Friday, April 29, 2011

MBUNGE AKATAA KUTUMIA OFISI YAKE.

KATIKA hali isiyo ya kawaida Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini Vicent Nyerere amekataa ofisi yake kwa madai kuwa siyo nzuri.

Habari kutoka katika chanzo chetu cha habari kutoka Mjini Musoma kimesema kuwa Mbunge huyo tangu achaguliwe na wananchi hajawahi kufika ofisi kwake licha ya wananchi lukuki kumsaka ofisi hapo kutoa hoja zao bila mafanikio.

Chanzo hicho kimesema kuwa Mbunge huyo amedai kuwa ofisi hiyo siyo nzuri na kwamba anasubiri kumalizika kwa jengo jipya la ghorofa moja lililopo katika halmashauri ya Mji wa Musoma,mkabala kabisa na ilipo ofisi yake aliyoikataa.

Mwandishi wa habari hii alifanikiwa kufika katika Halmashauri ya Mji wa Musoma na kugundua kuwa ni kweli ofisi hiyo haitumiki,na kushuhudia tangazo lililobandikwa ofisini kwa Meya wa Mjini Alex Kisulula kuwa ndiyo ofisi ya Mbunge na Meya.

Chanzo hicho kimezidi kusema kuwa Mbunge huyo alikabidhiwa ofisi hiyo kuwa ndo atakuwa anaitumia lakini cha kushangaza ameamua kutumia ofisi ya Meya bila kutoa taarifa ya maandishi kwa uongozi huska wa halmashauri hiyo.

Katika uchaguzi uliomalizika Mwaka jana, Mbunge huyo alishinda na kutangazwa kuwa Mbunge wa Musoma Mjini,ambapo tangu achaguliwe hajawahi kushiriki vikao vyovyote vya halmashauri,Baraza la Madiwani,Bodi ya barabara na vinginevyo.

Pia katika uchaguzi huo viti 10 vya udiwani vilichokuliwa na Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) ambapo CCM ilipata viti vitatu.

Kata zilizoko Mji wa Musoma ni Mukendo,Iringo, Kitaji, Nyamatare, Buhare, Bweri, Makoko, Nyasho, Nyakato, Mwisenge, Kigera, Mwigobero,Kamunyonge.

Jitihada za kumpata Mbunge huyo kuzungumzia ni kwa nini hataki kutumia ofisi aliyopangiwa na kukabidhiwa na Mkurugenzi wa Mji wa Musoma hazikuzaa matunda.

Saturday, April 16, 2011

BAJETI YA HALMASHAURI YA SERENGETI

HALMASHAURI ya Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara imekisia kutumia jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 23,216,215,911.20 katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2011/2012.

Afisa Mpango wa halmashauri hiyo Joseph Kitanana aliyasema hayo kwenye kikao cha baraza la madiwani cha kupitisha bajeti ya mwaka huo wa fedha kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.

Kitanana akisoma taarifa ya makisio ya bajeti ya fedha hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Kimulika Kalikinga alisema upitishaji wa bajeti hiyo ni sambamba na na mwongozo wa Taifa wa mpango ya maendeleo wa miaka mitano wa serikali za mitaa kwa mwaka 2011/12 hadi 2015/16 kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya CCm ya mwaka 2010/15.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha wa kati na bajeti 2011/12 hadi 2015/2016 halmashauri itaendelea kutekeleza majukumu ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo Shilingi mili.12,714,110,499.20 ni kwa ajili ya mishaharana matumizi mengineyozitatumika sh. Milioni 3,183,993,576 na katika miradi ya maendeleo zitagharimia shilingi milioni 7,318,376,836 .

Alisema kuwa kati ya kiasi hicho shilingi milioni 1,171,772,000 ni vyanzo vya mapato ya ndani,ambapo shilingi milioni 797,515,000 ni makusanyo ya halmashauri na shilingi milioni 337,992,000 ni fidia ya vyanzo vilivyofutwa sawa na ongezeko la asilimia 30.79 ikilinganishwa na makusanyo ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2010/2011 wa kiasi cha shilingi milioni 551,959.

Katika elimu ya utalawa na watu wazima zitatumika shilingi Milioni 415.931,elimu ya shule za msingi shilingi mil.7,482,shule za sekondari zitagahrmu shilingi mil.2.724 na katika shughuli za ukaguzi wa shule zitatumia shilingi mil.14.1 na katika mradi wa kilimo zitatumika shilingi milioni 352.124 ambapo mifugo ni shilingi milioni 316.118.

Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni utekelezaji wa miradi katika sekta ya miundombinu unaokabiliwa na upungufu wa wakandarasi wenye na ujuzi,vifaa n auzoefu wa kutosha.

Aidha kupanda kwa bei za mafuta aina ya petrol sanjali na vyakula,mali ghafi na pembejeo vitadhiri bajeti na hali ya ugumu wa maisha kwa wakazi wa Wilaya hiyo zitakuwa kikwazo.

Akizungumzia zaidi Wilaya hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo,Kimulika Galikinga aliwataka madiwani hao kupendekeza mikakati ya maendeleo na badal ayake kuachana na itikadi za vyama.

MABADILIKO YA KATIBA


MABADILIKO YA KATIBA KAMA NYENZO YA UFISADI

Na jenerali Ulimwengu.


