Friday, May 6, 2011

WANASIASA WAPEWA ONYO!!!

MUSOMA.

KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Mara,John Henjewele amewaharisha viongozi wa vyama vya siasa kutotumia nafasi yao vibaya kwa kuwashawishi wananchi kukataa kutenga maeneo yao yaliyoko vijijini kwenda mijini kwa kuofia kupoteza mamlaka yao kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamekiuka utekelezaji wa sera na sheria ya Ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999.

Akifunga semina juu ya utekelezaji wa sheria ya ardhi ya vijiji ya namba 5 ya mwaka 1999 kwa viongozi wa Mkoa wa Mara alitoa tahadhari hiyo mara baada ya kuzuka mijadala kutoka kwa wenyeviti wa halmashauri kuwa hakuna haja ya kuongezwa vitongoji kuja mjini kwa kuwa tayari mji umekwishajaa.

Akitoa hoja katika semina hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma vijijini Magina Magesa alidai kuwa hakuna haja ya kumega kata zilizoko vijijini kuja Manispaa ya Musoma kuwa wananchi hawana miundo mbinu inayostahili na Kwamba kata hizo endapo zitaletwa mjini,watakuwa na hofu kwa kuwa kipato chao kinategemea ufugaji na kilimo.

Akitoa mada juu ya upanuzi na kukua kwa Miji,Afisa mipango miji Mkuu,wa wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mganga Majura alitanabaisha taratibu za kuzingatia wakati wa upanuzi wa miji kwa mujibu wa sheria kifungu kwa kifungu alisema kuwa Katika kifungu Na. 7(1) hubainisha kuwa kila mamlaka husika ni mamlaka ya upangaji katika eneo lake la utawala.

Pia Katika kifungu Na. 7(2) hutamuka waziwazi kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa ndie mwenye mamlaka ya kuamua kupanua mipaka ya miji hapa nchini na kifungu Na. 7(3) hubainisha kwamba endapo kuna vijiji vitamezwa na mipaka mipya ya mamlaka yeyote basi vijiji hivyo vitatakiwa kufutwa katika daftari ya usajili wa vijiji kwanza.

Aidha, katika kifungu Na. 7(4) inamtaja Waziri mwenye dhamana na masuala ya Mipango miji kuweza kutangaza katika gazeti la umma ingawa baada ya kushauriana na Waziri wa Serikali za Mitaa, chombo chochote kuwa mamlaka ya upangaji au shirika na kinginecho

Aliongeza kuwa vifungu mbalimbali vya Sheria hiyo pia hubainisha majukumu mbalimbali ya Mamlaka ya Upangaji inatakiwa kuyafanya na katika kifungu Na. 8(1) kinamtaja Waziri mwenye dhamana na Mipangomiji kuwa na mamlaka ya kutangaza katika Gazeti la umma eneo lolote la ardhi kuwa eneo la kupangwa (declaration of planning areas) .

Alisema kuwa katika kutekeleza sera ya umilikishwaji wa ardhi vijijini wananchi wawe na uwezo wa kupata cheti cha ardhi na kila kijiji kuwa na daftali la kijiji ili kubainisha ardhi inayomilikiwa na kupima mipaka ya kila kijiji Tanzania Bara hatua kwa hatua.

Kata ambazo ziko Wilaya ya Musoma vijijini ambazo zitaingizwa mjini ni pamoja na Nyankanga, Nyakatende, Etaro na Nyegina.

Akichangia mada juu ya uhawilishaji,Afisa ardhi kutoka Wilaya ya Bunda,Dennis Masami alionyesha wasiwasi wake juu fidia kwa kuwa na mlolomgo mrefu na upatikanaji wa fedha kutoka serikalini za kuweza kugharamia utekelezaji wa zoezi hilo.

“Kuna tatizo kubwa kwa mabaraza kwa kuwa hayana nguvu ya kisheria kutoa maamuzi katika maeneo yaliyopimwa na mabaraza yanaongozwa na watu wasio kuwa na taaluma ya sheria,ufanisi wa kuweza kutekeleza mjaukumu yao kwa kuwa hauna utaratibu mzuri wa malipo ya kazi zao”Alisema Masami.

Akitoa wito alisema kuwa sheria ya baraza la kata ifanyiwe marekebisho ili baraza lipewe wataalamu wenye taaluma ya sheria,pia Wenyeviti na wajumbe wake waajiriwe na serikali kwani itapunga kero nyingi ambazo kwa sasa wananchi wanakabiliana nazo.

Kaimu Mkuu wa Mkoa huyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele aliitaka wizara kutoa kipaumbele kwa Mkoa wa Mara kwa kuwa migogoro mingi ya ardhi iko Mkoani hapo hasa katika wilaya ya Tarime ambapo imefikia hatua ya malumbano hata kusabisha ugomvi kutokana na ardhi.,Sanjali na mafunzo zaidi kwa wataalamu ili waweze kutatua migogoro ya ardhi ambayo ni kikwazo kikubwa mkoani humo.

Wizara ya nyumba na maendeleo na makazi ilianza kuhamasisha na kuwezesha mikoa na wilaya ili kuanza utekelezaji katika vijiji ili umilikaji wa ardhi kimila vijijini kurasimisha ardhi kuwa mtaji hai ambapo wamiliki wa ardhi wapewe hatia za kumiliki ardhi kimila na kuboresha usalama wa kumiliki ardhi zao.


No comments:

Post a Comment