Monday, December 16, 2013

KEGONGA WAOMBA ENEO KATIKA HIFADHI YA SERENGETI


NYANUNGU-TARIME.

WAKAZI wa Kijiji cha kegonga kata ya Nyanungu Wilaya ya Tarime wameiomba hifadhi ya Taifa ya Serengeti kugawa eneo la malisho ya mifugo katika bonde hilo ili kuondoa mgogoro uliopo.

Wakizungumza na waaandishi wa habari waliokuwa na ziara katika maeneo ya bonde hilo wananchi hao wameiomba pia Serikali kuangalia upya mipaka iliyowekwa kwa ajili ya kutenga eneo la hifadhi ya mbuga ya Serengeti na eneo la kilimo na mifugo.

Hata hivyo maisha duni na uelewa mdogo wa sheria mpya kwa wakazi wa bonde hilo ndicho chanzo cha kuwepo kwa migongano kati yao na hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa).

Elimu ya ufugaji bora na kilimo inatakiwa kutolewa kwa wakazi wa bonde hilo lililoko Wilaya ya Tarime ambalo linapakana na hifadhi hiyo ili kuondokana na migogoro mbalimbali inayojitokeza katika bonde hilo.

Vile vile imeonekana kuwa Maafisa ugani hawatembelei katika maeneo hayo ili kuwasaidia wananchi juu ya kilimo na ufugaji bora wa kisasa ambao una tija kwa wananchi.

Elimu hiyo itasaidia mfumo wa maisha duni waliyonayo wakazi hao ili kwenda maisha bora kwani wana mifugo mingi ambayo wangeweza kuiuza na kubakiza mifugo michache wangeweza kusomesha watoto wao pia kujenga nyumba bora.

Naye Lucia Mariane alisema kuwa kuwa chanzo ya mgogoro huo ni eneo la kuchungia na kulima ambapo alidai kuwa kwa muda mrefu walikuwa wakilitegemea bonde hilo la Nyanungu kwa shughuli hizo, lakini kwa mujibu wa sheria bonde hilo liko ndani ya hifadhi ya Serengeti hivyo hawapaswi kuendesha shughuli zozote za kibinadamu kwa hiyo endapo watapewa mafunzo wataweza kulima na kufuga kisasa hali itakayosababisha wahitaji eneo dogo.

Monday, December 2, 2013

Mwendesha Pikipiki afariki


MUSOMA.
Mwendesha Pikipiki maarufu kama Boda boda Ibrahim yusuph(17) mkazi wa Kamnyonge Mjini Musoma amegongana na gari uso kwa uso akiwa katika harakati za kujinasua na askari wa usalama barabarani kwa kosa la kutovaa kofia,akiwa anaivaa ambapo aliacha njia na kuifuata gari na kufa papo hapo na pikipiki kuteketea kwa moto kufuatia kulipuka kwa tanki la mafuta .

Ajali hiyo imetokea leo asubuhi majira ya saa moja, karibu na stendi kuu ya mabasi iliyoko Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma ikihusisha gari lenye namba za usajiriT816 CLS lililokuwa likitokea makutano kuelekea mjini Musoma.

David Goodluck ni shuhuda wa ajali hiyo ambaye ni dereva wa daladala iendayo Wilayani Butiama alisema ameshangazwa na baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo badala ya kutoa msaada kwa majeruhi waliokuwa katika gari hiyo na aliyepoteza maisha ,walianza kuchangamkia samaki zilizomwagika katika mfuko na kutapakaa barabara nzima.
.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ,SACP Ferdinand Mtui amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Friday, November 15, 2013

TEMBO WAFANYA MAUAJI-SERENGETI.

SERENGETI.


SERIKALI imetakiwa kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na njaa pamoja na mauaji ya watu kutokana na tembo kuvamia maeneo ya mashamba na makazi ya watu wilayani Serengeti Mkoani Mara.

Wakizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ,madiwani hao wamesema kuwa tembo wamekuwa tishio na kero kwa wananchi wa wilaya hiyo kutokana na kuvamia makazi na mashamba mara kwa mara na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi.


Wamesema kuwa wilaya ya Serengeti haina tabia ya kuomb achakula cha msaada lakini kutokana na uvamizi huo wa tembo wameiomba serikali kuleta chakula cha msaada kwa wale wasio na uwezo pamoja na cha bei nafuu haraka iwezekanavyo kutokana na watu kuanza kula maembe usiku na mchana ili kunusuru maisha yao.

Waliongeza kuwa serikali imekuwa ikiwachukulia hatua kali na a kisheria kwa wananchi wanaowaua wanyama hasa tembo na faru lakini wanyama hao wanapowadhuru wananchi serikali imekuwa ikaa kimya bila kujali wananchi walioadhiriwa na wanyama hao hasa kwa familia iliyoachwa yatima kutokana na wazazi/mzazi wao kuuawa na tembo.

Waliiomba Tanzania National Park(TANAPA) kusimamia kikamilifu familia zilizoadhirika hasa watoto yatima kwa kuwasomesha watoto na kuwasimamia maisha yao yote mpaka pale watakapo jitegemea wenyewe ili kuweza kufikia malengo yao ya baadae.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw.John Ng’oina alisema kuwa Wizara ya Maliasili na utalii inatakiwa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo na sababu kubwa hasa ya kuwafanya wanyama hao tembo kutoka maeneo ya hifadhi na kuvamia mashamba ya wananchi hadi kuua wananchi ili kuthibiti hali hiyo ambayo imeendelea kuleta hofu miongoni mwa wananchi.

“Nadhani kuna tatizo ndani ya hifadhi huenda wanyama hao wanabugudhiwa ndani ya hifadhi au chakula kimepungua na ndio maana wanyama hao wanaamua kutoka ndani ya hifadhi na kutafuta sehemu nyingine ambapo wanaweza kuishi lakini wanajikuta tayari wamevamia mashamba ya watu na kusababisha njaa”alisema Mwenyekiti huyo.

Akitoa tamko la baraza mwenyekiti huyo alisema kuwa ni vema sasa maeneo yote yanayozunguka hifadhi hiyo yakawekewa uzio ili kuthibiti hali hii kutokana na madhara makubwa ya njaa na vifo kwa watu kuendelea kutokea katika Halmashauri hiyo.

Hata hiyo waliongeza kuwa zamani tembo alikuwa haonekani katika maeneo ya makazi ya watu wakati wa mchana ilikuwa ni usiku tu lakini siku hizi hata muda wa mchana saa nane tembo anaonekana na kusababisha madhara makubwa kwa binadamu na mifugo kwani tayari ngombe watatu wamekwisha uawa na tembo.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Goody Pamba kuna haja kubwa ya madiwani kwenda katika maeneo mengine yanayozungukwa na hifadhi ya wanyama kama vile maasai Mara kujifunza namna wenzetu wanavyoishi na wanyama hao bila kuleta madhara yoyote.

Diwani wa kata ya Manchira Michael Shaweshi alisema kuwa imefikia hatu tembo anaingia hadi kwenye ghala la mtu alilohifadhia mazao ya chakula mbali na kuvamia mashambani hali inayoendelea kuleta adhari kuwa wananchi ili hali walikuwa wamelima chakula cha kutosha.

Tuesday, October 15, 2013

WANARIADHA WAMUENZI NYERERE



BUTIAMA

CHAMA cha riadha Mkoa wa Mara, Oktoba 14 mwaka huu, kilimuenzi Baba wa Taifa,Hayati Mwl.J.K Nyerere kwa kufanya mbio ya Kilometa 21 na ushindi kupatiwa zawadi.

Akizungumza mara baada ya Mashindano hayo, Kamishina wa habari na uenezi  wa Chama chama cha riadha Mkoa wa Mara, Eva-Sweet Musiba alisema kuwa Chama kimeamua kufanya mbio hiyo ili kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere katika nchi hii kwa kuleta Uhuru, uzalendo,Amani na Utulivu katika nchi hii.

