

Na jenerali Ulimwengu.
MWAKA 2000, kabla ya uchaguzi mkuu, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilifanya mabadiliko ya kikatiba ambayo, miongoni mwa mambo mengine, yalibainisha kwamba mgombea urais anaweza kuchaguliwa na akakabidhiwa madaraka ya rais bila kulazimika kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.
Kwa wale waliojua kilichokuwa kikifanyika hii ilikuwa ni hatua muhimu sana, ingawaje haikupokelewa kwa kelele ambazo zilikuwa zinastahili. Umuhimu wake unatokana na kwamba mabadiliko hayo yalikuwa yanaingiza mbegu za utata mkubwa unaoweza kuikumba nchi hii huko tuendako, hata kama hivi sasa hatujui kwamba bomu limetegwa ila sisi hatujui.
Nitaeleza. Kukubali kikatiba na kisheria kwamba mgombea anaweza kuwa rais bila kulazimika kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa ni kukubali kwamba mtu anaweza kuwa rais bila kuwa na ridhaa, angalau, ya nusu ya wapiga kura wake. Ina maana kwamba, hata kama asilimia sitini, au sabini, au hata themanini wakimkataa, tena wakasema hivyo kwa kishindo, mtu huyo atakuwa rais alimradi ndiye aliyepata kura nyingi kuliko mgombea ye yote mwingine.
Tuchukue sura tuliyo nayo ya vyama vya siasa nchini Tanzania hivi leo. Tuseme kwamba vyama vinane vimewaweka wagombea wa nafasi ya urais, na vyama hivyo ni CCM, CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP, Democrasia Makini, DP na TPP.
Iwapo miongoni mwa wagombea wa vyama hivyo wagombea wa vyama saba, (tuseme CCM, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP, Demokrasia Makini, DP na TPP), watapata jumla ya asilimia 70 ya kura zilizopigwa, kisha mgombea wa CHADEMA akapata asilimia 30, mgombea wa CHADEMA atakuwa rais.
Mantiki ya uamuzi huo bado haijanielea, na wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa, kisheria na kikatiba wanasema haijawaelea. Ilikuwa vigumu zaidi (labda kuliko ilivyo leo) kuielewa wakati huo ikipitishwa kwa sababu ya tukio moja kuu la miaka mitano tu kabla ya uamuzi huu wa kushangaza. Nitalisimulia.
Mwaka 1995, mwishoni kabisa mwa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM pale Chimwaga, wagombea watatu wa mwisho waliopigiwa kura walikuwa Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Cleopa Msuya.
Kura zilipohesabiwa ikadhihirika kwamba hakuna mmoja aliyeweza kupata zaidi ya nusu ya kura, na kwa hiyo ikabidi wawili wa juu warudiane katika kile kinachoitwa run-off. Msuya alipata kura za chini zaidi, kwa hiyo run-off ikawa kati ya Kikwete na Mkapa, na Mkapa akashinda.
Najua wapo watu wanaodai kwamba ulikuwa uamuzi wa mzengwe; kwamba Kikwete alikuwa kashinda; kwamba Mwalimu Nyerere aliingilia kati “kumnusuru Mkapa” ; eti Mwalimu alimwambia Kikwete: Wewe bado kijana, mwachie mwenzako, zamu yako itakuja.
Hadithi hii nitaijadili mbele ya safari, lakini kwa sasa niseme tu kwamba si kweli. Katika majukumu ya mkutano mkuu wa CCM katika mwaka wa uchaguzi mkuu wa Taifa, mojawapo ni “kumchagua” mwanachama atakayegombea urais wa Jamhuri, na kwa mujibu wa katiba ya CCM uchaguzi katika nafasi ya aina hiyo hauna budi uheshimu kanuni mbili kuu, miongoni mwa nyingine: moja, uchaguzi uwe kwa kura ya siri; pili mshindi apatikane kwa zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.
Iwapo hivyo ndivyo ilivyo na ndivyo ilivyokuwa huko Chimwaga wakati huo; na iwapo matakwa hayo ya katiba ya CCM yalijengeka juu ya msingi wa mantiki fulani; na iwapo mantiki hiyo ndiyo iliyomfanya Mkapa awe mgombea wa CCM na siyo Kikwete; na iwapo mantiki hiyo ndiyo iliyotaka kwamba uchaguzi wa Taifa umpate rais kutokana na mgombea aliyepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa, sasa ni kwa nini mgombea aliyepitishwa kwa kanuni ya “zaidi ya nusu ya kura” katika chama chake aifutilie mbali kanuni hiyo kwenye ngazi ya Taifa kabla ya kugombea muhula wa pili?
Jibu rahisi ni kwamba washauri wa Benjamin Mkapa, wakati huo akiwa rais, hawakuamini, au yeye mwenyewe hakuamini kwamba angeweza kupata zaidi ya nusu ya kura ambazo zingepigwa katika uchaguzi wa 2000. Kwa hiyo, kama kawaida ya watawala wetu wanapotaka kukidhi maslahi yao bila ya kujali maslahi ya Taifa, ikaamuliwa kuiondoa ‘kero’ hiyo kutoka katiba ya Jamhuri.
