Thursday, December 29, 2011

MAFUTA YAWA KERO.

MUSOMA.

Hali ya Nishati ya Mafuta ya Petroli na mafuta ya taa imezidi kuwa mbaya katika Manispaa ya Musoma, Mkoani Mara ambapo katika visima vyot vya mjini hapo kufungwa kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo muhimu.

Bei ya mafuta kwa sasa mjini hapo yanauzwa kati ya sh.7,000 hadi sh. 10,000 kwa lita moja kutoka kwa walanguzi wa mitaani huku mafuta ya taa kuadimika kabisa hali iliyomlazimu mbunge wa jimbo hilo, Vicent Nyerere (CHADEMA) kufanya ziara na kuona hali halisi ya ukosefu wa bidhaa hiyo ya mafuta.

Baadhi ya vituo ambavyo alitembelea na kukutana na uongozi wa vituo walisema kuwa mafuta yamewaishia tangu siku ya jumatano na wengine siku ya alhamisi na kudai kuwa bidhaa hiyo itapatikiana kuanzia jumanne mwaka ujao wa 2012 kutokana na ukosefu katika maghala wanayochukulia.

Meneja wa kituo cha kampuni ya White Said Fundikira alisema kuwa wao huagiza mafuta jijini Mwanza katika kituo cha GAPCO na kudai kuwa wamew3asiliana kwa njia ya simu na kuambiwa kuwa anaweza kupata mafuta siku ya jumanne au jumatano mwakani.

“Najitahidi tuone tunanusuru upungufu huu lakini jitihada zinagonga mwamba kwani tumeshaambiwa hadi mwakani na hakuna jinsi tunasubiria hadi watakapotuletea na akiba yetu imeisha jana (juzi),”alisema Fundikira.

Naye mkurugenzi wa kituo cha Kiraba Kampani Shamsa Kiraba alimeioma EWURA kujipanga na kujidhatiti ili kuona hali haiwi mbaya nchini kutokana na ukosefu huu ambao unaendelea sehemu mbalimbali nchini na kusababisha kushuka kwa uchumi wa nchi na maisha kupanda.

“EWURA ijipange vizuri na kuona ni jinsi gani wanaweza kutatua tatizo hilo kubwa la uhaba wa mafuta nchini lakini ingiwa kuna tuhuma nyingi zinaelekezwa kwetu sisi wauzaji naweza kusema katika kituo chetu sisi hata kama bei wa bidhaa tumenunua kwa bei ya juu na siku ya pili bei inashuka hatujali tunauza kwa bei hiyo mpya elekezi na sio kuficha mafuta,” Kiraba.

Pia ziara hiyo ya mbunge ilifika hadi kwa baadhi ya watumiaji wakubwa wa bidhaa hiyo waendesha pikipiki maarufu bodaboda katika kituo cha Nyasho ambapo hawakusita kueleza hasira zao na kupaza sauti kwa wauzaji wa mafuta mjini hapo kilichosababisha pikipiki kubakia tatu badala ya 27.

Mmoja wa dereva wa bodaboda Bakari Bega alisema kuwa wanapata usumbufu mkubwa kutoka kwa wauzaji hao kwani wanatumia mwanya huo wa upungufu wa mafuta kuuza kwa bei ya juu hasa kuwapa kuwapa walanguzi na kuuza kwa bei ya juu.

“Hapa kwanza kazi hakuna hata pesa imeshakosekana kwetu pamoja na hilo tunaomba serikali ya Manispaa ya Musoma ikakague baadhi ya vituo vya mafuta watakuta kuna mafuta yapo ila ndio hivyo wanataka kupata faida kubwa kwani jioni wanafungua kwa wizi na kuuza bei ya s. 3,000 kwa lita,”alisema Bega.

Madereva hao hawakusita kutaja kituo kimojawapo ambacho kinauza mafuta kwa siri kinachojulikana kwa jina la Petrolux kinachomilikiwa na Zembwela ambapo mbunge Nyerere hakusita kwenda kujionea ambapo msemaji wa kituo hicho Justine Dida alikanusha ingawa alionekana kujikanyaga kwa kusema kuwa kituo hicho kiliishiwa mafuta tangu siku ya jumatano saa 9 jioni wiki hii huku mmoja wa wateja wake alipouliza alisema kuwa mafuta yameisha jana asubuhi.

“Huo ni uongo hatuna mafuta je? Wewe mwandishi unajua mafuta ya petrol twende nikakuoneshe kama utayaona maana naona mnanilazimisha kuwa yapo mimi nimesema hakuna mafuta hakuna jingine,”alisema kwa jaziba baada ya kuona amebanwa kwa maswali.

Wakati huo huo wakati tupo katika kituo hicho dereva wa gari lenye namba T 726 BMT, Christopher Paulo alikutwa akiweka mafuta katika gari lake ambayo yalikuwa yamehidhadhiwa kwenye dumu na alipoulizwa alisema kuwa mafuta hayo ameyatoa Buhemba Musoma Vijijini ambako alinunua kwa sh. 3,000 kwa lita.