MWAKA 2000, kabla ya uchaguzi mkuu, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilifanya mabadiliko ya kikatiba ambayo, miongoni mwa mambo mengine, yalibainisha kwamba mgombea urais anaweza kuchaguliwa na akakabidhiwa madaraka ya rais bila kulazimika kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.
Kwa wale waliojua kilichokuwa kikifanyika hii ilikuwa ni hatua muhimu sana, ingawaje haikupokelewa kwa kelele ambazo zilikuwa zinastahili. Umuhimu wake unatokana na kwamba mabadiliko hayo yalikuwa yanaingiza mbegu za utata mkubwa unaoweza kuikumba nchi hii huko tuendako, hata kama hivi sasa hatujui kwamba bomu limetegwa ila sisi hatujui.
Nitaeleza. Kukubali kikatiba na kisheria kwamba mgombea anaweza kuwa rais bila kulazimika kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa ni kukubali kwamba mtu anaweza kuwa rais bila kuwa na ridhaa, angalau, ya nusu ya wapiga kura wake. Ina maana kwamba, hata kama asilimia sitini, au sabini, au hata themanini wakimkataa, tena wakasema hivyo kwa kishindo, mtu huyo atakuwa rais alimradi ndiye aliyepata kura nyingi kuliko mgombea ye yote mwingine.
Tuchukue sura tuliyo nayo ya vyama vya siasa nchini Tanzania hivi leo. Tuseme kwamba vyama vinane vimewaweka wagombea wa nafasi ya urais, na vyama hivyo ni CCM, CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP, Democrasia Makini, DP na TPP.
Iwapo miongoni mwa wagombea wa vyama hivyo wagombea wa vyama saba, (tuseme CCM, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP, Demokrasia Makini, DP na TPP), watapata jumla ya asilimia 70 ya kura zilizopigwa, kisha mgombea wa CHADEMA akapata asilimia 30, mgombea wa CHADEMA atakuwa rais.
Mantiki ya uamuzi huo bado haijanielea, na wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa, kisheria na kikatiba wanasema haijawaelea. Ilikuwa vigumu zaidi (labda kuliko ilivyo leo) kuielewa wakati huo ikipitishwa kwa sababu ya tukio moja kuu la miaka mitano tu kabla ya uamuzi huu wa kushangaza. Nitalisimulia.
Mwaka 1995, mwishoni kabisa mwa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM pale Chimwaga, wagombea watatu wa mwisho waliopigiwa kura walikuwa Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Cleopa Msuya.
Kura zilipohesabiwa ikadhihirika kwamba hakuna mmoja aliyeweza kupata zaidi ya nusu ya kura, na kwa hiyo ikabidi wawili wa juu warudiane katika kile kinachoitwa run-off. Msuya alipata kura za chini zaidi, kwa hiyo run-off ikawa kati ya Kikwete na Mkapa, na Mkapa akashinda.
Najua wapo watu wanaodai kwamba ulikuwa uamuzi wa mzengwe; kwamba Kikwete alikuwa kashinda; kwamba Mwalimu Nyerere aliingilia kati “kumnusuru Mkapa” ; eti Mwalimu alimwambia Kikwete: Wewe bado kijana, mwachie mwenzako, zamu yako itakuja.
Hadithi hii nitaijadili mbele ya safari, lakini kwa sasa niseme tu kwamba si kweli. Katika majukumu ya mkutano mkuu wa CCM katika mwaka wa uchaguzi mkuu wa Taifa, mojawapo ni “kumchagua” mwanachama atakayegombea urais wa Jamhuri, na kwa mujibu wa katiba ya CCM uchaguzi katika nafasi ya aina hiyo hauna budi uheshimu kanuni mbili kuu, miongoni mwa nyingine: moja, uchaguzi uwe kwa kura ya siri; pili mshindi apatikane kwa zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.
Iwapo hivyo ndivyo ilivyo na ndivyo ilivyokuwa huko Chimwaga wakati huo; na iwapo matakwa hayo ya katiba ya CCM yalijengeka juu ya msingi wa mantiki fulani; na iwapo mantiki hiyo ndiyo iliyomfanya Mkapa awe mgombea wa CCM na siyo Kikwete; na iwapo mantiki hiyo ndiyo iliyotaka kwamba uchaguzi wa Taifa umpate rais kutokana na mgombea aliyepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa, sasa ni kwa nini mgombea aliyepitishwa kwa kanuni ya “zaidi ya nusu ya kura” katika chama chake aifutilie mbali kanuni hiyo kwenye ngazi ya Taifa kabla ya kugombea muhula wa pili?
Jibu rahisi ni kwamba washauri wa Benjamin Mkapa, wakati huo akiwa rais, hawakuamini, au yeye mwenyewe hakuamini kwamba angeweza kupata zaidi ya nusu ya kura ambazo zingepigwa katika uchaguzi wa 2000. Kwa hiyo, kama kawaida ya watawala wetu wanapotaka kukidhi maslahi yao bila ya kujali maslahi ya Taifa, ikaamuliwa kuiondoa ‘kero’ hiyo kutoka katiba ya Jamhuri.
Labda tungekumbushana kwamba wakati mabadiliko haya yanafanyika Mwalimu Nyerere alikwisha kuaga dunia, na tunajua sasa kwamba mambo mengi ya kifisadi yalifanyika wazi wazi pale watawala walipojua kwamba hakuna mtu mwenye kauli nzito angeweza kuwakemea hata wangefanya nini.
Kwa maneno mengine, kifo cha Mwalimu kilikuja kama fursa kwa kila aina ya ufisadi kuchanua bila kuchelea kusutwa. Sote tunajua kwamba Mwalimu katika miaka yake ya ustaafu alikuwa amejenga utamaduni wa kushiriki, kama raia ye yote anayejali, katika mijadala kuhusu mustakabali wa Taifa, na ni vigumu kuamini kwamba angekaa kimya kuhusu suala hili, kama ambavyo najua asingenyamaa kuhusu ule ufisadi mwingine unaohusu mali.
Kwamba Mkapa na watu wake walikuwa wametishika katika uchaguzi wa mwaka 1995 ni dhahiri, nami naweza kulirudia hili mara nyingi. Augustine Mrema alikuwa amechota akili za watu wengi kiasi cha kuifanya kampeni ya Mkapa iegemee zaidi nguvu ya ushawishi aliokuwa nao Mwalimu kwa watu wake walio wengi. Bila Mwalimu ilikuwa vigumu kuona ni jinsi gani Mkapa angeshinda.
Hata hivyo, mwaka 2000 mambo yalikuwa yamekwisha kubadilika sana. Kweli, Mwalimu alikwisha kuondoka, lakini Mkapa alikuwa amefanya kazi nzuri (kwa ujumla) katika miaka mitano ya uongozi wake, na wala hakuwa na sababu ya kuichezeachezea katiba ili kujihakikishia ushindi kwa njia yo yote ile, kitendo ambacho bila shaka kilizidisha nguvu ya uvumi kwamba hata Chimwaga 1995 utaratibu ulipindwa ili kumlinda Mkapa.
Hapa tunakumbana na suala kubwa, zito na la msingi. Kwa kubadili katiba kama ilivyoelezwa hapo juu, Mkapa na watu wake, hususan washauri wake wakuu akiwamo Mwanasheria Mkuu, waliitendea nchi hii haki?
Je, maslahi ya Mkapa na watu wake ya kurejea madarakani mwaka 2000 yalikuwa na ushawishi wenye uzani wa kutosha kuiingiza nchi katika utaratibu ambao hapo baadaye unaweza kuifanya nchi ikatawaliwa na mtu ambaye hatakiwi?
Je, kitendo cha kubadili katiba jinsi kilivyofanywa hakikuwa na maana ya kwamba Mkapa na washauri wake walikuwa radhi kubakia madarakani kwa njia yo yote ile, hata kama wananchi wangekuwa hawamtaki? Au siyo maana yake?
Hapa sitaki kuingia katika uchunguzi wa kazi hiyo muhimu waliyotaka kuifanya (Mkapa na watu wake katika muhula wa pili) hadi wakaichezea katiba (nitaijadili katika sura zijazo), bali tu nataka niseme kwamba kilikuwa kitendo cha hovyo, kitendo cha uhuni na kilichodhihirisha udhaifu mkubwa wa imani, yote ambayo leo hii hayashangazi.
Mwanademokrasia (dhahiri, Mkapa na washauri wake sio) hawezi kubadilisha kanuni za ushindani kwa sababu tu ameona kwamba zitamnyima ushindi. Atazibadili pale tu anaposhawishika kwamba kwa kuzirekebisha atatoa uhuru mkubwa zaidi kwa raia zake, ili sauti yao katika uendeshaji wa nchi isikike zaidi.
Katika awamu ya tatu tulizoea sana kusikia maneno “uvivu wa kufikiri” ambao, mimi nakiri, umejaa tele nchini mwetu, hususan miongoni mwa watawala wasiotaka kusumbua vichwa vyao kudurusu mifumo mbadala ya kuendeshea shughuli za utawala na maendeleo ya watu wao. Uvivu huo wa kufikiri unatokana na kwamba muda wao ulio mwingi wanashughulika na mambo mengine, ambayo hawakuyasema katika ilani zao.
Isingekuwa hivyo wangetumia muda mwingi zaidi kujadili nini kifanyike iwapo hakuna mgombe mmoja aliyepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa. Njia moja ni kufanya kama ilivyotokea Chimwaga 1995 Kikwete na Mkapa waliporudiana baada ya kumtoa Msuya. Njia nyingine ni ushirikiano, katika serikali, baina ya vyama vinavyokaribiana katika falsafa na mwelekeo. Kwa vyo vyote vile, mwaka 2000 hatukufika huko, kwani Mkapa, pamoja na woga wake wote, pamoja na kutojiamini, alishinda.







KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA

KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA,

UTANGULIZI

MISINGI YA KATIBA

Kwa kuwa sisi Wananchi wa Shirikisho wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki udugu na amani;

Na kwa kuwa misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasi ambayo serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi, na pia yenye mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumisha na kulindwa, na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu:

Kwa hiyo, basi, Katiba hii Imetungwa na wananchi, kwa kura ya maoni Kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasi.

SURA YA KWANZA

SHIRIKISHO

SEHEMU YA KWANZA

SHIRIKISHO

Kutangaza Shirikisho

1. Tanzania ni nchi moja na ni Shirikisho.

Eneo la Jamhuri la Shirikisho

2.(1) Eneo la Shirikisho ni eneo lote la Tanganyika na eneo la Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzanyika na Zanzibar inaimiliki chini ya Sheria za Kimataifa.

Bunge

2. Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Shirikisho au Serikali ya Zanzibar, au Serikali ya Tanganyika, Waziri Mkuu wa Serikali ya Zanzibar na wa Serikali ya Tanganyika wanaweza kugawa maeneo yao katika mikoa, wilaya baada ya kupat amaoni ya wananchi, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge la Tanganyika au Bunge la Zanzibar.

Bunge

Na kwamba maamuzi ya kugawa nchi katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo yatakayofanywa na Waziri Mkuu anayehusika kama ilivyoelezwa katika Ibara hii, itakuwa ni lazima yafikishwe katika Bunge la Tanganyika au Bunge la Zanzibar kwa jinsi itakavyokuwa kwa uthibitisho.

Tangazo la nchi yenye mfumo wa vyama vingi

3. (1) Jamhuri ya Shirikisho ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

2. Mambo yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa Tanzania yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Tanganyika na sheria zilizotungwa na vyombo husika kwa ajili hiyo.

