Thursday, August 9, 2012

MAKARANI WAANDAMIZI WA SENSA WAPATA MAFUNZO


 MUSOMA.

Makarani waandamizi wasimamizi wa Washiriki wa Sensa ya watu na makazi wameombwa kufuatilia na kusikiliza kwa makini mafunzo watakayopewa na wawezeshaji wa zoezi hilo ili kuleta ufanisi katika zoezi hilo.

Hayo yamesemwa LEO na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome wakati akifungua semina kwa  Makarani Waandamizi na wasimamizi wa sensa na makazi katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara.

Jackson Msome amesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kupata mbinu za kuuliza maswali, namna ya kujaza dodoso refu na  taarifa mbalimbali za kaya na   kutambua namna ya kuhifadhi siri na taarifa za kaya ambazo wamezipata.

Amesema kamati imewaamini kufanya kazi hiyo hivyo washiriki wanaombwa watambue dhamana kubwa waliyopewa na serikali hivyo ufanisi na uhodari wao katika kazi utapimwa kwa mafanikio ya sensa iyo itakayoanza Agosti 26, 2012.

Aidha  Serikali inapenda kuona sensa hiyo ikipata mafanikio makubwa hivyo semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo mkubwa na ufanisi ili kila wilaya ifanikishe zoezi hilo kwa ufanisi zaidi kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.

Aidha ametaka viongozi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari kwani ndio sekta muhimu katika kuelimisha wananchi kuhusiana na sensa ya watu na makazi na kwamba vyombo vya habari vina nguvu na mchango mkubwa katika kutoa elimu ya uhamasishaji hivyo ni vema kama vyombo hivyo vitatumia nafasi hiyo kuhamasisha  wananchi ili watoe ushirikano wa  kutosha katika zoezi hilo.


Mafunzo hayo ya Sensa ya watu na makazi yamefunguliwa rasmi Agosti 9 katika Wilaya ya Musoma  na jumla ya washiriki wapatao 200 wamehudhuria mafunzo hayo na kwamba yatafanyika muda wa  siku kumi na moja.

No comments:

Post a Comment