Labda tungekumbushana kwamba wakati mabadiliko haya yanafanyika Mwalimu Nyerere alikwisha kuaga dunia, na tunajua sasa kwamba mambo mengi ya kifisadi yalifanyika wazi wazi pale watawala walipojua kwamba hakuna mtu mwenye kauli nzito angeweza kuwakemea hata wangefanya nini.
Kwa maneno mengine, kifo cha Mwalimu kilikuja kama fursa kwa kila aina ya ufisadi kuchanua bila kuchelea kusutwa. Sote tunajua kwamba Mwalimu katika miaka yake ya ustaafu alikuwa amejenga utamaduni wa kushiriki, kama raia ye yote anayejali, katika mijadala kuhusu mustakabali wa Taifa, na ni vigumu kuamini kwamba angekaa kimya kuhusu suala hili, kama ambavyo najua asingenyamaa kuhusu ule ufisadi mwingine unaohusu mali.
Kwamba Mkapa na watu wake walikuwa wametishika katika uchaguzi wa mwaka 1995 ni dhahiri, nami naweza kulirudia hili mara nyingi. Augustine Mrema alikuwa amechota akili za watu wengi kiasi cha kuifanya kampeni ya Mkapa iegemee zaidi nguvu ya ushawishi aliokuwa nao Mwalimu kwa watu wake walio wengi. Bila Mwalimu ilikuwa vigumu kuona ni jinsi gani Mkapa angeshinda.
Hata hivyo, mwaka 2000 mambo yalikuwa yamekwisha kubadilika sana. Kweli, Mwalimu alikwisha kuondoka, lakini Mkapa alikuwa amefanya kazi nzuri (kwa ujumla) katika miaka mitano ya uongozi wake, na wala hakuwa na sababu ya kuichezeachezea katiba ili kujihakikishia ushindi kwa njia yo yote ile, kitendo ambacho bila shaka kilizidisha nguvu ya uvumi kwamba hata Chimwaga 1995 utaratibu ulipindwa ili kumlinda Mkapa.
Hapa tunakumbana na suala kubwa, zito na la msingi. Kwa kubadili katiba kama ilivyoelezwa hapo juu, Mkapa na watu wake, hususan washauri wake wakuu akiwamo Mwanasheria Mkuu, waliitendea nchi hii haki?
Je, maslahi ya Mkapa na watu wake ya kurejea madarakani mwaka 2000 yalikuwa na ushawishi wenye uzani wa kutosha kuiingiza nchi katika utaratibu ambao hapo baadaye unaweza kuifanya nchi ikatawaliwa na mtu ambaye hatakiwi?
Je, kitendo cha kubadili katiba jinsi kilivyofanywa hakikuwa na maana ya kwamba Mkapa na washauri wake walikuwa radhi kubakia madarakani kwa njia yo yote ile, hata kama wananchi wangekuwa hawamtaki? Au siyo maana yake?
Hapa sitaki kuingia katika uchunguzi wa kazi hiyo muhimu waliyotaka kuifanya (Mkapa na watu wake katika muhula wa pili) hadi wakaichezea katiba (nitaijadili katika sura zijazo), bali tu nataka niseme kwamba kilikuwa kitendo cha hovyo, kitendo cha uhuni na kilichodhihirisha udhaifu mkubwa wa imani, yote ambayo leo hii hayashangazi.
Mwanademokrasia (dhahiri, Mkapa na washauri wake sio) hawezi kubadilisha kanuni za ushindani kwa sababu tu ameona kwamba zitamnyima ushindi. Atazibadili pale tu anaposhawishika kwamba kwa kuzirekebisha atatoa uhuru mkubwa zaidi kwa raia zake, ili sauti yao katika uendeshaji wa nchi isikike zaidi.
Katika awamu ya tatu tulizoea sana kusikia maneno “uvivu wa kufikiri” ambao, mimi nakiri, umejaa tele nchini mwetu, hususan miongoni mwa watawala wasiotaka kusumbua vichwa vyao kudurusu mifumo mbadala ya kuendeshea shughuli za utawala na maendeleo ya watu wao. Uvivu huo wa kufikiri unatokana na kwamba muda wao ulio mwingi wanashughulika na mambo mengine, ambayo hawakuyasema katika ilani zao.
Isingekuwa hivyo wangetumia muda mwingi zaidi kujadili nini kifanyike iwapo hakuna mgombe mmoja aliyepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa. Njia moja ni kufanya kama ilivyotokea Chimwaga 1995 Kikwete na Mkapa waliporudiana baada ya kumtoa Msuya. Njia nyingine ni ushirikiano, katika serikali, baina ya vyama vinavyokaribiana katika falsafa na mwelekeo. Kwa vyo vyote vile, mwaka 2000 hatukufika huko, kwani Mkapa, pamoja na woga wake wote, pamoja na kutojiamini, alishinda.
No comments:
Post a Comment