
Tukemee na kuwabeza wale wote wanaoleta chokochoko zinazoenezwa hivi sasa na tujiepushe na kutoa kauli ama lugha za kashfa kwa waasisi wa nchi hii, ambao historia waliyoiweka hakuna anaeweza kuifikia hasa kwa kizazi cha sasa.
Ndugu wananchi, Hivi karibuni wilaya yetu tumekubwa na matukio kadhaa ambayo yanafanya amani, utulivu na mshikamano kuanza kupotea. Kamwe tusitoe nafasi kwa watu wachache wanaotaka kututia doa, wilaya yenye historia na heshima kubwa ndani na nje ya nchi. Rai yangu kwenu wana Butiama tukatae kadhia hii ambayo si tu kwamba inatutia doa bali inapunguza heshima ya taifa kwa ujumla wake. Tutoe taarifa kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama pale tunapopata taarifa zenye kuashiria uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa haki za binadamu. Ni ukweli usiopingika kuwa, changamoto kubwa tuliyonayo katika wilaya yetu niushiriki mdogo/duni wa jamii katika suala zima la ulinzi na usalama wa watu, mali na rasilimali zetu, na uvivu uliokithiri.
Ndugu wananchi, niwaombe wote kwa pamoja tuendelee kukemea suala hili ili kurejesha imani wa akina mama ambao wameanza kukata tamaa kufanya kazi za maendeleo. Wazee wangu mtakuwa mashahidi kuwa mambo haya yanatokea sasa na huko nyuma hamkuwahi kuyaona.
Ndugu Wananchi, Matukio yanayoanza kushamiri wilayani kwetu ni pamoja na haya yafuatayo:-
• Matukio ya mauaji kwa visa mbalimbali
• Mauaji yanayohusishwa na imani za ushirikina na hasa yakilenga akinamama.
• Wananchi na hasa vijana kutopenda kufanyakazi zakujipatia kipato na uhakika wa chakula na hivyo kutegemea chakula cha msaada mara kwa mara
• Vijana wengi kukosa uzalendo na kutaka utajiri wa haraka haraka
Ndugu Wananchi, Serikali inahimiza uwajibikaji wa wananchi, watendaji na viongozi wa vijiji kuhusu masuala ya ulinzi na usalama wa maeneo yao (kuwekeana mikataba) kuhimiza ulinzi wa sungusungu, uanzishwaji wa madaftari ya wageni kwenye vitongoji na vijiji, kuhimiza matumizi ya wazee na viongozi wa Dini, katika kukemea maovu. Aidha kufuatilia kwa karibu nyendo za waganga wa jadi na kuwahakiki pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wapiga ramli. Wakurugenzi wa Halmashauri kuwekeana mikataba na WEO’s na VEO’s wa maeneo yenye matatizo maalum kwamba kama wizi wa mifugo, ujambazi na uhalifu utajitokeza kwenye eneo husika, WEO au VEO wa eneo hilo awajibishwe.
Ndugu Wananchi, Bila shaka wote tunatambua mabadiliko mengi yaliyotokana na matukio kadhaa katika nchi yetu, kwa msingi huo, Serikali ilidhamiria kuanzisha mchakato wa kupata katiba mpya ili hatimaye tuwe na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoendana na mahitaji, mabadiliko na matarajio mapya ya nchi yetu.
Nitoe rai kwenu nyote kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa bunge maalumu la katiba, ili itakapofika zamu yetu kuipigia kura rasimu watakayoipitisha wabunge wa bunge maalumu la katiba basi tuwe na uelewa wa nini tunachokwenda kukipigia kura. Taratibu zimewekwa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanashiriki kikamilifu, kwa kuwa jambo hili ni la kupanua demokrasia na kuhakikisha tunakuwa na Katiba ya nchi inayoonesha utashi wenu kwa Jamhuri ya Muungano,
Ndugu Wananchi, Napenda kuwaasa tena tuitumie amani, upendo na utulivu tulionao kwa kufanyakazi kwa bidii na maarifa, Tuepuke kukaa vijiweni bila kazi maalum hivyo tujihusishe na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Tutumie vizuri fursa tulizonano, mkulima ahakikishe anakuwa na kilimo chenye tija. Vivyo hivyo kwa wafanyakazi tufanye kazi kwa bidii na kutumia fursa zilizopo ndani ya Muungano wetu, kufanya biashara halali, tufuate taratibu na sheria zilizowekwa.
Mwisho; niamalizie kwa kusema kuwa, Muungano wetu umekuwa na mafanikio katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Wananchi wanaendelea kunufaika kwakupata fursa ya kuishi kwa amani na kufanya shughuli za kimaendeleo popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watanzania ni wamoja tusikubali kugawanywa kwa misingi ya tofauti zetu za Dini, Itikadi za Vyama, Rasilimali na Rangi sote ni mashahidi kuwa, Muungano wetu ndiyo nguzo kuu ya umoja na amani. Kijana unapoambiwa kufanya jambo tafakari kwanza kabla yakuchukua hatua yoyote.

“Utanzania wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha” Katu vijana tusirubuniwe na wachache wanaojitafutia umaarufu kwa gharama za watanzania.
Niwatakie sherehe njema, tuudumishe Muungano wetu kwani utanzania wetu ni muungano wetu hatunabudi kuulinda na kuutunza.
Asanteni kwa kunisikiliza.

Wednesday, April 16, 2014

BALOZI CHINA AENDELEA KUDUMISHA UHUSIANO




Ilikuwa wiki ya shamra shamra katika Mkoa wa Mara kwa kupata ugeni mzito kwa mara ya kwanza, kutoka China, Balozi wa China Dk. Lu Youqing katika Wilaya za Musoma, Rorya Tarime na Butiama.

Akiwa Manispaa ya Musoma alizindua urafiki kati ya Mji wa Xiang Tan kwa Rais Mao Zedong aliyekuwa Rais wa China kuanzia mwaka 1949-1976 na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania.

Nia ya ziara yake ikiwa ni uwekezaji katika Mji huu,huduma za elimu na afya bora kwa wakazi wa Mkoa wa Mara.
Balozi ameambatana na maafisa kutoka ubalozi wa China,Taasisi ya Mama Salma ya WAMA ambayo iligawa vyerehani 18,dawa za Malaria, kandambili, mipira,radio aina ya Tec Sun R-102 mini size Am/Fm stereo Receiver kadhaa za walimu.