Nao madereva wa Bajaji walisema kuwa hali kwao ni ngumu kwani katika kituo chao kuna jumla ya bajaji 25 lakini kwa sasa kuna bajaji nne tu ndizo zinazofanya kazi kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo ya mafuta.

“Hapa kuna jumla ya bajaji 25 lakini kwa sasa kuna bajaji nne tu zinazofanya kazi kwa maana hiyo maisha yameshaanza kuwa magumu kutokana na kukosekana kwa mafuta ya petroli kwa hivyo hata bei ya kusafirisha mizigo imepanda nayo kwa kilometa 8 tunatoza kati ya sh. 20,000 hadi 25,000 hali inayofanya kugombana na wateja wetu,”alisema Lazaro Kumburu mmoja wa madereva wa bajaji.

Baada ya ziara hiyo Mbunge Nyerere alisema kuwa EWURA inabidi itoe tamko kama bei ya mafuta imepanda kabla ya mwakani kwani tetesi nyingi zinasema kuwa bei ya mafuta itapanda kwa kiwango Fulani hivyo kwa hali hii wananchi wetu watapata shida kwa kipindi hiki chote.

“EWURA inabidi itoe tamko haraka iwezekanavyo kunusuru hali mbaya ya mji wetu kwani hata usafiri wa watu wa chini wanaotumia pikipiki utakuwa wa taabu sana na watalipa nauli kubwa hivyo tamko lao ndio ukombozi wa wana Musoma,”alisema Nyerere.

Gazeti hili wiki iliyopita iliandika habari ya ukosefu wa nishati hiyo kuanzia siku ya mkesha wa Krismasi ambapowakazi wa mji huo wamelazimikakusheherekea sikukuu ya Krismasi huku mji huo ukighubikwa na uhabamkubwa wa nishati ya mafuta ya Petroli ambayo imesababisha kupanda beina kuuzwa kwa walanguzi tu.

Wiki hiyo bei ya mafuta ilipanda kutoka sh. 2,199 bei halali iliyopangwa na EWURA hadi sh. 5,000 kwa lita lakini kwa wiki hii imepanda na kuuzwa kati ya sh. 7,000 hadi 10,000 kutokana kuadimika kwa nishati hiyo hali iliyiosababisha hadi bei yausafiri wa pikipiki maarufu bodaboda kupanda 2,000 kwa masafa ya mjini na nje ya mji kufikia hadi 5,000.


Thursday, December 1, 2011

MAAMBUKIZI YA UKIMWI MKOA WA MARA YAKO JUU

MUSOMA.

MKOA wa Mara unaongoza katika maambukizi mapya kwa asilimia 4.2 kwa mwaka 2007/2008 kutoka asilimia 3.5 mwaka 2003/ 2004.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa kwa niaba yake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Godfey Ngatuni katika siku ya maadhimisho ya Ukimwi Duniani kimkoa yalifanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Kamunyonge Manispaa ya Musoma.



Amesema kuwa kutokana na utafiti wa kisayansi uliofanyika mwaka 2007/ 2008 maambukizi kitaifa yamepungua kidogo kutoka asilimia 7 mwaka 2003/ 2004 hadi asilimia 5.7 wanawake wakiwa na asilimia 6.6 na wanaume wakiwa na asilimia 4.6.



Aidha amesikitishwa na ongezeko la maambukizi mapya kwa Mkoa wa Mara na kwamba ni jambo la aibu ambapo Mkoa uliokuwa ukiongoza wa Iringa, Wilaya ya Makete umeweza kupungua kutoka asilimia 2.3.
Amewataka viongozi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mara, kushirikiana pamoja na taasisi kufanya jitihada za kuwez kutokomeza ugojwa huo kama Mikoa mingine walivyoweza kujikinga.



Awali kabla ya kutoa hotuba yake, Mkuu wa Mkoa walipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali ambayo yanafanya shughuli za kuelimisha jamii juu ya Ukimwi ni janga la Kitaifa na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na watu wanoishi na VVU, ambapo wawili walitoa ushuhuda wa jinsi wanavyoishi na VVU na kuwapa moyo waliombukizwa kutokata tamaa.


Tangu maadhimisho hayo yameanza Novemba 29- Disemba 1 mwaka huu jumla ya wakazi wa Musoma wapatao 784 wamejitokeza kupima ambapo kati ya hao walioathirika walikuwa 14. Wanawake SABA na wanaume SABA.


Kauli mbiu ya siku ya Ukimwi Duniani Kitaifa ni Tanzania bila ya maambukizi mapya, Unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi inawekana, ambapo kauli mbiu ya Mkoa ni Mara bila ya maambukizi mapya inawezekana.