Utekelezaji wa shughuli za Mamlaka ya Nchi

4.(1) Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Shirikisho zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo vitatu vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo vitatu vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.

(2) Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Shirikisho, na Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar na vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho, Idara ya Mahakama ya Tanganyika na Zanzibar na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga Sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge la Shirikisho, Mabunge ya Tanganyika na Zanzibar.

(3)Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Shirikisho, na Serikali ya Zanzibar, na Serikali ya Tanganyika, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na Mambo ya Shirikisho kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, na pia kutakuwa na mambo yasiyo ya Shirikisho, ambayo ni mambo mengine yote ambayo hayakutajwa katika nyongeza hiyo na ambayo yametajwa katika Nyongeza ya pili katika Katiba hii.

(4) Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake kwa kufuata masharti yaliyomo katika Katiba hii,

(5) Bunge na Mahakama vitakuwa ni vyobo huru katika utendaji wa kazi zake na Serikali ya Shirikisho itawajibika kuchukua hatua zote za lazima kuhakikisha kwamba Bunge na Mahakama zinafanya kazi zake kwa ufanisi na malengo yaliyokusudiwa na Katiba hii.

SEHEMU YA PILI

MALENGO MUHIMU NA MISINGI YA MWELEKEO WA SHUGHULI ZA SERIKALI

Ufafanuzi

5. Katika sehemu hii ya sura hii, isipokuwa kama maelezo yahitaji vinginevyo, neno "Serikali" maana yake ni pamoja na Serikali ya Shirikisho, na Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar, Serikali za mitaa na pia mtu anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali yoyote.

Matumizi ya masharti ya Sehemu ya Pili

6. (1) Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (2), Serikali vyombo vyake vyote na watu wote au mamlaka yoyote yenye kutekeleza madaraka ya utawala, madaraka ya kutunga sheria au madaraka ya utoaji haki, watakuwa na jukumu na wajibu wa kuzingatia, kutilia maanani na kutekeleza masharti yote ya sheemu hii ya Sura hii.

Serikali na watu

7.(1) Shirikisho la Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasi na haki ya kijamii, na kwa hiyo

(a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali zitapata madaraka na mamlaka zake zote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.

(b) Lengo kuu la Serikali zote litakuwa ni ustawi wa wananchi;

(c) Serikali zitawajibika kwa wananchi; na

(d) Wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali zao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

(2) Muundo wa Serikali ya Shirikisho na Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar, au wa chochote kati ya vyombo vyake na uendeshaji wa shughuli zake, utatekelezwa kwa kuzingatia umoja wa Shirikisho na haja ya kukuza umoja wa kitaifa na kudumisha heshima ya Taifa.

8. Lengo la Katiba hii ni kudumisha udugu na amani katika Shirikisho. Kwa hiyo, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha-

(a) kwamba utu na haki zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa;

(b) kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa;

(c) kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufa aya wananchi wote kwa jumla.

(d) kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa;

(e) kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu riziki yake;

(f) kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu na makubaliano ya kudumisha Haki za Binadamu ya Umoja wa nchi Huru za Afrika na yale ya Umoja wa Mataifa;

(g) kwamba Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa waume, bila ya kujali rangi, kabila , dini au hali ya mtu;

(h) kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaoondolewa nchini;

(I) kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umaskini, ujinga na maradhi.

(j) kwamba nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia.

Wajibu wa kufanya kazi, kupata elimu na nyinginezo

9.(1) Mamlaka ya Nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa wajibu wamtu kufanya kazi haki ya kujipatia elimu na haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi au hali ya ulemavu, na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi.Bila kuathiri haki hizo, Mamlaka ya Nchi itaweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mtu anaishi kwa jasho lake.

(2) Kila mtu anao wajibu wa kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake.

(3) Serikali itafanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa na za kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo katika ngazi zote za shule na vyuo vinginevyo vya mafunzo.

SEHEMU YA TATU

HAKI NA WAJIBU MUHIMU

Haki ya Usawa

Usawa wa binadamu

10 (1) Binadamu wote wana asili moja huzaliwa huru na wote ni sawa.

(2) kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake

Usawa mbele ya Sheria

11.(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.

(2) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Shirikisho au inayotumika nchini kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.

(3) Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya Mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na Sheria au kwa mujibu wa sheria.

(4) Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya Mamlaka ya Nchi.

(5) Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara hii neno "kubagua" maana yake ni kutimiza haja, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, jinsia, kabila , pahala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini au hali yao ya maisha kwa namna ambayo watu wa aina fulani wanafanyiwa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima.

(6) Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria, Mamlaka ya nchi itaweka taratibu zinazofaa au zinazozingatia msiingi kwamba-

(a) wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi na mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufani au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo hicho kinginecho kinachohusika; na kwamba shauri hilo litasikilizwa bila kuchelewa;

(b) ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo;

(c) ni marufuku kwa mtu kukamatwa na kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chochote ambacho alipokitenda hakikuwa ni kosa chini ya sheria, na pia kwamba ni marufuku kwa adhabu kutolewa ambayo ni kubwa kuliko adhabu iliyokuwapo wakati kosa linalohusika lilipotendwa;

(d) kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshaji wamambo ya jinai na katika shughuli nyingine ambazo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu;

(e) ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.

Haki ya kuishi

Haki ya kuwa hai

12. Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake.

Haki ya Uhuru wa watu binafsi

13. (1) Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru

(2) kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo, isipokuwa tu-

(a) katika hali na kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria inayohusu upelelezi wa makosa ya jinai au

(b) katika kutekeleza hukumu, amri au adhabu iliyotolewa na mahakama kutokana na shauri au mtu kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.

Haki ya faragha na ya usalama wa mtu

14. (1) Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi.

