ALIYEMFUNDISHA BABA WA TAIFA, DRS LA I LA 11,
JAMES IRENGE(120) AFARIKI DUNIA.
MUSOMA.
ALIYEMFUNDISHA Mwalimu wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu
Julius Nyerere darasa la
Kwanza na la Pili katika shule ya Msingi Mwisenge
Mjini Musoma, Mkoa wa Mara, Mwaka 1934,James Irenge (120) amefariki dunia.
Mwalimu James Irenge alifariki dunia nyumbani kwake Mwisenge katika Manispaa ya Musoma Julai 21
mwaka huu kwa ugojwa wa moyo na uzee.
Akizungumza na Uhuru nyumbani kwa marehemu jana, msemaji wa
familia Josiah Irenge alisema kuwa Baba yake alifariki dunia majira ya 4 usiku
akiwa nyumbani kwake na baadae mwili wake ukapelekwa kuhifadhiwa katika chumba
cha kuhifadhia maiti kilichoko katika hospitali ya Mkoa mjini Musoma.
Akizungumza kwa majonzi alisema kuwa ameshangazwa na
Madaktari ambao waliagizwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kumfanyia matibabu
kutofika kabisa tangu Waziri huyo alifika mwaka jana Mjini Musoma kwa Ziara ya
kikazi.
“Nakumbuka baba wakati wa uhai wake alimwomba Waziri Mkuu kuwa
awe anapata matibabu na akaagiza madaktari kumpatia matibabu lakini cha
kushangaza tangu siku hiyo hawakuonekana na hivyo kuilazimu familia kuendelea
kumuhudumia hadi mauti ilipompata”
Alisema Josiah na kuongeza kuwa anaishukuru
serikali kwa kuleta pesa za chakula
ambazo pia aliomba kwa Waziri Mkuu ambapo zilipelekwa Sh.300,000 mara tatu tangia mwaka jana.
Alisema wakati wa uhai wake Mwalimu Irenge alikuwa anadai kiinua mgongo na
gharama za usafiri kutoka Mkoa wa Geita kuja Musoma alikokuwa anafanya kazi
kabla ya kustaafu kuanzia mwaka 1969 na kuiomba serikali kuingilia kati suala
hilo ambalo ni la muda mrefu na fedha hizo apewe mjane wa Marehemu,Josephina
Nyirembe ili zimsaidie.
Katika Uhai wake Mwalimu Irenge aliwahi kuwa Mkaguzi Mkuu wa
Elimu Kanda ya Ziwa, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Fulwe iliyoko Mkoa wa Geita
na baada ya kustaafu Mwaka 1969/1970 alianzisha
Kijiji cha ujamaa cha Hiyayabuyaga-Geita na mwaka 1980 aliendelea kuwa mkulima,
.Marehemu ameacha mjane, watoto 12, wajukuu zaidi ya 30,
vitukuu 20 na vilembwe 8.
Katika uhai wake na kuhitimisha miaka 120 duniani, amefariki
akiwa na meno yote kasoro jino moja ambalo aliwahi kuanguka na kulipoteza, pia
alikuwa hatumii miwani kuona.
Aidha aliipongeza kampuni ya uhuru Publication kwa ufuatiaji
na umakini wao katika kuhabarisha Umma na hatimaye kusaidia kijana na marehemu
,Nassoro Irenge ( Bondia) ambaye alikuwa amepatwa na mkasa wa kesi isiyo yake
nchini Afrika Kusini na kurejea nchini jambo
ambalo marehemu aliiomba asaidiwe na kufanikiwa.
Maziko yanatarajiwa kuwa Alhamisi,julai 26 katika Mahame ya kijijini kwao Busegwe Wilaya ya Butiama, ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa kuongoza mamia ya waombolezaji katika maziko hayo.
No comments:
Post a Comment