Siku ya Ukimwi Duniani Kitaifa imefanyika Mkoa wa Shinyanga.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Shirika ya Aids Relief Dk. Protace Ndayanga amesema ni wajibu wa kila mmoja kutofanya unyanyapaa kwa mtu mwenye virusi vya ukimwi na badala yake wananchi wasaidie kutoa huduma na kushiriana nao kwa pamoja kwa kuwaptia tiba na chakula bora.

Amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali bado maambukizi yamekuwa hali inayoweza kuwavunja moyo watoa huduma ili kutokomeza ama kupunguza ugojwa huu.
Ameongeza kuwa Shirika lake linafanya kampeni ya kila Wilaya ya kutoa elimu kupitia vyombo vya habari.

Wednesday, November 30, 2011

AFISA UVUVI MKOA WA MARA LAWAMANI

MUSOMA


WADAU wa mazingira katika Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara wameilalamikia sekta ya uvuvi Mkoani MARA kwa kutokuwa makini katika ufuatiliaji wa vitendo vya uvuvi haramu vinavyofanyika ndani ya ziwa Victoria ambavyo vinasababisha uharibifu wa mazingira,

Hayo wamesema Novemba 29 katika siku ya maadhimisho ya siku ya Ziwa Victoria yaliyofanyika katika ukumbi wa uwekezaji Mkoani Mara ulioko katika Manispaa ya Mji wa Musoma, ambapo walitaka kujua kulikoni zana haramu zinazidi kutumika na kupelekea Samaki wanaovuliwa ndani ya ziwa victioria kutokuwa na kiwango cha kimataifa wakati wanadai kuwa samaki wanaovuliwa wana kiwango cha Kimataifa.

Walisema hata kama wanawapatia semina juu ya utunzaji wa mazingira ya ziwa Victoria lakini iwapo hawatakuwa wafuatiliaji itabakia kuwa maneno ya karatasi tu kwa kuwa mara kwa mara wamekuwa wakitoa semina kama hizo lakini ufuatiliaji wake kwa vitendo umekuwa ni mdogo .

Walimtaka Afisa Uvuvi Mkoa Mara awaeleze kwa nini zana haramu kama makokoro ya kuvulia samaki wachanga,dawa za sumu wanazotumia wavuvi kuvulia samaki bado zinazidi kuongezeka ndani ya ziwa, sehemu madawa hayo yanapouzwa wanapafahamu na hata nyumba wanazohifadhia zana hizo wanazifahamu wakati polisi na BMU wapo kila koma na kazi yao ni nini, huku baadhi yao wakimtuhumu kushirikiana na wavuvi haramu.

Akijibu maswali yaliyoulizwa na wadau hao Afisa Uvuvi Mkoani Mara Apolinary Kyoja alionekana kutokuwa na majibu sahihi ya moja kwa moja ya kuwaeleza wadau hao kulingana na maswali yaliyoulizwa badala yake aliwaomba ushirikiano katika kutoa taarifa.

Kyoja amewataka wadau hao kumsaidia kupambana na wavuvi haramu kwa maana kuwa yeye peke yake hawezi kufuatilia kila mahala kwani hana vyenzo za kutosha za kufuatilia kila sehemu kwa kuwa kila mtu ni mlinzi wa ziwa Victoria.

Amesema kila mtu anatakiwa awe mlinzi wa ziwa hilo kwani hata yeye anao uwezo wa kuzunguka kila mahala kukagua usafi wa ziwa ila anachokiomba kutoka kwa wananchi ni kusaidiana nae ili kutokomeza tatizo la uchafuzi wa ziwa hasa kwa kupashana taarifa pale wananchi wanapoona wavuvi haramu wakitumia zana haramu za uvuvi.

Akizindua semina iliyoendana na maadhimisho hayo ya siku ya ziwa Victoria Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara ,NDUGU GEOGFEY NGATUNI amesema kuwa wananchi wanatakiwa kutunza mazingira hususani ya ziwa Victoria kwa kuwa maji hayo ndiyo yanayotumika katika shughuli mbalimbali viwandani na kwa matumizi ya majumbani.

Amesema wavuvi wanapoendelea kutumia zana hizo haramu wanasababisha madhara mengi kwa afya ya binadamu na kwa mazingira hali inayoadhili uchumi wa Taiafa letu.

Kauli mbiu ya ziwa Victoria ni Ziwa Victoria ni uhai wetu,mali yetu tuilinde.

ZIWA VIKTORIA LACHANGIA KIPATO KIKUBWA SERIKALINI.

MUSOMA.

ZIWA Victoria linachangia pato la Taifa kwa takribani Dola za kimarekani Bilioni 3 hadi Bilioni 4 kwa Mwaka.

Hayo yamesema Novemba 29 na Katibu Tawala wa Mkoa, Clement lujaji katika kilele cha maadhimisho ya siku ya ziwa Viktoria kitaifa iliyofanyika katika Mkoa wa Mara, Manispaa ya Musoma , iliyofanyika katika Bwalo la Polisi, Mwisenge.

