Saturday, October 22, 2011

UWEKAJI MAMBOMBA YA MAJI WAKWAMA

BUNDA.

MKANDARASI ambaye alikuwa aanze kazi ya ujenzi wa miundo mbinu katika Mradi wa Maji wa vijiji vya Mugeta na Nyang’aranga katika Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara hajaanza kazi hadi apatikane mtaalamu mshauri wa Mkandarasi.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii, Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bunda, Tanu Deule alisema kuwa limetolewa agizo kutoka Wizara ya Maji jijini Dar es Salaam kuwa huduma ya kutandaza mabomba isitishwe kwanza hadi atakapopatikana Mtaalamu MShauri wa Mkandarasi huyo.

Jiwe la Msingi la Ujenzi wa mradi wa maji wa Mugeta na Nyang’aranga katika Wilaya ya Bunda liliwekwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa na ziara yake ya kikazi Mkoa wa Mara ulitarajiwa kuanza septemba mwaka huu.

Mradi wa maji wa vijiji vya Mugeta na Nyang’aranga umebuniwa ili kusaidia wananchi wapatao 5,000 wa vijiji hivyo kuondokana na adha ya kutafuta maji yasiyo salama kwenye umbali mrefu.

Lengo ni kuwawezesha wapate maji safi na salama karibu na makazi yao ili waweze kuwa na afya bora na kutumia muda wao kwa shughuli za maendeleo na kuboresha mahudhurio ya wanafunzi shuleni.

Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bunda Tanu Deule alisema Mradi huo unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 5000 kwa saa, ujenzi wa bomba kuu la kupeleka maji kwenye tanki umbali wa kilomita 1. 982, ujenzi wa mtandao wa mabomba kilomita 31.158 ya kusambaza maji kwa watumiaji, Ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji, ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000, kuweka mfumo wa umeme kwenye kisima cha maji, Ujenzi wa nyumba ya pampu na usimikaji wa pampu ya kusukuma maji.

Mradi huo unajengwa kwa ubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Japani kupitia mfuko wa “Tanzania/Japan Food Aid Counterpart Fund (FACF) ulio chini ya Wizara ya Kilimo na Chakula.

Mradi unakadiriwa kugharimu jumla ya Tsh 270,000,000,Serikali ya Japani (J FACF) itatoa Tsh 240,000,000,Serikali ya Tanzania kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Bunda itatoa Tsh 23,000,000 ,Wananchi watachangia nguvu zao sawa na Tsh. 7,000,000

Mpaka sasa Halmashauri imekwisha pokea kiasi cha Tshs 107,000,000 kutoka Serikali ya Japan na Tshs 90,778,809 zimetumika, na Halmashauri imekwisha toa Tshs 3,000,000.

Aidha Kazi ambazo tayari zimekwisha kufanyika ni pamoja na uchimbaji wa kisima kirefu na Ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 kwenye nguzo ya urefu wa mita 10 katika kijiji cha Mugeta.

Sanjali na hilo kuna kazi ambazo bado hazijafanyika ikiwa ni pamoja na kununua mabomba na kuyalaza kwenye njia kuu na njia ya kusambaza maji kwa watumiaji, kuvuta umeme hadi kwenye kisima cha maji, kununua pampu na kuisimika na kujenga nyumba ya pampu.


No comments:

Post a Comment