(2) Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kwa mujibu wa ibara hii , Bunge la shirikisho na Mabunge ya Tanganyika na Zanzibar itaweka utaratibu wa sheria kuhusu hali, namna na kiasi ambacho haki ya mtu ya faragha na ya usalama wa nafsi yake, mali yake na maskani yake, yaweza kuingiliwa bila ya kuathiri ibara hii.

Uhuru wa mtu kwenda atakako

15. (1) Kila raia wa Shirikisho anayo haki ya kwenda kokote katika Shirikisho na kuishi katika sehemu yoyote , kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Shirikisho.

Uhuru wa mtu kwenda atakako

15. (1) Kila raia wa Shirikisho anayo haki ya kwenda kokote katika Shirikisho na kuishi katika sehemu yoyote , kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Shirikisho.

(2) Sheria yoyote yenye madhumuni ya-

kuweka mipaka kwa matumizi ya uhuru wa mtu kwenda anakotaka ili-

(a) kuwezesha upelelezi wa kosa la jinai;

(b) kutekeleza hukumu au amri ya mahakama; au

(c) kumlazimisha mtu kutimiza kwanza wajibu wowote anaotakiwa na sheria kuutimiza; au

(d) kulinda manufa ya umma kwa jumla au kuhifadhi maslahi fulani mahususi au maslahi ya sehemu fulani ya umma, ambayo yataelezwa bayana kwenye Sheria hiyo haitahesabiwa kuwa ni batili au ni kinyume cha ibara hii.

Haki ya Uhuru wa Mawazo

Uhuru wa Maoni

16. (1) kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

(2) Kila raia anayo uwezo wa kutafuta na haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na dunia kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

Uhuru wa mtu kuamini dini atakayo

17.(1) Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru kubadilisha dini au imani yake.

(2) Bila ya kuathiri sheria za kulinda amani za Shirikisho, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi; na shughuli na uendeshaji wa Jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za Mamlaka ya Nchi.

(3) Kila palipotajwa neno "dini" katika ibara hii ifahamike kwamba maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengineyo yanayofanana au kuambatana na neno hilo.

Uhuru wa mtu kushirikiana na wengine

18. (1) Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za kulinda amani, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.

(2) Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1) haitakuwa halali kwa chama cha siasa kuandikishwa ambacho kutokana na Katiba au sera yake-

(a) kina kusudia kukuza au kupigania maslahi ya-

(I) imani au kundi lolote la dini;

(ii) kundi lolote la kikabila, pahala watu watokeapo, rangi au jinsia;

(iii) eneo fulani tu katika sehemu yoyote ya Shirikisho;

(b) kinapigania kuvunjwa kwa Shirikisho;

(c) kinakubali au kupigania matumizi ya nguvu au mapambano kama njia za kufikia malengo yake ya kisiasa;

(d) kinapigania au kina kusudia kuendesha shughuli zake za kisiasa katika sehemu moja tu ya Shirikisho.

(e) hakiruhusu uongozi wake kuchaguliwa kwa vipindi na kwa njia za kidemokrasia.

(3) Bunge laweza kutunga sheria inayoweka masharti yatakayohakikisha kuwa vyama vya siasa vinazingatia mipaka na vigezo vilivyowekwa na masharti ya ibara ndogo ya (2) kuhusu uhuru, haki ya watu kushirikiana na kujumuika.

(4) Bila kuathiri ibara ndogo ya (2) ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote cha Siasa, au chama chochote cha siasa kukataliwa kusajiliwa kwa sababu tu ya itikadi au falsafa.

(5) Itakuwa ni marufuku kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama ya Shirikisho, Jaji wa Mahakama Kuu, Hakimu wa ngazi yoyote kujiunga na chama chochote cha Siasa, isipokuwa tu kwamba atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 19 ya Katiba hii.

Haki ya kupiga kura

19.(1) Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywaTanzania na wananchi. Haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengineyo ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi.

(2) Bunge laweza kutunga sheria na kuweka masharti yanayoweza kuzuia raia asitumie haki ya kupiga kura kutokana na yoyote kati ya sababu zifuatazo, yaani raia huyo-

(a) kuwa na uraia wa nchi nyingine;

(b) kuwa na ugonjwa wa akili;

(c) kutiwa hatiani kwa makosa fulani ya jinai;

(d) kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura.

Mbali na sababu hizo hakuna sababu nyingine yoyote inayoweza kumzuia raia asitumie haki ya kupiga kura.

(3)Bunge litatunga Sheria ya Uchaguzi na kuweka masharti kuhusu mambo yafuatayo-

(a) utaratibu wa kuandikisha wapiga kura katika uchaguzi wa Rais wa Shirikisho, Wabunge, majimbo ya uchaguzi wa Tanganyika na Zanzibari, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.

(b) kutaja sehemu na nyakati za kuandikisha wapiga kura na kupiga kura;

(c) utaratibu wa kumwezesha mpiga kura aliyejiandikisha sehemu moja kupiga kura sehemu nyingine na kutaja masharti ya utekelezaji wa utaratibu huo;

(d) Kutaja kazi na shughuli za Tume za Uchaguzi na utaratibu wa kila uchaguzi ambao utaendeshwa chini ya uongozi na usimamizi wa Tume za Uchaguzi katika Shirikisho, Tanganyika na Zanzibar.

Uhuru wa kushiriki shughuli za umma

20. (1) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 19, ya 39 na ya 65 ya Katiba hii kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi , kila raia wa Shirikisho anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.

(2) Kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa.

Wajibu wa kufanya kazi

Wajibu wa Haki ya kufanyakazi

21. (1) Kila mtu anayo Wajibu wa kufanyakazi.