“ Tumeamua kuunga mkono jitahada za Mwalimu Nyerere alizozifanya katika nchi hii, pia kuipenda michezo,hatukutaka kuwa nyuma kwa michezo ingawaje yeye alikuwa anapenda mchezo wa bao, lakiji sisi tumeamua kufanya hivyo ili kumkumbuka Baba yetu ambaye alikuwa msitari wa mbele katika michezo yote” Alisema Musiba.

Pia alitoa shukurani kwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara Barrick kwa kuchangia gharama za mashindano hayo na kuwataka wawekezaji wengine, mashirika  ya umma, watu binafsi na Serikali kuunga mkono jitihada za wawekezaji  ili kukuza mchezo huo ambao ndio pekee unalitangaza Taifa hilo kwa wachezaji kuwakilisha Taifa.

Mbio hizo zilizoanza majira ya asubuhi juzi ambapo Mkuu wa wilaya ya Butiama, Angeline Mabula alizianzisha kwa kupuliza kipenga,kutoka  viwanja vya Joseph Kizurira Nyerere kuelekea barabara ya Kiabakari na kurudi.
Mbio hizo zilishirikisha wanariadha wapatao 10 kutoka wilaya za Butiama, Musoma Mjini, Rorya na Tarime ambapo washindi  wa tano bora walipatiwa zawadi zao za fedha taslimu.


Mshindi wa Kwanza Majina yao na fedha zikiwa kwenye mabano ni Mwita Kopilo kutoka Wlaya ya Tarime aliyekimbia 1:05:23 alipewa Sh. (70,000), Mshindi wa pili Juma Issa Wambura wa Tarime aliyekimbia 1:10: 03 alipata Sh. (50,0000), Mshindi wa tatu,Mukama Magesa kutoka Wilaya ya Butiama 1:13:19 alipata Sh. (30,0000) wa nne  na wa tano ,Nyakutonya Berias wa Wilaya ya Butiama 1:20:47 na Chagembe Maira  1:22:00 walipewa Sh. 25,000 ambapo Mkuu wa Wilaya Angelina Mabula alikabidhi zawadi hizo.

Thursday, October 3, 2013

VICENT NYERERE MBUNGE WA MUSOMA ADANGANYA



MUSOMA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere,(CHADEMA) amewadanganya wanachi wa Jimbo lake kuwa Ikulu ndogo inadaiwa Sh. Bilioni 1,  za gharama za maji  huku Mamlaka ya Maji  safi na taka (MUWASA) ikikanusha vikali kauli hiyo ya Mbunge na kudai kuwa gharama hizo ndiyo bajeti ya Mamlaka yao.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mjumbe wa bodi ya Maji hivi karibuni katika Mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni katika viwanja wa Shule ya Sekondari  ya Mara alitamka kuwa  Ikulu ndogo inadaiwa Bilioni 1 ambazo gharama hizo wananchi ndio wanaozilipa.

Akikanusha kauli hiyo wakatia kizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya maji safi na taka Musoma ( MUWASA), Emmanuel Ruyobya alisema kuwa siyo kweli kwamba Ikulu ndogo inadaiwa fedha hizo.

Alisema kuwa Taasisi zinazodaiwa ni Hospitali M.40, Polisi M. 96,Shule za Msingi M.8 jeshi kwa maana ya watumishi na nyuma zo ni Sh. M1.2 na RAS Mara kwa maana ofisi pamoja na Ikulu ndogo ni Sh. M. 10 si Bilioni 1 kama ambavyo Mbunge huyo alidai.


Alisema kuwa MUWASA inaendelea na shughuli zake za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga wateja wapya kulingana na miundo mbinu iliyopo,pia imepata mkandarasi wa kuweza kujenga mradi mkubwa wa Maji  eneo la Bukanga, Makoko utakaogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 41 na utakamilika mwaka 2014.


