MUSOMA.
Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Musoma umezindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Miradi iliyozinduliwa ni pamoja na ufunguzi wa matanki matano ya maji yenye uwezo kuchukua lita 5000 za maji katika Shule ya Sekondari ya Ufundi ( Musoma Alliance) ambapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewahi kusoma hapo.
Akizungumza mara baada ya kweka jiwe la Msingi kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Capt. Honest Erenest Mwanosa alisema uwekaji wa huduma hiyo itawasaidia wanafunzi hao kufanya masomo yao badala ya ile ya awali ya kutembea hatua kadhaa kwenda ziwani kuyatafuta hali ambayo ilikuwa inawapa shida wanafunzi.
Aliwataka pia wanafunzi hao kusoma kwa bidii kwani elimu ndio msingi wa maisha, badala ya kuweka migomo isiyo ya lazima.
Akizungumza na Mliki wa Blog hii, Mwanafunzi wa kidato cha tano katika Sekondari hiyo, Sabaya Kinyi alitoa shukrani kwa Serikali na kuiomba kufanya ukarabati shule hiyo ambayo majengo yake ni muda mrefu na sasa yanaelekea kuwa chakavu pia kuongezewa walimu kwani shule hiyo ina upungufu wa walimu.
Mwenge huo ukiwa Kata ya Bweri-Songe, uliweka jiwe la msingi kwenye nyumba bora ya mwananchi iliyogharimu kiasi ya Sh Milioni 180.
Aidha uliweka jiwe la msingi vyumba viwili vya maabara ya sekondari ya Bweri ambavyo mara baada ya kukamilika utagharimu kiasi cha Sh. Milioni 68 ambapo sasa umegharimu Sh. Milioni 34 na kuzindua klabu ya TAKUKURU.
Akisoma hotuba kwa Kiongozi huyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Bweri, Alphonce Kameta, alisema Mradi huo utakapokamilika wanafunzi watapata fursa nzuri ya kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo na hivyo kupata maarifa na ujuzi wa kutosha kuwawezesha kufanya vyema katika masomo ya Sayansi.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya wapinga rushwa wa Shule ya Sekondari Kamunyonge, Salum Masesa alisema kuwa klabu za wapinga rushwa ambayo kwa sasa ina wanafunzi 20, imeanzishwa kwa lengo la kuwajenga wanafunzi kimaadili na kuwashirikisha katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwawezesha kutambua nafasi na wajibu wao katika mapambano ya rushwa na hivyo kushiriki ipasavyo kuzuia na kupambana na rushwa
Alisema kutoka na elimu waliyipata na wanayoendelea kuipata wako tayari kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa, kukemea,kuelimisha wanafunzi wenzao na jamii kwa ujuml ana kwamba tayari kulitumikia Taifa kwa uaminifu mkubwa.
Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika wodi ya watoto iliyoko Nyakato, ambapo Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Nyakato, Shadrack Ndaro, alitoa taarifa ya ujenzi wa wodi hiyo kwamba kwa kipindi cha Mwaka 2010/2011 awamu ya kwanza zilitumika Sh. Milioni 30 hadi hatua ya kupaua na michango ya wananchi Sh. Milioni 2 na hadi kukamilika utagharimu jumla ya Sh. Milioni 56 fedha ambazo zimetokana na Mradi wa CDG (central Development Government).
Aidha Mwenge huo uweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Kwangwa kilometa 2, kufungua vyumba vinne vya madarasa shule ya msingi kigera vilivyogharimu Sh. Milioni 62.2 na kupanda miti ya vivuli na matunda pia kufungua jengo la kuhifadhia maiti (Mochwari)lililogharimu Sh. Milioni 190 hadi kukamilika, jengo ambalo ndani yake lina ofisi sanjali na Kantini ya Chuo cha VETA ambayo imegharimu Sh.Milioni 18.8, kukagua na kuhamasisha kikundi cha vijana cha useremala na Saccos ya akinamama iliyoko uwanja wa Mpira wa Karume.
Mwenge huo umemaliza Mbio zake Mkoa wa Mara na huko Wilaya ya Bunda.