Alisema kuwa ziwa Viktoria ni raslimali muhimu katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na lina hazina kubwa zaidi ya samaki wa maji baridi Duniani.

Aliongeza kuwa samaki wanovunwa kwa mwaka ni kati ya tani 400,000 hadi 500,00o kwa mwaka, sambamba na hilo pia ziwa hilo ni kivutio cha utalii na chanzo cha mto Nile ambao una maporomoko ya Owen, Jinja-Uganda yanayotumika kuzalisha umeme unaosambazwa katika nchi za Uganda, Kenya, Tanzania na Rwanda.

Aidha madhumuni ya maadhimisho hayo ni kuwapa fursa wananchi na wadau wa Bonde la Ziwa Vikroria kukutana ba kuonesha shughuli mbalimbali za kuendeleza bonde hilo na mafanikio yake pia kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na kutafakari mbinu mpya za kutimiza azma ya kukuza uchumi wa eneo la nchi wanachama.

Hata hivyo pamoja na nia nzuri ya serikali kukutananisha wadau hao, wengi wa wadau hao hawakuweza kushiriki kikamilifu katika kilele hiki, zikiwemo nchi zinazonufaika na Ziwa hilo.

Alisema kuwa changamoto zinazolikabili ziwa ni pamoja na kuwepo kwa gugu maji, kuongezeka kwa vitendo vu auvuvi haramu wa kutumia baruti na mabomu, uharibifu wa uchafuzi wa vyanzo vya maji na kwamba takwimu zinaonyesha kuangamia kwa ziwa hivyo basi hamna budi kuchukua hatua za makusudi ili kunusuru ziwa hilo.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuhifandhi Ziwa Viktoria ni pamoja na kubni na kutekeleza Mradi wa kuhifadhi na kutunza Mazingira ya ukanda wa Bone la Ziwa Viktoria pamoja na ziwa lenyewe liwe sakama na kitovu cha uhai na maendeleo endelevu ya wananchi wa eneo lote la ziwa na viumbe wengine wanaoishi katika ukanda.

Serikali imeweka sheria mbalimbali zinazolenga kutunza mazingira zikiwemo sheria ya mazingira Namba 20 ya Mwaka 2004.

Aidha Mwaka 2009,Serikali ilipitisha Sheria Namba 11 ya Rasilimali za maji na Sheria Na.12 ya huduma za maji safi na Usafi wa Mazingira ambazo zinalenga kulinda na kutunza vyanzo vya maji.

Kifungu cha 52(1) cha Sheria Na.12 ya huduma za Maji na usafi wa mazingira zinatoa adhabu ya faini ya kiwango cha Sh. Milioni 1 au kifungo cha kwenda jela miezi 12 au vyote viwili kwa pamoja kwa mtua yeyote atakayesababisha uchafuzi wa chanzo cha maji.

Awali akisoma hotuba yake kwa mgeni rasmi, Afisa Maji Bonde la Ziwa Viktoria

( LVBWO) ,ofisi ndogo ya Musoma, Jumanne Sudi alitanabaisha kazi zinazofanywa na ofisi hiyo kuwa ni pamoja na kutoa hati ya haki ya kutumia maji,kushughulikia maombi na kutoa vibali vya kutiririsha vya majitaka kwenye ziwa na mito baada ya kuridhika na viwango vya maji hayo kulingana na viwango vilivyowekwa, kukusanya na kutunza takwimu za maji kutoka kwenye miti, ziwa na maji chini ya ardhi kwa ajili ya kuratibui matumizi endelevu.

Friday, November 18, 2011

WATUMISHI WABOVU KUPOTEZA KAZI.

MUSOMA.

MKUU wa Mkoa wa Mara,John Tuppa, amewataka watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Musoma kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa ndicho chama kilichoshinda katika uchaguzi Mkuu na kinachotakiwa kutekeleza Ilani yake huku akiwakemea watendaji wabovu na ambao hawawajibiki katika kazi zao.

Aliyasema hapo jana alipokutana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma katika ziara yake ya kwanza katika ukumbi wa Halmashauri uliopo katika Manispaa ya Musoma,tangu ateuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Alisema CCM ilishinda na Ilani yake ndiyo inayoongoza na ndiyo yenye kutekelezwa hivyo amewataka kuitekeleza na kuhakikisha watumishi wao wanafanya kazi pasipo kuingiza siasa kwani muda wake umepita na sasa utekelezaji, na kwamba siasa wawaachie wanasiasa wenyewe wakiwa majukwaani.

“Nimekuja leo kunitambulisha kwenu,tufahamiane uso kwa uso kabla sijaanza ziara ya kukutana na watendaji kwani nikachokiomba kwenu ni ushirikiano kwani nyie watumishi mnaoshughulika na wananchi ili mtatue kero zao” Alisema Tuppa.

Alisema kama watumishi wa halmashauri hawatatui kero za wananchi wanachi nao wataichukia serikali yao. “Kila mtu atimize wajibu wake mimi sitaki majungu, sitaki kuona mtu anakuja kwani anipatia majungu majungu kuwa mtu fulani hafai, nitakachofautailia ni ni vitendo vyenu,kama mnafanya kazi, na ukinidhibitishiea kuwa haufai nitaanza na wewe” Alisisitiza.

Aidha aliwataka kuhakikisha kuwa mipango ya halmashauri inakwenda sawa na kupata matokeo chanya na kuwataka kuepuka na hali ya kuwa na hati yenye mashaka kwani Waziri Mkuu ametoa agizo endapo hati itaendelea kuwa ya mashaka atawajibishwa Mkuu wa Mkoa.

“Waziri Mkuu kaniagiza niafatilie vinginevyo ataniwajibisha, kwani mmepata hati ya mashaka, kabla sijaanguka kwenye sementi, naweka godoro, Matatizo yetu tuyatatue wenyewe si kufuatana fuatana kwami kil amtu anajua kilichomleta ni kufanya kazi na ameisomea kazi hiyo, nikikwambia ufanye moja, mbili ,tatu, fanya na kama hukufanya nitakushumshughulikia mtumishi huyo” Alisema Mkuu wa Mkoa.

Akisoma taarifa ya Wilaya kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dk. Karaine Kunei alisema Wilaya hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na chakula chake kikuu aina ya muhogo kukumbwa na ugonjwa wa batobato.

Akizungumzia juu elimu ya elimu ya sekondari alisema jumla ya watoto 376 wa shule mbalimbali za sekondari walipata ujauzito na hivyo kushindwa kuendelea na elimu na kwamba hali ya maambukizi ya vvu katika halmashauri hiyo iko juu kwa asilimia 6.4.


Wilaya ya Musoma ina jumla ya shule za sekondari 42 sita kati ya hizo zikiwa za taasisi mbalimbali na ina kata 43 na vijiji 116.


Mkuu wa Mkoa wa Mara alianza ziara yake ya kikazi juzi ambapo alikutana na viongozi wa vyama vya siasa na kufanya mazungumzo nao, ataendelea na ziara yake katika Wilaya za Bunda, Rorya, Tarime na Serengeti.

Monday, November 14, 2011

HABARI MOTO MOTO KUTOKA WILAYA YA WAJANJA

AGIZO LA WAZIRI TAMISEMI LAKIUKWA

RORYA.

BARAZA la Madiwani Wilaya ya Rorya kwa pamoja limetoa pendekezo la kufanya marekebisho ya haraka katika ujenzi wa wodi la Wazazi lililoko Changuge, kutokana na vyoo vyake kujengwa nje ya wodi hilo,na wajawazito kukosa huduma,kufuatia agizo la Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri alipofanya ziara katika Wilaya hiyo.

Walisema kutokana na kuchelewa kwa uvunjwaji wa ukuta na kutengeneza vyoo upya kwa agizo la Naibu Waziri, Mkandarasi huyo hana budi kuharakisha ujenzi huo kwa kuwa wanawake kwa sasa wanapata taabu ya sehemu ya kujifungua na huku wodi likiwa halina choo na ucheleweshwaji wa Ujenzi upya.

Mkandarasi wa ujenzi huo, Mhini Construction wa Wilaya ya Tarime alipaswa kukabidhi jengo hilo mapema juni 15 mwaka huu,ambapo mradi wa ujenzi wa wodi hiyo ulianza Juni 9 2010.

Fedha ambayo ilikuwa tayari imelipwa ni kiasi cha Sh. M. 35,470,0720,Ambapo gharama kuu ya mradi hadi ungekamilika ilikuwa kiasi cha Sh. Milioni 40.

Lengo la Mradi wa ujenzi wa wodi ya wazazi Changuge ilikuwa kulaza wajawazito walio na uchungu, kujifungua na kutunza watoto ambao wanazaliwa kabla ya muda wao wa kuwaruhusu wazazi kwenda nyumbani wakiwa salama na lingehudumia watu 36 kwa siku endapo lingekamilika.

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri, alipofanya ziara yake katika Wilaya hiyo Mei 24 mwaka huu alikataa kufungua wodi hiyo kutokana na kutokidhi viwango ikiwa ni pamoja na vyoo vya wodi hiyo kujegwa nje ya wodi na Milango ya wodi hiyo ikiwa na mbao zisizokidhi viwango, na kutoa agizo kwa mkandarasi wa ujenzi huo kutwalipwa fedha zilizobaki na kuhakikisha linafanyiwa marekebisho ya haraka, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.



NYAVU ZACHOMWA MOTO.

