WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda na Mkewe Mama Tunu Pinda wameongoza Mamia ya waombolezaji katika Maziko ya aliyemfundisha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu
Julius Nyerere katika Shule ya Msingi Mwisenge
Mjini Musoma,Mkoa wa Mara, Darasa la III na la IV Mwaka 1934, Marehemu James Irenge (120) katika mahame ya nyumbani kwao kijiji cha Busegwe Wilaya ya Butiama.
Akitoa
salama za pole kwa familia ya Marehemu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
amemtaja Mzee James Irenge kuwa alikuwa na dhamani kubwa katika nchi hii
kwani alimfundisha Baba wa Taifa na kwamba ndiye Mwalimu Mkuu wa Taifa
hili kwani ndiye aliyemjengea misingi bora na kwamba ndiye aliyepanda
mbegu bora kwa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kuwa
kiongozi bora, mhadilifu na mchakapakazi.
Aliitaka familia kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu ambapo
wamepoteza mtu muhimu ambaye walikuwa wanaendelea kupata baraka kutoka
kwake na malezi bora.
Amesema kuwa wakati wa Ziara yake ya Mwaka jana Marehemu Irenge alimwomba msaada wa chakula ambapo kwa jitihada za serikali zilitolewa
fedha kiasi cha Sh.300,000 kila mwezi na kwamba serikali haitaiacha
familia bila kutoa msaada kwani Mjane wake bado yupo hivyo itaendelea
kutoa huduma.
Aidha familia imeiomba Serikali kufuatilia kiinua mgongo na gharama za usafiri alizokuwa anadai Marehemu Mwalimu Irenge kutoka Mkoa wa Geita kuja Musoma alikokuwa anafanya kazi
kabla ya kustaafu kuanzia mwaka 1969 suala ambalo ni la muda mrefu sasa ambapo fedha hizo apewe mjane wa Marehemu,Josephina
Nyirembe ili zimsaidie.
Mwalimu James Irenge alifariki dunia nyumbani kwake Mwisenge katika Manispaa ya Musoma Julai 21
mwaka huu kwa ugojwa wa moyo,Baba yake alifariki dunia majira ya 4 usiku.
Waziri Mkuu na Mkewe Mama Tunu Pinda waliweka mashada ya maua katika kaburi la Mwalimu James Irenge.
Katika Uhai wake Mwalimu Irenge aliwahi kuwa Mkaguzi Mkuu wa
Elimu Kanda ya Ziwa, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Fulwe iliyoko Mkoa wa Geita
na baada ya kustaafu Mwaka 1969/1970 alianzisha
Kijiji cha ujamaa cha Hiyayabuyaga-Geita na mwaka 1980 aliendelea kuwa mkulima.Marehemu ameacha mjane, watoto 8 walioko hai, wajukuu 30,
vitukuu 20 na vilembwe 8.
Katika uhai wake na kuhitimisha miaka 120 duniani, amefariki
akiwa na meno yote kasoro jino moja ambalo aliwahi kuanguka na kulipoteza, pia
alikuwa hatumii miwani kuona.
Katika maziko hayo viongozi mbalimbali wa Chama na
Serikali walihudhuria akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu,Steven
Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bunda, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vicent
Nyerere na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Nimrode Mkono.