Sunday, December 25, 2016

MBUNGE WA JIMBO LA MUSOMA VIJIJIJI AWAASA WAUMINI WA KANISA LA MENNONITE.



MUSOMA.
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka Waumini wa kanisa la Mennonite kata ya Nyakatende vijiji vya Nyakatende na Kamuguruki, kuachana na tabia za ugomvi bali wapendane ,waungane na kudumisha Amani kwa mujibu wa Imani ya Kikristo.

Mbunge huyo ambaye alijumuika na waumini wa kanisa hilo kusherehekea sikukuu ya kuzaliwa Yesu kristo karne nyingi zilizopita alisema kuwa si jambo jema kuendeleza ugomvi bali wawe pamoja kwa kuwa na upendo kama Yesu alivyokuwa hapa duniani.

Aliwataka kuachana na malumbano yasiyo na misingi bali wawe kitu kimoja na kufanya shughuli za maendeleo, hususani ujenzi wa shule, zahanati, nyumba za walimu na makanisa.

Aidha Mbunge huyo alimwagiza msaidizi wake kwa kanda ya Nyanja, Juma Shaban kufanya tathimini ya gharama za mahitaji ya ujenzi wa kanisa la Menonite la vijiji vya Nyakatende na Nyasurula .

Akiwa katika kijiji cha Kamuguruki alisema kuwa katika jimbo zima kuna upungufu wa vyumba vya madarasa shule za msingi na Sekondari vipatavyo 748, ambapo tayari makotena ya saruji na mabati yameagizwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba hivyo.

Aidha amekabidhi vifaa vipatavyo 10 vya umeme wa jua vitavyotumika kwa ajili ya mwanga na kuchaji simu kwa ajili ya majaribio, ambapo mara baada kujaribishwa timu ya wataalamu kutoka korea watakuja kutoa elimu kwa vijana waliomaliza kidato cha Nne wa jimbo hilo kufundishwa ili waweze kupata utaalamu na ujuzi wa kuvitengeneza ambapo watajipatia kipato kutokana na uuzwaji wa vifaa hivyo kwa kila kifaa kiasi cha Sh.15,0000.

Akitoa ibada kwa waumini hao, Askofu wa Kanisa la Menonite, Dayosisi ya Mara na Mwanza(mstaafu), Jairo Onyengo aliwataka vijana wanawake na wanaume kutumia ujana wao vizuri,kwa kumkumbaka bikira Maria ambaye alipata ujauzito kwa njia ya roho Mtakatifu.

‘’Ni vijana wangapi na mabinti kwa sasa ambao unaweza kushuhudia kama bikira, na ndiyo maana ugonjwa wa Ukimwi unaendelea kuwepo kutokana na maadili yasiyo mpendeza mwenyezi Mungu,..Utii ni bora kama mafuta ya beberu aliongeza Askofu huyo.

Alisema sikukuu hii ni maalumu kwa kuomba na kumshukuru Mungu na si ilivyo sasa kwa walio wengi wakifanya mkesha kwa uasheretari kwenye madangulo wakiutafuta ukimwi na kulewa pombe na hata katika sikukuu yenyewe,bali Yesu alikuja kutukomboa ili tutubu na kuepukana na maovu.

No comments:

Post a Comment