Tuesday, April 5, 2011

MOHAMMED TRANS YAUA

BASI la abiria kampuni ya Mohammed Trans lenye namba za usajili T597 APF aina ya Scania linalofanya safari zake kutoka Musoma-Dodoma limepata ajali leo asubuhi eneo la Sabasaba, Wilaya ya Musoma vijijini na kuua watu wapatao wawili.

Akizungumza na waandishi wa habari,kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Deusdedit Kato alisema ajali hiyo inatokana na mwendo kasi wa dreva wa basi hilo ambapo baada ya kupanda tuta lililowekwa katikati ya barabara basi hilo lilipinduka.

Aidha mtu mmoja ambaye amemtaja kwa jina la Ally Mohammed(30) hali yake siyo nzuri na amelazwa katika hospitali ya Mkoa iliyopo Manispaa ya Musoma na amewataja waliofariki dunia kuwa ni Tungaraza Ngeleja (70) na Martha Wedson Mwakatage Mkazi wa Rugwe mkoani Mbeya ambapo alikuwa anaishi Buhare Musoma.

Majeruhi wengine wapatao 10 walipata matibabu katika hospital ya Mkoa na kuruhusiwa kuondoka na dreva wa basi hilo, Hamidu Mohammed (38) anashikiliwa na jeshi la polisi.

Alisema kuwa jeshi la polisi Mkoa wa Mara lina mikakati mipya ya kuweka ratiba mpya za mabasi kwani basi hilo lilikuwa linafukuzana na mabasi mengine ambayo yalikuwa yametangulia sanjali na kuchunguza uwezo wa madreva ambao hawana taaluma hiyo.

Ametoa wito kwa abiria wanaosafiri kutoa taarifa kama dreva ana mwendo kasi ili hatua kali dhidi yao ziweze kuchukuliwa kabla ya tukio la ajali halijatokea kwani jeshi hilo linagawa vipeperushi vilivyo na namba ili watoe taarifa mapema.

No comments:

Post a Comment