JUMLA ya nyavu 45 na samaki wachanga aina sangara zenye thamani ya Sh Milioni 4,522,000 zimeteketezwa kwa moto katika oparesheni iliyofanyika katika Wilaya ya Rorya mwezi Agosti na Septemba mwaka huu.

Mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wilaya ya Rorya, Cosmas Ngangaji kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichokaa hivi karibuni imebainisha kuwa kitengo cha uvuvi,katika doria za ulinzi wa Rasilimali ya uvuvi ilifanyika oparesheni hiyo.

Aidha vituo vya Sota, Nyang’ombe, Kibuyi na Ruhu vikiendelea kupokea samaki aina ya Sangara kutoka kwa wavuvi na kuzipeleka viwandani kwa ajili ya kuchakatwa na kupelekwa kwenye soko la Nchi za Ulaya.

Alisema Agosti 15 nyavu zipatazo 15 aina ya timba zenye matundu ( Mesh) yenye ukubwa wa inchi 3 zikiwa na thamani ya Sh. 1,350,000 zilikamatwa.

Aliongeza kuwa nyavu aina ya timba (Monofilament) zapatazo 18 zenye macho ya 3.1\2 zikiwa na thamani ya Sh. 1,620,000 zilikamatwa pamoja na samaki wachanga aina ya sangara zenye thamani ya Sh. 60,000 zilichomwa moto na samaki ziligawiwa wananchi.

Samaki wengine wachanga aina hiyo hiyo walikamatwa katika kisiwa cha Bugambwa Kibuyi zenye thamani ya Sh. 150,000 ambazo pia ziligawiwa wananchi.

Aidha nyavu zingine aina Monofilament 4 za nchi 3 zenye thamani ya Sh. 360,000 pamoja na samaki wachanga wenye wa Sh. 90,000 zilichomwa moto na samki ziligawiwa wananchi.

Kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruhu na wadau, Nyavu wa aina ya Timba (Monofilament) za nchi 4.5 zenye thamani ya Sh. 100,000 na samaki wachanga aina ya sato wenye thamani ya Sh. 72,900 zilikamatwa na kugaiwa wanachi na nyavu kuteketezwa kwa moto.

Vile vile mwezi Septemba nyavu zingine nane aina ya Monofilament ya inchi 3 zilichomwa moto,zikiwa na thamani ya Sh. 720,000.

Katika tukio hilo vatu watatu wamefikishwa mahakamani ya Wilaya ya Tarime kwa tuhuma ya kuvua samaki kwa kutumia madawa katika Shauri Na. CC.371/2011 dhidi ya Tumaini Makasa, Amani Makasa, Iddi Obeid na Nyarongo Waryoba, Shauri jingine linasubiri uthibitisho kutoka maabara ya Taifa ya Uvuvi ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.

Aidha Wilaya ya Rorya ina mkakati wa kuboresha ukusanyaji mapatto kutokana an ada za leseni za uvuvi,biombo vya majini na usajili wa biombo vipya na ulinzi wa rasilimali za uvuvi.

Saturday, November 12, 2011

UKAGUZI WA SHULE WILAYA YA RORYA ZERO!!!!

RORYA.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rorya, Cosmas Ngangaji, amesikitishwa na mahudhurio mabaya ya wanafunzi wa shule ya Msingi Irienyi,pamoja na shule zipatazo 30 kutokaguliwa kwa takribani miaka saba, wakati wakaguzi wa shule walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya shule za Msingi katika Wilaya ya Rorya.

Aliyasema hayo,wakati akizungumza na Blog hii, juu ya matatizo yanayoikabili Wilaya hiyo kwa upande wa elimu,mara baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Novemba 11.

Alisema kuwa wakaguzi hao walifanya ziara mapema septemba 10 mwaka huu na kubaini upungufu mkubwa wa mahudhurio ya wanafunzi kutoka wanafunzi 788 wanaopaswa kuwa madarasani na kukuta wanafunzi 217 tu sawa na asilimia 27.5.

Alisema kuwa katika hali isiyo ya kawaida kuna shule zipatazo 30 ambazo haizijawahi kukaguliwa kati ya miaka 6-7 na kwamba zina hali mbaya sana.

Aliongeza kuwa pamoja na matatizo hayo pia kuna upungufu mkubwa wa wa madawati hasa shule ya msingi Ryagati ambapo jumla ya madawati 193 yanahitajika na kwamba mpaka sasa yapo madawati 47,kwa kuwa haikupata mgao wa madawati ya Mbunge wa jimbo la Rorya,Lameck Airo na mgao kutoka mfuko wa jimbo.


Aidha umefanyika pia ukaguzi maalumu kwa kata zipatazo mbili za Bukwe na Nyathorogo kwa shule za Msingi za Chuchuri na Mori ambazo pia zina mapungufu ikiwa ni pamoja na kuongeza ujenzi wa vyumba za madarasa katika shule ya Msingi Chuchuri,ambapo Shule ya Msingi Nyathorogo imeaza ujenzi wa vumba viwili vya madarasa ya awali.