Mradi huo utakapokamilika utatoa huduma zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa Musoma kwa kuzalisha mita za ujazo 36,000 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji ya mita za uajzo 24,000 za sasa.

Alisema kuwa kutokana na kukatatika kwa mabomba,mafundi wanafanya jitihada ili kurejesha huduma hiyoa mbapo leo baadhi ya maeneo yataanza kupata maji.


Wednesday, October 2, 2013

MJI WA MUSOMA WAKUMBWA NA UHABA WA MAJI



MUSOMA


ZIWA Victoria limekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Mji wa Musoma kutokana na tatizo la ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo ya Mji wa Musoma Mkoa wa Mara, ambapo kwa sasa ni la  takribani siku tano.

Uchunguzi uliofanywa na blog hii, umebaini kuwa wakazi wa maeneo ya kando kando ya ziwa hasa, Baruti, Bweri na Iringo wamekuwa wakichota maji katika ziwa hilo kutokana na kukosa maji ya bomba katika maeneo wanayoishi huku njia mbalimbali za boda boda na baiskeli na vichwa vya  akina mama wakibeba maji hayo kutoka ziwa hilo.

Wakizungumzia suala hilo kwa nyakati tofauti, Mkazi wa Bweri, Gabriel Kambuga Mkazi wa Kata ya Bweri, alisema kuwa kwa sasa wana takribani wiki moja hawajapata huduma hiyo na hivyo kuwalazimu kwenda kuchota ziwani ambapo maji hayo hayana usalama.

Naye mkazi wa Kigera, Edward Patrick aliyefika katika ofisi za Muwasa kutaka kujua   huduma hiyo itarejea lini,alisema kuwa eneo hilo halijapata maji kwa muda wa wiki moja,lakini tatizo lao halihusiani na kutatika kwa bomba Mtaa wa  Nyerere.

Afisa Mahusiano wa Mamlaka ya  Maji safi na Taka Mjini Musoma(MUWASA), Emmanuel Ruyobya  amesema kuwa tatizo hilo limetokana na upanuzi wa barabara ambapo Kampuni ya Kichina imekata mabomba ambayo yanasafirisha maji kwenda kwa wakazi sehemu mbalimbali za mji huo.

“Mabomba yaliyopo yamechakaa sana, na yana miaka kama 50 hivi, sasa yanapokuwa yanahamishwa ili kupisha ujenzi wa barabara yanakatika, hilo ndo tatizo kubwa lililosabisha wakazi hawa kukosa maji,jitihada zinafanywa ili kurejesha huduma hiyo haraka” Alisema Ruyobya

Maeneo ambayo hayana  Maji ni Iringo, Nyamatare, Mkendo kati, Kigera, Kwangwa, Nyakato, Nyasho, kitaji,Bweri na Kiara.

Sunday, September 29, 2013

PROF MBARAWA NA MKONGO WA TAIFA





MUSOMA.

WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara, kutunza Mkongo wa Taifa kwani una manufaa makubwa kwa uchumi wa Taifa hili.

Ilikuwa ni siku ya kukamilisha ziara yake ya siku moj akatika Mkoa wa Mara,Wilayani Tarime mji wa  Sirari mara baada ya kumaliza kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mkongo huo na changamoto zinazoukabili.

Alisema Mkongo wa Taifa una manufaa makubwa kwa uchumi wa Taifa hili kwa kuwapatia  mawasiliano wananchi wake, ambapo Mikoa ya Tanga na Arusha ina watumiaji wengi na  Mkoa wa Mara bado haujawa na watumiaji wengi, ambapo pia kuna changamoto mbalimbali zinazoukabili ikiwa ni pamoja na maporoko upande wa  Arusha ambapo udongo umekuwa ukiingia kwenye miundo mbinu ya Mkongo huo.

