Sunday, January 1, 2017
TATIZO LA UVAMIZI WA TEMBO KUTOWEKA
SERENGETI.
SERIKALI kupitia wizara mbalimbali itaangalia upya uwezekano wa kutatua matatizo ya uvamizi wa wanyama aina ya Tembo wanaoharibu mazao ya wananchi.
Naibu Waziri wa Mali asili na Utalii, Mhandisi, Ramo Makani aliyasema hayo katika uwanja wa ndege wa Ikorongo baada ya kumaliza ziara yake katika Wilaya ya Serengeti, kutokana na hali asili aliyoina serikali kupitia Wizara zote nne itaangalia uwezekano wa kuangalia na kupitia upya na kuweka mikakati ya kuzuia wanyama hao wasiharibu mazao ya wananchi.
''Tuna Wizara zinazohusika na masuala mbalimbali, ikiwemo,ya Ardhi, Mifugo, Maliasili, na nyingine tutakaa kwa pamoja kuangalia changamoto zilizopo,nimeona kuna watu wanaishi kihalali na ni vijiji vilivyopo kwa mujibu wa sheria vinapakana sana na mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti ambavyo kwa sasa vimekuwa vimekuwa vikivamiwa mara kwa mara’’Alisema Makani.
Akiwa katika kijiji cha Makundusi Wilaya ya Serengeti kinachopakana na mapori ya akiba alishuhudia wanyama hao walivyobomoa nyumba katika tukio lilitokea oktoba mwaka jana na kusababisha madhara makubwa ya kuhama kwa familia mbili ikiwemo ya Malimi Nyamuhanga yenye jumla ya wakazi 10 na nyingine ambapo wanyama hao walikula chakula chote kilichokuwa ndani ya nyumba.
Alisema kutokana na wananchi kuishi katika njia za mapitio ya wanyama(shoroba) na mabadiliko ya wanyama kwa kuvamia majumba ya watu na kula chakula na kuvamia mashamba ni jambo jipya ambalo linatizamwa kwa upana wake.
Akizungumza katika majumuisho ya ziara hiyo katika ofisi za pori la akiba la Ikorongo,Afisa wanyamapori Wilaya ya Serengeti, John Meitamei (DGO) alisema kuna ongezeko kubwa la wanyamapori aina ya Tembo,na wao kuwa na tabia ya kukumbuka walikotokea, mabadiliko ya tabia nchi, kumesababisha waingie katika maeneo ya wakazi na kusababisha madhara, hivyo wanaiomba serikali kunusuru wananchi wasipate matatizo.
Alisema kuwa wameweka mikakati mbalimbali ya kunusuru ikiwemo ya ujenzi wa uzio wa umeme ili wanyama hao wasiingie kwenye makazi ya watu pia wameiomba Wizara kuongeza vitendea kazi yakiwemo magari ya kuweza kufanya doria ya mara kwa mara ili wananchi waweze kuvuna mazao yao na kuunda kikosi kazi cha ulinzi kitakachoshirikiana na wananchi.
Akiwa katika kijiji cha Mugeta Wilaya ya Bunda katika mkutano wa hadhara, wananchi hao walimwomba Naibu Waziri huyo kuwasaidia chakula cha njaa haraka, ili kuwanusu na njaa kwani kwa sasa debe moja la mahindi linauzwa Sh.21,000 na kwamba endapo Serikali hatachukua hatua za makusudi debe la mahindi wiki ijayo litafikia sh.40,000.
Aliagiza kikosi dhidi Ujangili (KDU) na magari yaliyokuwa yakilinda mwaka wa juzi yaanza doria na vikundi vya ulinzi vya vijana viundwe na vitambuliwe na Serikali ili viendelee kulinda katika kijiji cha Maliwanda Wilayani humo ambapo alitoa tochi zipatazo 200 kwa ajili ya kufukuzia wanyama hao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment