Friday, July 27, 2012

WAZIRI MKUU AONGOZA MAZIKO YA MWALIMU WA BABA WA TAIFA

BUTIAMA.
WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda na Mkewe Mama Tunu Pinda wameongoza Mamia ya waombolezaji  katika Maziko ya aliyemfundisha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere katika  Shule ya Msingi Mwisenge Mjini Musoma,Mkoa wa Mara, Darasa la III na la IV Mwaka 1934, Marehemu James Irenge (120) katika mahame ya nyumbani kwao kijiji cha Busegwe Wilaya ya Butiama.

Akitoa salama za pole kwa familia ya Marehemu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  amemtaja Mzee James Irenge kuwa alikuwa na dhamani kubwa katika nchi hii kwani alimfundisha Baba wa Taifa na kwamba ndiye Mwalimu Mkuu wa Taifa hili kwani ndiye aliyemjengea misingi bora na kwamba ndiye aliyepanda mbegu bora kwa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kuwa kiongozi bora, mhadilifu na mchakapakazi.


Aliitaka familia kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu ambapo wamepoteza mtu muhimu ambaye  walikuwa wanaendelea kupata baraka kutoka kwake na malezi bora.


Amesema kuwa wakati wa Ziara yake ya Mwaka jana Marehemu Irenge alimwomba msaada wa chakula ambapo kwa jitihada za serikali  zilitolewa  fedha kiasi cha Sh.300,000 kila mwezi na kwamba serikali haitaiacha familia bila kutoa msaada kwani Mjane wake bado yupo hivyo itaendelea kutoa huduma.


Aidha familia imeiomba Serikali kufuatilia kiinua mgongo na gharama za usafiri alizokuwa anadai Marehemu  Mwalimu Irenge kutoka Mkoa wa Geita kuja Musoma alikokuwa anafanya kazi kabla ya kustaafu kuanzia mwaka 1969 suala  ambalo ni la muda mrefu sasa ambapo fedha hizo apewe mjane wa Marehemu,Josephina Nyirembe ili zimsaidie.

Mwalimu James Irenge alifariki dunia nyumbani kwake  Mwisenge katika Manispaa ya Musoma Julai 21 mwaka huu kwa ugojwa wa moyo,Baba yake alifariki dunia majira ya 4 usiku.

Waziri Mkuu na Mkewe Mama Tunu Pinda waliweka mashada ya maua katika kaburi la Mwalimu James Irenge.


Katika Uhai wake Mwalimu Irenge aliwahi kuwa Mkaguzi Mkuu wa Elimu Kanda ya Ziwa, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Fulwe iliyoko Mkoa wa Geita na baada ya kustaafu Mwaka 1969/1970 alianzisha  Kijiji  cha  ujamaa cha Hiyayabuyaga-Geita  na mwaka 1980 aliendelea kuwa mkulima.Marehemu ameacha mjane, watoto 8 walioko hai, wajukuu  30, vitukuu 20 na vilembwe 8.

Katika uhai wake na kuhitimisha miaka 120 duniani, amefariki akiwa na meno yote kasoro jino moja ambalo aliwahi kuanguka na kulipoteza, pia alikuwa hatumii miwani kuona.



Katika maziko hayo viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali walihudhuria akiwemo Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu,Steven Wasira ambaye pia ni  Mbunge wa Jimbo la Bunda, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vicent Nyerere na  Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Nimrode Mkono.

Ibada ya Maziko iliongozwa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mara, Helkia Omindo.

No comments:

Post a Comment