Saturday, November 12, 2011

UKAGUZI WA SHULE WILAYA YA RORYA ZERO!!!!

RORYA.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rorya, Cosmas Ngangaji, amesikitishwa na mahudhurio mabaya ya wanafunzi wa shule ya Msingi Irienyi,pamoja na shule zipatazo 30 kutokaguliwa kwa takribani miaka saba, wakati wakaguzi wa shule walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya shule za Msingi katika Wilaya ya Rorya.

Aliyasema hayo,wakati akizungumza na Blog hii, juu ya matatizo yanayoikabili Wilaya hiyo kwa upande wa elimu,mara baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Novemba 11.

Alisema kuwa wakaguzi hao walifanya ziara mapema septemba 10 mwaka huu na kubaini upungufu mkubwa wa mahudhurio ya wanafunzi kutoka wanafunzi 788 wanaopaswa kuwa madarasani na kukuta wanafunzi 217 tu sawa na asilimia 27.5.

Alisema kuwa katika hali isiyo ya kawaida kuna shule zipatazo 30 ambazo haizijawahi kukaguliwa kati ya miaka 6-7 na kwamba zina hali mbaya sana.

Aliongeza kuwa pamoja na matatizo hayo pia kuna upungufu mkubwa wa wa madawati hasa shule ya msingi Ryagati ambapo jumla ya madawati 193 yanahitajika na kwamba mpaka sasa yapo madawati 47,kwa kuwa haikupata mgao wa madawati ya Mbunge wa jimbo la Rorya,Lameck Airo na mgao kutoka mfuko wa jimbo.


Aidha umefanyika pia ukaguzi maalumu kwa kata zipatazo mbili za Bukwe na Nyathorogo kwa shule za Msingi za Chuchuri na Mori ambazo pia zina mapungufu ikiwa ni pamoja na kuongeza ujenzi wa vyumba za madarasa katika shule ya Msingi Chuchuri,ambapo Shule ya Msingi Nyathorogo imeaza ujenzi wa vumba viwili vya madarasa ya awali.

Wednesday, November 2, 2011

KWA KHERI MDOGO WANGU.

KWA KHERI MDOGO WANGU OLIVA VEDASTUS MASHAURI, ULITUTOKA TAREHE 28.10.2011, UTAKUMBUKWA NA MWANAO MPEDWA, VEDASTUS.BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LITUKUZWE.

Wednesday, October 26, 2011

MTOTO MCHANGA ATUPWA AKUTWA HAI.

MUSOMA.


MTOTO Mchanga wa jinsia ya kike anayekadiriwa kuwa wa wiki mbili ,Agosti 25 ameokotwa akiwa ametupwa kwenye korongo katika Mtaa wa Mtakuja na Zanzibar, kata ya Mwisenge,kikiwa kimetupwa na mtu asiyejulikana.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishina Msiadizi wa Polisi (ACP),Robert Boaz alisema kuwa mtoto huyo amegunduliwa na watoto wa shule ya Msingi wa Tatu Issa (32) walipokuwa wakipita kwenye korongo hilo wakielekea shuleni na ndipo waliporudi nyumbani kumpatia taarifa Mama yao.

Alisema Mama huyo alimkuta mtoto huto akiwa mtupu na alikuwa hai ,ndiopo alipotoa taarifa kwa Polisi,mtoto huyo amehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa wa Mara iliyoko katika Manispaa ya Musoma.

Aidha ametoa wito kwa watu ambao wanahisi kuna mama alikuwa mjazito na hana ujauzito watoe taarifa kituo cha Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Katika tukio jingine lililotokea katika wilaya ya Bunda, majira ya saa 10 jioni stend ya Mabasi, mtoto mchanga wa jinsia ya kiume wa Chausiku Kelaryo( 21), mwenye umri wa wiki moja na nusu ameibiwa.