Wednesday, November 2, 2011

KWA KHERI MDOGO WANGU.

KWA KHERI MDOGO WANGU OLIVA VEDASTUS MASHAURI, ULITUTOKA TAREHE 28.10.2011, UTAKUMBUKWA NA MWANAO MPEDWA, VEDASTUS.BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LITUKUZWE.

Wednesday, October 26, 2011

MTOTO MCHANGA ATUPWA AKUTWA HAI.

MUSOMA.


MTOTO Mchanga wa jinsia ya kike anayekadiriwa kuwa wa wiki mbili ,Agosti 25 ameokotwa akiwa ametupwa kwenye korongo katika Mtaa wa Mtakuja na Zanzibar, kata ya Mwisenge,kikiwa kimetupwa na mtu asiyejulikana.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishina Msiadizi wa Polisi (ACP),Robert Boaz alisema kuwa mtoto huyo amegunduliwa na watoto wa shule ya Msingi wa Tatu Issa (32) walipokuwa wakipita kwenye korongo hilo wakielekea shuleni na ndipo waliporudi nyumbani kumpatia taarifa Mama yao.

Alisema Mama huyo alimkuta mtoto huto akiwa mtupu na alikuwa hai ,ndiopo alipotoa taarifa kwa Polisi,mtoto huyo amehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa wa Mara iliyoko katika Manispaa ya Musoma.

Aidha ametoa wito kwa watu ambao wanahisi kuna mama alikuwa mjazito na hana ujauzito watoe taarifa kituo cha Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Katika tukio jingine lililotokea katika wilaya ya Bunda, majira ya saa 10 jioni stend ya Mabasi, mtoto mchanga wa jinsia ya kiume wa Chausiku Kelaryo( 21), mwenye umri wa wiki moja na nusu ameibiwa.

Alisema Chausiku alimwachia Mama mmoja asiyemfahamu kumshikia ili akanunue mboga sokoni, kutoka sokoni akakuta mama huyo ametoweka na mwanae.

Ametoa wito kwa wakazi wa Wilaya hiyo kama kutakuwa na utata juu mama huyo na kwamba hakuwa na ujauzito watoe taaifa kituo cha Polisi ili hatua dhidi ya mama huyo zichukuliwe.

NOTI BANDIA ZAKAMATWA



MUSOMA.

JUMLA ya noti bandia zipatazo 16 za Sh 10,000 na Sh. 5,000 zipatazo 12 zimekamatwa katika Manispaa ya Mji wa Musoma.


Akizungumza na Mwandishi wa habari hii ofisini kwake Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Mkoa wa Mara, Robert Boaz alisema tukio hilo limetokea Agosti 24 mwaka huu katika mtaa wa Jamatini majira ya saa 2 usiku katika Super Market ya Msendo wakati mteja akinunua vocha ya Sh.5,000.

Alisema baada ya kuugundua si noti halali alipiga simu kwa askari wa doria na kumkamata mtuhumiwa aliyemtaja kuwa Mashaka Samson, mkazi wa Musoma Mjini mtaa wa Karume.

Kamanda Boaz alisema noti hizo zilikuwa na namba tofauti tofauti ambapo noti zipatazo nane za Sh.5,000 zilikuwa na namba aina moja AA 084 598 na nne zikiwa na namba ADO 845 927, noti za 10,000 zilikuwa nne , tatu zikiwa na namba BB 0315203 na moja ikiwa na namba BC 031 5209.

Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kujibu mashitaka.


Saturday, October 22, 2011

VIONGOZI WA MWENGE 2010


Mkimbiza Mwenge kitaifa, Nassoro Ally Matuzya akifuraia mara baada ya kukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

KAMPUNI YA SIMU TANZANIA YAHUJUMIWA.

MUSOMA.



KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) Mkoa wa Mara imehujumiwa kwa kukatiwa mikongo ya simu yenye urefu wa Mita 4,000 na wananchi wasio wema na kusababisha hasara kubwa ya Mamilioni ya fedha kwa kipindi cha miezi sita.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa na Mwandishi wa habari hii ofisini kwake wakati wa mahojiano, Meneja wa kampuni hiyo, Richard Augustine alisema ingawaje kampuni inajitahidi kutoa huduma nzuri kwa wakazi wa Mji wa Musoma na Tarimr lakini inakubiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisema kwa sasa wakazi wa kata za Bweri machinjioni na Rwamlimi na Wilani Tarime ambao wanakosa huduma hiyo muhimu majumbani kwao kutokana na tatizo hilo ambalo limeipatia kampuni hasara ya kiasi cha Sh Milioni 50.

Aliongeza kuwa ukaratabati wa miundo mbinu ya kupitisha maji, barabara imekata baadhi ya mikongo maeneo ya kiwanda cha Nguo cha Mutex suala ambalo linashughulikiwa ili kiwanda hicho kiweze kuendelea kupata huduma.