Aliwahadharisha wananchi kuwa nyaya za Mkongo huo zina madhara makubwa kwa kuwa zimetengezwa kwa kioo maalumu, hivyo unaweza kuharibu Mkongo huo, huku ukiambulia upofu, kwani nyaya zake ni hatari sana ziiingiapo kwenye jicho.

“Ni kosa kubwa kuhujumu miundo mbinu, wananchi waelewe kuwa miundo mbinu hii ni kwa ajili ya manufaa yao na Taifa kwa ujumla,pia hakuna shaba katika mkongo huu, ambayo  wahujumu wanafikiri kuwa ipo, ila nyaya zake ni nyuzi laini kama unywele  ambapo waya huo ni hatari sana kwani unaweze kukutia upofu” Alisema Mbarawa.

Akizungumza na wafanyakazi  wa Kammpuni ya Simu ya Tanzania ( TTCL), Mkoa wa Mara na Posta, katika ofisi zake zilizopo mkabala na uwanja wa Michezo wa Karume, alisema kuwa wafanyazi hao  wana thamana kubwa ya kuutunza  kwani ndio waliokabidhiwa jukumu hilo.

“TTCL yaani nyie mmepewa jukumu la kuuendeleza mkongo kwa maana ya kuusambaza nchi nzima kwa niaba ya Serikali ili kuleta ubora wa huduma kwa gharama nafuu, usalama wa nchi, watu na mali zao” Alisema Mbarawa.
Alisema kuwa Serikali inataka kufanya ubia  kati ya Bat Airtel ya India na TTCL ambapo Bat Airtel yuko tayari kuachia hisa zote kwa Kampuni ya TTCL na kwamba kwa sasa kila kampuni iko kwenye mchakato wa kutathimini hisa zake na kwamba tayari Bat Airtel wamekamilisha.

Kwa upande wa Shirika la Posta nchini aliwataka wafanyakazi kuwa wabunufu kwani teknolojia zinabadilika na kwamba Wizara itaaendelea kushirikina na  Shirika hilo hili liweze kukua kwani lisiposaidiwea linaweza kupotea.

Alizitaka taasisi zote za Serikali kutumia huduma ya  shirika hili kwa kutuma vifurushi vyote kwa njia ya posta kwani kuna baadhi ya Taasisi za Serikali zimeacha kutumia Shirika hilo, na hivyo kusababisha kukosa mapato.

Kuhusu nyongeza ya Mishahara ambayo watumishi wa Posta walimlilia Waziri aliwataka kutuma maombi yao kwa bodi, ambayo ndiyo yenye thamana ya kufikia maombi yao hazina na hazina ikashughulikia hivyo ana imani kuwa nyonyeza ya mshahara inawezekana kwani  Serikali yao ni sikivu.


Thursday, May 2, 2013

GAZETI LA MFANYAKAZI LAREJEA ULINGONI TENA.



Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizindua rasmi Gazeti la Mfanyakazi wakati wa kilele cha Sherehe ya Sikukuu ya Wafanyakazi,Mei mosi zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa michezo wa Sokoine mkoani Mbeya.kushoto ni Kaimu Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Bi.Nortiburga Maskini na kulia ni Katibu mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Ndugu Nicholaus Mgaya (picha na Freddy Maro) 

Saturday, March 16, 2013

WANANCHI WANAOZUNGUKA MGODI WA NORTH MARA KUPEWA FIDIA


TARIME.

KUFUATIA kuundwa kwa kikosi kazi (Task Force) kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchunguza uthamini fidia ya wakazi wanaozunguka mgodi wa Dhahabu wa North Mara,wananchi hao sasa watapatiwa ufumbuzi wa tatizo hilo.

Hayo yamesema na Afisa Mthamini Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mwenyekiti wa Kikosi kazi hicho, Adam Yusuf alipokuwa akijibu hoja ya Diwani wa kata ya Mbogi,Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara  Sylivester Nyankomo,katika kikao cha Baraza la Madiwani, kuhusu fidia utatuzi wa mgogoro wa Mgodi na wananchi wanaozungumka katika eneo hilo.