(2) Kila raia anastahili fursa ya haki sawa, kwa masharti ya usawa, ya kushika nafasi yoyote iliyo chini ya Mamlaka ya Nchi.

Haki ya kupata ujira wa haki

22. (1) Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa kazi wanayoifanya.

(2) Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.

Haki ya kumiliki mali

23.(1) Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

(2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo kwa manufaa ya Taifa bila ya idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili.

Wajibu wa Jamii

Wajibu wa kushiriki kazini

24. (1) Kazi pekee ndiyo huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu. Kila mtu anao wajibu wa-

(a) kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali; na

(b) kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji ya binafsi na yale ya pamoja yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria.

(2) Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1), hakutokuwapo na kazi ya shuruti katika Shirikisho.

(3) Kwa madhumuni ya ibara hii, na katika Katiba hii kwa jumla, ifahamike kwamba kazi yoyote haitahesabiwa kuwa ni kazi ya shuruti endapo kazi hiyo, kwa mujibu wa sheria ni-

(a) kazi inayobidi ifanywe kutokana na hukumu au amri ya mahakama.

(b) kazi inayobidi ifanywe na askari wa jeshi lolote katika kutekeleza majukumu yao;

(c) kazi ambayo mtu yeyote inabidi aifanye kutokana na kuwapo hali ya hatari au baa lolote linalotishia uhai wa ustawi wa jamii;

Wajibu wa kutii sheria za nchi

25. (1)Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na sheria za Shirikisho.

(2) Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.

(3) Bila kuathiri masharti ya Ibara hii kila mtu ana haki ya kupinga kufutwa kwa Katiba hii kinyume na utaratibu uliowekwa na Katiba hii.

Kulinda mali ya umma

26.(1) Kila mtu ana wajibu wa kuiheshimu mali ya mtu mwingine, kulinda mali asilia ya Shirikisho, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi.

Ulinzi wa taifa

27. (1) Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka , na umoja wa taifa.

(2)Bunge laweza kutunga Sheria zinazofaa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutumikia katika majeshi na katika ulinzi wa taifa.

(3) Kwa mujibu wa katiba hii ni marufuku kwa mtu yeyote kutia sahihi mkataba wa kukubali kushindwa vita na kulitoa taifa kwa mshindi, wala kuridhia au kutambua kitendo cha uvamizi au mgawanyiko wa Shirikisho au wa sehemu yoyote ya ardhi ya eneo la Taifa na;

(4) Bila ya kuathiri Katiba hii hakuna mtu atakayekuwa na haki ya kuwazuia raia wa Shirikisho kupigana vita dhidi ya adui yeyote anayeshambulia nchi.

(5) Uhaini kama unavyofafanuliwa na Ibara ndogo ya 6 ya Ibara hii utakuwa ni kosa la juu kabisa dhidi ya Shirikisho.

(6) Uhaini maana yake ni kitendo cha raia wa Shirikisho

(a) Kuonyesha nia ya kutenda vitendo vinavyokusaidia kuigawa Tanzania katika nchi tofauti.

(b) Kumuua, kujaribu kumuua au kula njama ya kumuua Rais wa Shirikisho , Waziri Mkuu wa Tanganyika ama Waziri Mkuu wa Zanzibar au

(c) Kuanzisha vita au kusaidia adui katika vita dhidi ya Shirikisho ama sehemu yoyote ya Shirikisho.

Masharti ya Jumla

Haki na wajibu muhimu

28. (1) Kila mtu katika Shirikisho anayo haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu, na matokeo ya kila mtu kutekeleza wajibu wake kwa jamii, kama zilivyofafanuliwa katika ibara ya 10 hadi ya 27 za sehemu hii ya sura hii ya Katiba.

(2) Kila mtu katika Shirikisho anayo haki ya kupata hifadhi sawa chini ya Sheria za Shirikisho.

(3) Raia yeyote wa Shirikisho hatakuwa na haki, hadhi au cheo maalum kwa misingi ya ubaguzi.

(4) Ni marufuku kwa sheria yoyote kutoa haki, hadhi inayotumika katika Shirikisho au cheo maalum kwa raia yeyote wa Shirikisho kwa msingi wa ubaguzi.

(5) Ili watu wote waweze kufaidi haki na uhuru vilivyotajwa na Katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.

29. (1) Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika sehemu hii ya Katiba hii, yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, haibatilishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo, kwa ajili ya-

(a) kuhakikisha ulinzi, usalama wa jamii na amani katika jamii;

(b) kuhakikisha utekelezaji wa hukumu au amri ya mahakama iliyotolewa katika shauri lolote la madai au kesi ya jinai;

(c) kulinda sifa, kutunza heshima, mamlaka na uhuru wa mahakama;

(d) kuweka vigezo vya uanzishaji, uendeshaji na shughuli za vyama na mashirika ya watu binafsi nchini;

(2) mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika sehemu hii ya sura hii au katika sheria yoyote inayohusu haki yake au wajibu kwake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote katika Shirikisho,

anaweza kufungua shauri katika Mahakama ya Shirikisho au Mahakama Kuu ya Tanganyika au Mahakama Kuu ya Zanzibar.

(3) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii, Mahakama ya Shirikisho au Mahakama Kuu ya Tanganyika au Zanzibar itakuwa na mamlaka ya kusikiliza kwa mara ya kwanza na kuamua shauri lolote lililoletwa mbele yake kwa kufuata ibara hii; na Bunge laweza kuweka sheria kwa ajili ya kusimamia utaratibu wa kufungua mashauri kwa mujibu wa ibara hii;

(4) Endapo katika shauri lolote inadaiwa kwamba sheria yoyote iliyotungwa au hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali au mamlaka nyingine inafuta au inakatiza haki, uhuru na wajibu muhimu zitokanazo na ibara ya 10 hadi 27 za Katiba hii, na Mahakama ya Shirikisho, Mahakama Kuu ya Tanganyika au Zanzibar inaridhika kwamba sheria au hatua inayohusika, kwa kiwango inachopingana na Katiba ni Batili au kinyume cha Katiba basi Mahakama ya Shirikisho au Mahakama Kuu ya Tanganyika au Mahakama Kuu ya Zanzibar itatamka kuwa sheria au hatua hiyo ni batili.

Madaraka ya Pekee ya Mamlaka ya Nchi

Ukiukaji wa haki na uhuru

30. (1) Mbali na masharti ya ibara ya 29(1), sheria yoyote iliyotungwa na Bunge haitakuwa batili kwa sababu tu kwamba inawezesha hatua kuchukuliwa wakati wa hali ya hatari, ambazo zinakiuka masharti ya ibara ya 12 na ya 13 za Katiba hii.

(2) Ni marufuku kwa hatua zilizotajwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara hii kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria yoyote wakati wa hali ya hatari, isipokuwa tu kwa kiasi ambacho ni lazima na halali kwa ajili ya kushughulikia hali iliyopo wakati wahali ya hatari.

(3) Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika ibara hii hayataidhinisha mtu kunyang’anywa haki yake ya kuwa hai.

(4) Kwa madhumuni ya ibara hii na ibara zifuatazo za sehemu hii "wakati wa hali ya hatari" maana yake ni kipindi chochote ambapo Tangazo la Hali ya Hatari, lililotolewa na Rais kwa kutumia uwezo aliopewa katika ibara ya 31, linatumika.

Madaraka ya kutangaza hali ya hatari

31. (1) Bila ya kuathiri Katiba hii, au sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, Rais aweza kutangazahali ya hatari katika Shirikisho au katika sehemu yake yoyote.

(2) Rais aweza tu kutangaza kuwa kuna hali ya hatari iwapo

(a) Shirikisho liko katika vita; au

((b) kuna hatari hasa kwamba Shirikisho linakaribia kuvamiwa na kuingia katika hali ya vita; au

(c) kuna hatari dhahiri na kubwa, kiasi kwamba amani ya jamii itavurugika na usalama wa raia kutoweka katika Shirikisho au sehemu yake yoyote ambayo haiwezi kuepukika isipokuwa kwa kutumia mamlaka ya pekee; au

(d) karibu kutatokea tukio la hatari au tukio la balaa au baa la kimazingira ambalo linatishia jamii au sehemu ya jamii katika Shirikisho.

(3) Endapo inatangazwa kwamba kuna hali ya hatari katika Shirikisho nzima, au katika Tanganyika nzima au Zanzibar nzima, Rais atatuma mara moja nakala ya tangazo hilo kwa Spika wa Bunge ambaye ataitisha mkutano wa Bunge, ndani ya siku zisizozidi kumi na nne, ili kuitafakari hali ya mambo na kuamua kupitisha au kutopitisha azimio, litakaloungwa mkono na kura za wajumbe wasiopungua theluthi mbili ya wajumbe wote, la kuunga mkono tangazo la hali ya hatari lililotolewa na Rais.

(4) Tangazo la hali ya hatari lililotolewa na Rais kwa mujibu wa ibara hii litakoma kutumika.

(a) wakati wowote ambapo mkutano wa Bunge utalitangua tangazo hilo kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za wajumbe wasiopungua theluthi mbili ya wajumbe wote.

(b) endapo zitapita siku kumi na nne tangu tangazo lilipotolewa kabla ya kupitishwa azimio lililotajwa katika ibara ndogo ya (3);

(c) iwapo litafutwa na Rais;

(d) baada ya kupita muda wa miezi mitatu tangu tangazo hilo lilipotolewa; isipokuwa kwamba kikao cha Bunge chaweza, kabla ya muda wa miezi mitatu kupita, kuongeza mara kwa mara muda wa tangazo hilo kutumika kwa vipindi vya miezi mingine mitatu kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za wajumbe wa kikao hicho wasiopungua theluthi mbili ya wajumbe wote, isipokuwa kwamba kipindi cha hali ya hatari hakitazidi miezi kumi na mbili.

(5) Bunge laweza kutunga sheria inayoweka masharti kuhusu nyakati na utaratibu ambao utawawezesha watu fulani wenye kusimamia utekelezaji wa mamlaka ya Serikali katika sehemu mahususi za Shirikisho kumuomba Rais kutumia madaraka aliyopewa na ibara hii kuhusiana na yoyote kati ya sehemu hizo endapo katika sehemu hizi kunatokea yoyote kati ya hali zilizotajwa katika aya ya (c) na (d) za ibara ndogo ya (2) na hali hiyo haivuki mipaka ya sehemu hizo; na pia kwa ajili ya kufafanua utekelezaji wa mamlaka ya Serikali wakati wahali ya hatari.

(6) Kwa madhumuni ya kuondoa mashaka juu ya ufafanuzi au utekelezaji wa masharti ya ibara hii, masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge inayohusu utangazaji wa hali ya hatari kama ilivyotajwa katika ibara hii, yatatumika tu katika sehemu ya Shirikisho ambapo hali hiyo ya hatari imetangazwa.



