Tuesday, August 23, 2011
MWANDISHI WA HABARI MUSOMA AGOMBEA POSHO.
Na Thomas Dominick,
Musoma
MWANDISHI wa habari na Mtangazaji wa Channel Ten Mkoa wa Mara, Mabere
Makubi anadaiwa kumpiga Mratibu wa Shirika lisilo la Kiserikali
linaloshughulika na Maendeleo ya Jamii Mkoani humo (TCDO), Rais
Kirangi baada ya mtangazaji huyo kudai posho kwa nguvu.
Tukio hilo lilitokea Agosti 22 mwaka huu saa 2 usiku baada ya viongozi
wa shirika hilo kumsindikiza sehemu ya kupumzika katika hosteli za
Kanisa la Katholiki Musoma mgeni ambaye ndiye Mlezi wa shirika Dkt.
Eliud Tongola ambaye amekuja toka nchini Korea kwa ajili ya uzinduzi
wa shirika hilo.
Akizungumzia tukio hilo jana, Mratibu huyo alisema kuwa baada ya watu
kutawanyika katika hosteli hizo mtangazaji huyo alitaka kwenda kuingia
chumbani kwa Dkt. Tongola ili kudai posho kwa nguvu.
“Mimi na wenzangu kumuambia aondoke atusubiri nje ili tumalizane naye
nikatoa shilingi 10,000/= na kumpatia agawane na mpiga picha iwe kama
nauli yao, akasema kuwa hawezi kufanya kazi ya shilingi elfu tano,”
“Lakini sisi hatukumwalika kuja kufanya kazi yeyote kwani yeye ana
mwaliko wa siku ya uzinduzi bali tuliokuwa tumemualika ni mpiga picha
kwa ajili ya matumizi ya ofisi lakini yeye alikuja na kusema kuwa
anataka posho kwa kuwa tayari amesharipoti habari Chanel Ten,”alisema
Kirangi.
Alisema kuwa baada ya kumpatia fedha hiyo akaanza kufanya fujo huku
akimrushia ngumi ambazo zilimpata kichwani na kumsababishia kuvimba
sehemu ya kichwa lakini kwa msaada wa mlinzi wa sehemu hiyo na ndugu
wa mtangazaji huyo walifanikiwa kumtoa nje.
“Alianza kufanya fujo pamoja na kunipiga ngumi kadhaa zingine
zilinipata kichwani kama unavyoona sehemu hii imevimba lakini mimi
sikumpiga ngumi hata moja kwa kuwa sikuona sababu ya kupigana lakini
wakati anatolewa nje na mlinzi na kaka yake Deo walimtolea vifungo vya
shati ambapo anadai nimlipe mimi,”alisema.
Alisema kuwa baada ya kuona anataka kurudi tena ndani kuendeleza fujo
waliamua kumpigia simu Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Robert Boaz
ambapo aliagiza askari kwenda eneo la tukio lakini alikuwa tayari
ameshaondoka.
“Tulimpigia simu RPC ili tupate msaada na ulinzi kwa kuwa Makubi
alitaka kuingia tena ndani ili kufanya fujo na kuingia chumbani kwa
mgeni wetu ili akamuambie ampe posho,”alisema.
Mtangazaji huyo alipoondoka hapo alikwenda polisi kuchukua PF 3 kwa
ajili ya kwenda hospitali kupata tiba kwa madai kuwa ameumizwa na
mratibu huyo kisha akafungua kesi yenye RB namba MUS/ RB 5855 ya mwaka
2011 kesi ya shambulio.
Mwandishi wa gazeti hili alipokutana na mtangazaji huyo na kumuuliza
nini kimetokea alikataa kuzungumzia tukio hilo na kuishia kusema kuwa
haki yake lazima ipatikane.
“Haki yangu lazima ipatikane na haki ichukue mkondo wake siwezi
kukubali kam kushindwa nikashindwie mahakamani na sio
vinginevyo,”alisema Makubi.
Dkt. Tongola ambaye anafanya kazi nchini Korea amekuja nchini kwa
ajili ya kuzindua shirika hilo siku ya Agosti 25 mwaka huu ambapo
atakabidhi misaada mbalimbali ya kijamii pamoja na vifaa vya hospitali
ya Mkoa wa Mara.
MWISHO
Friday, August 19, 2011
AMREF YATOA MIRADI TARIME
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la AMREF,Festus Ilako akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa Musoma Vijiji,Jamhuri William mkataba wa makubaliano ya miradi ya TUIMARISHE uzazi wa mpango,afya ya mama na maji utakaogharimu kiasi cha Sh.M.322, na mradi wa uzazi wa mpango na maendeleo ya mwanamke kiasi cha Sh.464 ikiwa na jumla ya Sh. Milioni 786 jana katika sherehe fupi zilizofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Polisi Mwisenge Musoma Mjini.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la AMREF,Festus Ilako akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Tarime, Magreth Momburi,mkataba wa makubaliano ya mradi wa uimaishaji utoaji huduma ya afya ya msingi utakaogharimu kiasi cha ShB.1.3 katika hafala fupi iliyofanyika jana katika ukumbi wa Bwalo la Polisi,Mwisenge Musoma Mjini.
AMREF WAANZA MIRADI YAO MKOA WA MARA.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara,Clement Lujaji mwenye suti nyeusi akipeana mkono na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika AMREF,Festus Ilako,mara baada ya kuweka saini za makubaliano kati ya AMREF na Serikali kuhusu uendeshaji wa miradi ya afya ya mama na motto na maendeleo ya janii Mkoa wa Mara kwa wilaya mbili za Tarime na kijiji cha Tegeruka cha Wilaya ya Musoma vijijini.
RAS huyo pia alishuhudia,usainiaji wa mikataba ya makubaliano kati ya Shirika la AMREF Tanzania na Serikali kuhusu uendeshaji wa miradi ya afya ya mama na mtoto, miradi ya TUIMARISHE uzazi wa mpango,afya ya mama na maji, wa Musoma vijini utakaogharimu kiasi cha Sh.M 322 na Mradi wa Uzazi wa mpango na maendeleo ya mwanamke ambao pia utagharimu kiasi cha Sh M. 464 na Wilaya ya Tarime katika mradi wa uimarishaji utoaji wa huduma ya afya ya msingi utakaogharimu kiasi cha Sh.B.1.3, baina ya Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo, Festus Ilako na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Musoma vijijini, Jamhuri William iliyofanyika katika bwalo la Polisi leo mchana.