Katika hatua nyingine Diwani huyo pia alikishtumu Kikosi kazi hicho kwa kutoa taarifa isiyo na sahihi wala uthibitisho kutoka kwa mwekezaji,jambo ambalo lilizua mgogoro katika kikao hicho na madiwani kuitaka taarifa hiyo iandikwe na kuwekewe sahihi ndipo ijadiliwe.



Akisoma taarifa hiyo mbele ya baraza la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Tarime,katika kikao cha dharula cha kupokea taarifa ya  vikao kati ya kikosi kazi cha kushughulikia masuala ya uthamini na fidia, Katibu wa kikosi kazi, Jeremiah  Minja alisema kuwa ni lengo la Serikali kuona kuwa matatizo yaliyojitokeza katika mgodi wa Noth Mara yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu na kumwezesha mwekezaji kuendelea na shughuli zake kama kawaida huku haki stahili za wananachi wa ardhi wanaozunguka mgdo huo zikizingatiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Aidha ni azam ya Serikali ni  kuona kuwa amani na Utulivu na mahusiano mema kati ya Mgodi na wananchi wanaozunguka Mgodi huo vinadumishwa na ndiyo maana ikaazimia kiudwe kikosi kazi kitakachojumisha wataalamu na maafisa kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali kusimamia utatuzi wa matatizo hayo.

Alisema kuwa matatizo yaliyojitokeza katika maeneo ya vijiji vinavyozunguka mgodi ni pamoja na wanachi ambao maeneo yao yalifanyiwa uthamini lakini bado hawako tayari kuchukua malipo yao,waliofanyiwa uthamini lakini hawako tayari kuondoka,waliopokea sehemu ya malipo nab ado wako katika maeneo yaliyofanyiwa uthamini,waliofanyiwa uthamini wakachukua malipo yao yote na kuwaendelea kukaa na kuendeleza maeneo ambayo yalifanyiwa uthamini ambapo kuna wengine hawako tayari kuona maeneo yao yakifanyiwa uthamini.


Wiki iliyopita katika kikao cha Baraza la Madiwani  wakati wa kutambulisha kikosi kazi hicho, Baraza liliagiza kikosi hicho kwenda katika vijiji vya Kewanja, Nyangoto na Nyakunguru na Baraza lipewe matokeo ya vikao hivyo kabla ya zoezi rasmi la uthamini na uhakika kuanza katika maeneo husika.
Alisema kuwa baada ya kikao cha halamshauri ya Kijiji cha Kewanja kulitolewa hoja na kujdiliwaambapo iliagizwa Uthamini ufanyike ndani ya wiki mbili,ambapo kikosi hicho kilifanya kazi hiyo kama kilivyoagizwa lakini dosari iijitokeza katika kijiji cha Nyangoto ambao hawakuwa tayari kuzungumza wala  kushirikia katika zoezi hilo hadi hapo Mgodi utakapotoa kesi yao Mahakamani na ndipo kipagwe kikao kingine na uongozi wa mgodi uwepo ili kuzungumza nao.


Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Amos Sagara aliiomba Wizara ya Nishati na Madini ,Baraza la Mazingira (NEMC), wao pia waunde kikosi kazi kingine kwa ajili ya kuchunguza matatizo yanayowakabili wakazi wanaozunguka mgodi huo kwani maisha yao yako hatarini kwa kuwa maji machafu  ya kusafishia dhahabu yanaathiri afya ya watanzania hao ambao hawana hatia.

Aidha alikiomba kikosi kazi hicho kuzunguka kwa vijiji vyote vinavyozunguka Mgodi huo ili kujua matatizo yao ingawaje nayo yanafafa na ya vijiji hivyo, vijiji ambavyo ‘Task Force’ imetakiwa kwenda na kurudisha  mrejesho ni pamoja na Kerende, Nyamwaga, Matongo,  na Genkuru.