“Suala hili la ukarabati wa barabara na upitishaji maji ni lazima tuwe tunashirikiana ili kuepuka gharama zingine zisizo za lazima, pia suala la ushirikiano baina ya vyombo vya dola na kampuni yetu ni jambo la msingi sana ili kuhakikisha vitendo vya namna hii vinatokemea,kwani wahujumu hawa wanafahamika na wengine tumekuwa tukiwakamata na ni wezi sugu wanafahamika”Alisema Richard.

Akizungumzia kuhusu kutanua wigo wa mtandao alisema kampuni ina mkakati huo kwani kwa sasa huduma ya simu ya mkononi ya TTCL Mobile haifiki maeneo mengi ukilinganisha na kampuni zingine, sanjali na mtandao wa Broad band ambao kwa sasa watumiaji wengi wamekuwa wakifahidika nayo.

Akizungumzia juu ya kupanda kwa gharama za umeme alisema gharama zimekuwa kubwa kulinganisha na awali ambapo huduma hiyo ilikuwa ikipatikana,haipungui japo kuwa kuna mgao na kwa maeneo mengine yameathiri utendaji kwa kampuni hiyo, kutokana na matumizi makubwa ya mafuta kwenye generator, huku Ankara pia zikipanda.



“Nilifikiri gharama zitapungua kutokana na mgao wa umeme,lakini cha ajabu tumekuwa tukitumia mafuta kwa wengi tukijua Ankara za Tanesco zitapungua lakini imekuwa kinyume zinakwenda sambamba” Alisema Richard kwa mshangao.


UWEKAJI MAMBOMBA YA MAJI WAKWAMA

BUNDA.

MKANDARASI ambaye alikuwa aanze kazi ya ujenzi wa miundo mbinu katika Mradi wa Maji wa vijiji vya Mugeta na Nyang’aranga katika Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara hajaanza kazi hadi apatikane mtaalamu mshauri wa Mkandarasi.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii, Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bunda, Tanu Deule alisema kuwa limetolewa agizo kutoka Wizara ya Maji jijini Dar es Salaam kuwa huduma ya kutandaza mabomba isitishwe kwanza hadi atakapopatikana Mtaalamu MShauri wa Mkandarasi huyo.

Jiwe la Msingi la Ujenzi wa mradi wa maji wa Mugeta na Nyang’aranga katika Wilaya ya Bunda liliwekwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa na ziara yake ya kikazi Mkoa wa Mara ulitarajiwa kuanza septemba mwaka huu.

Mradi wa maji wa vijiji vya Mugeta na Nyang’aranga umebuniwa ili kusaidia wananchi wapatao 5,000 wa vijiji hivyo kuondokana na adha ya kutafuta maji yasiyo salama kwenye umbali mrefu.

Lengo ni kuwawezesha wapate maji safi na salama karibu na makazi yao ili waweze kuwa na afya bora na kutumia muda wao kwa shughuli za maendeleo na kuboresha mahudhurio ya wanafunzi shuleni.

Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bunda Tanu Deule alisema Mradi huo unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 5000 kwa saa, ujenzi wa bomba kuu la kupeleka maji kwenye tanki umbali wa kilomita 1. 982, ujenzi wa mtandao wa mabomba kilomita 31.158 ya kusambaza maji kwa watumiaji, Ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji, ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000, kuweka mfumo wa umeme kwenye kisima cha maji, Ujenzi wa nyumba ya pampu na usimikaji wa pampu ya kusukuma maji.

Mradi huo unajengwa kwa ubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Japani kupitia mfuko wa “Tanzania/Japan Food Aid Counterpart Fund (FACF) ulio chini ya Wizara ya Kilimo na Chakula.

Mradi unakadiriwa kugharimu jumla ya Tsh 270,000,000,Serikali ya Japani (J FACF) itatoa Tsh 240,000,000,Serikali ya Tanzania kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Bunda itatoa Tsh 23,000,000 ,Wananchi watachangia nguvu zao sawa na Tsh. 7,000,000

Mpaka sasa Halmashauri imekwisha pokea kiasi cha Tshs 107,000,000 kutoka Serikali ya Japan na Tshs 90,778,809 zimetumika, na Halmashauri imekwisha toa Tshs 3,000,000.

Aidha Kazi ambazo tayari zimekwisha kufanyika ni pamoja na uchimbaji wa kisima kirefu na Ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 kwenye nguzo ya urefu wa mita 10 katika kijiji cha Mugeta.

Sanjali na hilo kuna kazi ambazo bado hazijafanyika ikiwa ni pamoja na kununua mabomba na kuyalaza kwenye njia kuu na njia ya kusambaza maji kwa watumiaji, kuvuta umeme hadi kwenye kisima cha maji, kununua pampu na kuisimika na kujenga nyumba ya pampu.