Thursday, April 14, 2011

DIWANI wa CHADEMA Kata ya Machochwe katika halmashauri ya wilaya Serengeti mkoa wa Mara Samwel Gibewa amesalimisha bunduki moja ikiwa na risasi zake 21 baada ya kubanwa na Mkuu wa Mkoa huo kanali Mstaafu Enos Mfuru . Diwani huyo amesalimisha silaha mbele ya kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo cha kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka 2011/12 hadi 2013/14. Gibewa alisema amelazimika kuisalimisha silaha hiyo aina ya SMG yenye 1960 KA 2823 ya nchi jirani ya Kenya baada ya kushambuliwa na madiwani wenzake ambapo awali alikana kuwa hana silaha yoyote ambayo anamiliki na kwamba madiwani hao ni waongo na pia ni wazushi. “Ni muda wa saa nzima sasa tumazungumzia suala lako,hivi hakuna ajenda nyingine zaidi ya kuanzisha Chuo Kikuu na silaha hiyo?”aliuliza Mfuru na kuongeza kuwa baada ya kikao kufunguliwa anaitaka silaha hiyo iwe imeshalimishwa kwake kwa usalama na iletwe mbele ya kikao cha baraza la Madiwani. “Lazima tuondoke wote ukanipe hiyo silaha,nasema.. leo lazima ukanipe hiyo silaha kwa nini tunapoteza muda kwa kuzxungumizia neon moja tu la silaha? Kanipe hiyo silaha ili ttuendelee na masuala mengine ya wananchi,tumefanya nini la maana badala ya kunga’ng’ania silaha tusipoteze muda watu wote hawa wankuzingizia?”Aliululiza Mfuru huku akiwa na sura ya makunyanzi. Akiwa katika kata ya Machochwe, Mkuu huyo wa Mkoa alikwenda nyumbani kwake na kukabidhiwa silaha hiyo ambayo alikuwa ameifukia kwenye kichuguu kilichoko nyumbani kwake. Kabla ya kwenda kufukua silaha hiyo Mkuu huyo alikwenda kuiona shule ya sekondari ya Machochwe ambayo kama itakuwa imekidhi kiwango cha kuwa Chuo Kikuu ifunguliwe,ambapo pia alikuwa ameitisha mkutano wa hadhara kuzungumza na wananchi kama kweli wamekataa shule hiyo na kwamba ikifunguliwa watachoma moto. Akikabidhi silaha hiyo mbele ya wananchi wa kata yake alisema kuwa silaha hiyo alipewa na kijana mmoja ambaye hakutaja jina lake amtunzie na kutangaza kuwa kama kuna mwanchi yeyote ana silaha akibidhi kwa jeshi la polisi. Aidha baada ya kurejesha silaha na kuonyesha mbele ya baraza la madiwani Mkuu huyo wa Mkoa aliomba baraza la madiwani kumsamehe kwani tayari amemsamehe mbele ya wananchi wa kata ya Machochwe. Naye Mwenyekiti wa Halmashauri,John Ng’oina amewatka madiwani kuzungumza ukwele badla ya kuzunsha taarifa za uongozi ba kuanchana na itikadi za vyama na balada yake watumike wananchi kama walivyowaahidi. “Ni vyema diwani akaachana na yaliyopita kuliko kutumia madaraka yake kukichafua chama na kwamba kama hana uzoefu aombe ushirikiana kwa walio na uzoefu” Alisema Ng’oina. Diwani huyo ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Jijini Mwanza, mwaka wa mwisho ambapo anasomea digrii ya kwanza ya elimu. Wiki hii wakazi wawili wa wilaya ya Serengeti,Marwa Mniko mkazi wa kijiji cha Nyamatare na Ngambarusu Ngaria wa kijiji cha Bwitengi walisalimisha silaha zao tatu aina ya SMG na Laifo kwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mara,Robert Boaz. Kutokana na matukio ya uhalifu na kumiliki silaha kinyume cha taratibu na sheria kukomaa,jitihada za makusudi zinahitaji ili kuhakikisha jina la Tanzani kuwa nchi ya Amani lizidi kudumishwa.

Tuesday, April 5, 2011

MOHAMMED TRANS YAUA

BASI la abiria kampuni ya Mohammed Trans lenye namba za usajili T597 APF aina ya Scania linalofanya safari zake kutoka Musoma-Dodoma limepata ajali leo asubuhi eneo la Sabasaba, Wilaya ya Musoma vijijini na kuua watu wapatao wawili.

Akizungumza na waandishi wa habari,kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Deusdedit Kato alisema ajali hiyo inatokana na mwendo kasi wa dreva wa basi hilo ambapo baada ya kupanda tuta lililowekwa katikati ya barabara basi hilo lilipinduka.

Aidha mtu mmoja ambaye amemtaja kwa jina la Ally Mohammed(30) hali yake siyo nzuri na amelazwa katika hospitali ya Mkoa iliyopo Manispaa ya Musoma na amewataja waliofariki dunia kuwa ni Tungaraza Ngeleja (70) na Martha Wedson Mwakatage Mkazi wa Rugwe mkoani Mbeya ambapo alikuwa anaishi Buhare Musoma.

Majeruhi wengine wapatao 10 walipata matibabu katika hospital ya Mkoa na kuruhusiwa kuondoka na dreva wa basi hilo, Hamidu Mohammed (38) anashikiliwa na jeshi la polisi.

Alisema kuwa jeshi la polisi Mkoa wa Mara lina mikakati mipya ya kuweka ratiba mpya za mabasi kwani basi hilo lilikuwa linafukuzana na mabasi mengine ambayo yalikuwa yametangulia sanjali na kuchunguza uwezo wa madreva ambao hawana taaluma hiyo.

Ametoa wito kwa abiria wanaosafiri kutoa taarifa kama dreva ana mwendo kasi ili hatua kali dhidi yao ziweze kuchukuliwa kabla ya tukio la ajali halijatokea kwani jeshi hilo linagawa vipeperushi vilivyo na namba ili watoe taarifa mapema.