Akizungumza katika Kikao  hicho, Meneja wa Mgodi huo,Champman Gerry alitoa shukrani kwa Serikali kuunda timu hiyo ili kuja kutatua matatizo  kwamba amesikia akilalamikiwa  kuwa walikuwa hawalipwi fidia kwa mujibu wa sheria,na kwamba atazingatia utaratibu atakaopewa na kwamba ataufuata   ili kuondoa kabisa matatizo yaliyopo baina yao na wananchi.



Tuesday, March 12, 2013

MKUU WA WILAYA YA BUTIAMA NA USALAMA

BUTIAMA MARA,



 Mkuu wa Wilaya ya Butiama,Angeline Mabula  amesema kuwa hali ya Ulinzi na Usalama katika Wilaya hiyo imeimarika tofauti na hapo awali ambapo ilikubwa na matukio ya mauaji ya kutisha.

Alikuwa akizungumza na Waandishi  kutoka vyombo mbalimbali vya  habari vya Radio, Magazeti na Luninga juu ya mafaniko ya awamu ya nne katika Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kipindi cha mwaka 2005-2012


Kwa siku za hivi karibuni, Wilaya ilikumbwa na wimbi la mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina, Serikali imechukua kila tahadhari kuhakikisha kwamba mauaji hayatokei tena,elimu imeendelea kutolewa, ili kuhimiza ulinzi shirikishi ambao utakuwa suluhisho la tatizo la mauaji”Alisema Mabula. 

Alisema kuwa historia inaonyesha kwamba, mbali na mauaji yatokanayo na ugomvi wa koo, wizi wa mifugo na ugomvi/migogoro ya ardhi mauaji ya sasa ya kuchinja watu hayakuwahi kutokea, yameibuka tu kwa udanganyifu  wa watu kutaka kujipatia utajiri wa haraka haraka.

Serikali inafanya kila linalowezekana kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahalifu wa aina zote, kwa kuwafichua na kuwafikisha mbele ya vyombo vya dola ili kulinda raia wake na mali zao. 
Aidha Wilaya ina vituo 10 vya polisi Buhemba, Bisumwa, Bukima, Suguti, Kiagata, Kyabakari, Kigera etuma, Butiama, Saragana na Tegeruka.

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua katika kuwahimiza na kuwaelewesha wananchi kuwa ulinzi wao na mali zao uko mikononi mwa wananchi wenyewe wakishirikiana na Polisi, dhana ya Polisi jamii na ulinzi shirikishi inaendelea kuhimizwa.


Wilaya imeweka mpango madhubuti wa  kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana au wanamgambo waliokwishapitia mafunzo ili kuimarisha ulinzi na Usalama katika maeneo yao na kuwatahadharisha kutojichukulia sheria mikononi.


Amewataka vijana na akinamama kuunda vikundi ili wapewe vitendea kazi ambavyo vitawasaidia katika kazi zao za ujasiliamali na kwamba jumla ya Sh. Milioni 90 zimetegwa kwa aili ya kuwawezesha vijana na akina mama ,ambapo kati ya hizo Milioni 45 ni za Vijana na Milioni 45 ni za vikundi vya akina mama ambapo watapewa vitendea kazi watakapokuwa wamejisajili.


Aidha vikundi 4 vya wajasiliamali vilipewa mikopo yenye thamani ya Sh. 180,000,000 kutoka mfuko wa wajasiliamali unaofadhiliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Vikundi vilivyopewa fedha ni Mwangaza SACCOS Buhemba Tshs. 80,000,000, Imani Bwai (Kiriba) Shs. 31,000,000 na Mwamucha SACCOS (Mugango) Tshs. 30,000,000




Katika kipindi cha miezi sita halmashauri imeweza kusimamia vizuri fedha zilizopatikana katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kugharamia matumizi ya mishahara, matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo.  Pia Ruzuku ya Serikali imeongezeka kutoka Sh.571,556,000 mwaka 2005 hadi Sh.975,426,302  mwaka 2012 sawa na 59%.