Alisema Chausiku alimwachia Mama mmoja asiyemfahamu kumshikia ili akanunue mboga sokoni, kutoka sokoni akakuta mama huyo ametoweka na mwanae.

Ametoa wito kwa wakazi wa Wilaya hiyo kama kutakuwa na utata juu mama huyo na kwamba hakuwa na ujauzito watoe taaifa kituo cha Polisi ili hatua dhidi ya mama huyo zichukuliwe.

NOTI BANDIA ZAKAMATWA



MUSOMA.

JUMLA ya noti bandia zipatazo 16 za Sh 10,000 na Sh. 5,000 zipatazo 12 zimekamatwa katika Manispaa ya Mji wa Musoma.


Akizungumza na Mwandishi wa habari hii ofisini kwake Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Mkoa wa Mara, Robert Boaz alisema tukio hilo limetokea Agosti 24 mwaka huu katika mtaa wa Jamatini majira ya saa 2 usiku katika Super Market ya Msendo wakati mteja akinunua vocha ya Sh.5,000.

Alisema baada ya kuugundua si noti halali alipiga simu kwa askari wa doria na kumkamata mtuhumiwa aliyemtaja kuwa Mashaka Samson, mkazi wa Musoma Mjini mtaa wa Karume.

Kamanda Boaz alisema noti hizo zilikuwa na namba tofauti tofauti ambapo noti zipatazo nane za Sh.5,000 zilikuwa na namba aina moja AA 084 598 na nne zikiwa na namba ADO 845 927, noti za 10,000 zilikuwa nne , tatu zikiwa na namba BB 0315203 na moja ikiwa na namba BC 031 5209.

Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kujibu mashitaka.


Saturday, October 22, 2011

VIONGOZI WA MWENGE 2010


Mkimbiza Mwenge kitaifa, Nassoro Ally Matuzya akifuraia mara baada ya kukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

KAMPUNI YA SIMU TANZANIA YAHUJUMIWA.

MUSOMA.



KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) Mkoa wa Mara imehujumiwa kwa kukatiwa mikongo ya simu yenye urefu wa Mita 4,000 na wananchi wasio wema na kusababisha hasara kubwa ya Mamilioni ya fedha kwa kipindi cha miezi sita.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa na Mwandishi wa habari hii ofisini kwake wakati wa mahojiano, Meneja wa kampuni hiyo, Richard Augustine alisema ingawaje kampuni inajitahidi kutoa huduma nzuri kwa wakazi wa Mji wa Musoma na Tarimr lakini inakubiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisema kwa sasa wakazi wa kata za Bweri machinjioni na Rwamlimi na Wilani Tarime ambao wanakosa huduma hiyo muhimu majumbani kwao kutokana na tatizo hilo ambalo limeipatia kampuni hasara ya kiasi cha Sh Milioni 50.

Aliongeza kuwa ukaratabati wa miundo mbinu ya kupitisha maji, barabara imekata baadhi ya mikongo maeneo ya kiwanda cha Nguo cha Mutex suala ambalo linashughulikiwa ili kiwanda hicho kiweze kuendelea kupata huduma.

“Suala hili la ukarabati wa barabara na upitishaji maji ni lazima tuwe tunashirikiana ili kuepuka gharama zingine zisizo za lazima, pia suala la ushirikiano baina ya vyombo vya dola na kampuni yetu ni jambo la msingi sana ili kuhakikisha vitendo vya namna hii vinatokemea,kwani wahujumu hawa wanafahamika na wengine tumekuwa tukiwakamata na ni wezi sugu wanafahamika”Alisema Richard.

Akizungumzia kuhusu kutanua wigo wa mtandao alisema kampuni ina mkakati huo kwani kwa sasa huduma ya simu ya mkononi ya TTCL Mobile haifiki maeneo mengi ukilinganisha na kampuni zingine, sanjali na mtandao wa Broad band ambao kwa sasa watumiaji wengi wamekuwa wakifahidika nayo.

