MUSOMA
WADAU wa mazingira katika Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara wameilalamikia sekta ya uvuvi Mkoani MARA kwa kutokuwa makini katika ufuatiliaji wa vitendo vya uvuvi haramu vinavyofanyika ndani ya ziwa Victoria ambavyo vinasababisha uharibifu wa mazingira,
Hayo wamesema Novemba 29 katika siku ya maadhimisho ya siku ya Ziwa Victoria yaliyofanyika katika ukumbi wa uwekezaji Mkoani Mara ulioko katika Manispaa ya Mji wa Musoma, ambapo walitaka kujua kulikoni zana haramu zinazidi kutumika na kupelekea Samaki wanaovuliwa ndani ya ziwa victioria kutokuwa na kiwango cha kimataifa wakati wanadai kuwa samaki wanaovuliwa wana kiwango cha Kimataifa.
Walisema hata kama wanawapatia semina juu ya utunzaji wa mazingira ya ziwa Victoria lakini iwapo hawatakuwa wafuatiliaji itabakia kuwa maneno ya karatasi tu kwa kuwa mara kwa mara wamekuwa wakitoa semina kama hizo lakini ufuatiliaji wake kwa vitendo umekuwa ni mdogo .
Walimtaka Afisa Uvuvi Mkoa Mara awaeleze kwa nini zana haramu kama makokoro ya kuvulia samaki wachanga,dawa za sumu wanazotumia wavuvi kuvulia samaki bado zinazidi kuongezeka ndani ya ziwa, sehemu madawa hayo yanapouzwa wanapafahamu na hata nyumba wanazohifadhia zana hizo wanazifahamu wakati polisi na BMU wapo kila koma na kazi yao ni nini, huku baadhi yao wakimtuhumu kushirikiana na wavuvi haramu.
Akijibu maswali yaliyoulizwa na wadau hao Afisa Uvuvi Mkoani Mara Apolinary Kyoja alionekana kutokuwa na majibu sahihi ya moja kwa moja ya kuwaeleza wadau hao kulingana na maswali yaliyoulizwa badala yake aliwaomba ushirikiano katika kutoa taarifa.
Kyoja amewataka wadau hao kumsaidia kupambana na wavuvi haramu kwa maana kuwa yeye peke yake hawezi kufuatilia kila mahala kwani hana vyenzo za kutosha za kufuatilia kila sehemu kwa kuwa kila mtu ni mlinzi wa ziwa Victoria.
Amesema kila mtu anatakiwa awe mlinzi wa ziwa hilo kwani hata yeye anao uwezo wa kuzunguka kila mahala kukagua usafi wa ziwa ila anachokiomba kutoka kwa wananchi ni kusaidiana nae ili kutokomeza tatizo la uchafuzi wa ziwa hasa kwa kupashana taarifa pale wananchi wanapoona wavuvi haramu wakitumia zana haramu za uvuvi.
Akizindua semina iliyoendana na maadhimisho hayo ya siku ya ziwa Victoria Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara ,NDUGU GEOGFEY NGATUNI amesema kuwa wananchi wanatakiwa kutunza mazingira hususani ya ziwa Victoria kwa kuwa maji hayo ndiyo yanayotumika katika shughuli mbalimbali viwandani na kwa matumizi ya majumbani.
Amesema wavuvi wanapoendelea kutumia zana hizo haramu wanasababisha madhara mengi kwa afya ya binadamu na kwa mazingira hali inayoadhili uchumi wa Taiafa letu.
Kauli mbiu ya ziwa Victoria ni Ziwa Victoria ni uhai wetu,mali yetu tuilinde.