Akizungumzia juu ya kupanda kwa gharama za umeme alisema gharama zimekuwa kubwa kulinganisha na awali ambapo huduma hiyo ilikuwa ikipatikana,haipungui japo kuwa kuna mgao na kwa maeneo mengine yameathiri utendaji kwa kampuni hiyo, kutokana na matumizi makubwa ya mafuta kwenye generator, huku Ankara pia zikipanda.



“Nilifikiri gharama zitapungua kutokana na mgao wa umeme,lakini cha ajabu tumekuwa tukitumia mafuta kwa wengi tukijua Ankara za Tanesco zitapungua lakini imekuwa kinyume zinakwenda sambamba” Alisema Richard kwa mshangao.


UWEKAJI MAMBOMBA YA MAJI WAKWAMA

BUNDA.

MKANDARASI ambaye alikuwa aanze kazi ya ujenzi wa miundo mbinu katika Mradi wa Maji wa vijiji vya Mugeta na Nyang’aranga katika Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara hajaanza kazi hadi apatikane mtaalamu mshauri wa Mkandarasi.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii, Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bunda, Tanu Deule alisema kuwa limetolewa agizo kutoka Wizara ya Maji jijini Dar es Salaam kuwa huduma ya kutandaza mabomba isitishwe kwanza hadi atakapopatikana Mtaalamu MShauri wa Mkandarasi huyo.

Jiwe la Msingi la Ujenzi wa mradi wa maji wa Mugeta na Nyang’aranga katika Wilaya ya Bunda liliwekwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa na ziara yake ya kikazi Mkoa wa Mara ulitarajiwa kuanza septemba mwaka huu.

Mradi wa maji wa vijiji vya Mugeta na Nyang’aranga umebuniwa ili kusaidia wananchi wapatao 5,000 wa vijiji hivyo kuondokana na adha ya kutafuta maji yasiyo salama kwenye umbali mrefu.

Lengo ni kuwawezesha wapate maji safi na salama karibu na makazi yao ili waweze kuwa na afya bora na kutumia muda wao kwa shughuli za maendeleo na kuboresha mahudhurio ya wanafunzi shuleni.

Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bunda Tanu Deule alisema Mradi huo unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 5000 kwa saa, ujenzi wa bomba kuu la kupeleka maji kwenye tanki umbali wa kilomita 1. 982, ujenzi wa mtandao wa mabomba kilomita 31.158 ya kusambaza maji kwa watumiaji, Ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji, ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000, kuweka mfumo wa umeme kwenye kisima cha maji, Ujenzi wa nyumba ya pampu na usimikaji wa pampu ya kusukuma maji.

Mradi huo unajengwa kwa ubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Japani kupitia mfuko wa “Tanzania/Japan Food Aid Counterpart Fund (FACF) ulio chini ya Wizara ya Kilimo na Chakula.

Mradi unakadiriwa kugharimu jumla ya Tsh 270,000,000,Serikali ya Japani (J FACF) itatoa Tsh 240,000,000,Serikali ya Tanzania kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Bunda itatoa Tsh 23,000,000 ,Wananchi watachangia nguvu zao sawa na Tsh. 7,000,000

Mpaka sasa Halmashauri imekwisha pokea kiasi cha Tshs 107,000,000 kutoka Serikali ya Japan na Tshs 90,778,809 zimetumika, na Halmashauri imekwisha toa Tshs 3,000,000.

Aidha Kazi ambazo tayari zimekwisha kufanyika ni pamoja na uchimbaji wa kisima kirefu na Ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 kwenye nguzo ya urefu wa mita 10 katika kijiji cha Mugeta.

Sanjali na hilo kuna kazi ambazo bado hazijafanyika ikiwa ni pamoja na kununua mabomba na kuyalaza kwenye njia kuu na njia ya kusambaza maji kwa watumiaji, kuvuta umeme hadi kwenye kisima cha maji, kununua pampu na kuisimika na kujenga nyumba ya pampu.