HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA VIONGOZI WA TAKUKURU- MWANZA, 25 FEBRUARI 2010.
Mhe. Sophia Simba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora),
Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Dkt. Edward Hoseah, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Viongozi na Watumishi wa TAKUKURU,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Nakushukuru Mheshimiwa Waziri na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa mwaliko wenu kwangu wa kuja kushiriki katika Mkutano wa Mwaka wa taasisi yetu hii muhimu. Hii ni mara yangu ya pili kuzungumza nanyi tangu niwe Rais wa nchi yetu Desemba, 2005. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa, mara ya kwanza, ilikuwa tarehe 20 Februari 2006 kule Mbeya – miezi miwili tu baada ya kuapishwa kuwa Rais.
Wakati ule, niliwaeleza matumaini yangu kwenu katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo chombo chetu hiki ndicho kilicho mstari wa mbele. Niliwaahidi ushirikiano wangu wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa tunapata mafanikio makubwa zaidi katika mapambano haya. Niliwaahidi kutoa msaada wa hali na mali kwa Taasisi yetu hususan katika kujenga uwezo wake wa kiutendaji. Niliwaeleza pia kwamba katika kufanya kazi zenu msikubali kutishwa au kuingiliwa na mtu kwa sababu mimi sitawaingilia, kuwashinikiza au kuwatisha. Nilichosisitiza kwenu ni kwamba mhakikishe kuwa mnatenda kazi zenu kwa umakini na kwa haki. Niliwataka muepuke kuonea au kukomoa mtu. Aidha, nilitaka mtambue kuwa mashtaka yahusuyo rushwa yanafedhehesha na yanamtia mtu doa kubwa katika jamii, hivyo basi ni muhimu kwenu kujiridhisha kuwa kweli mtu anazo tuhuma za kutosheleza kabla ya kumfungulia mashtaka.
Tunapokutana leo, mwanzo mwa mwaka wa tano na wakati ambapo miezi si mingi kabla ya uchaguzi mkuu, ni vyema kutumia fursa hii kutafakari mafanikio tuliyoyapata na changamoto zinazokubalika katika kupambana na rushwa nchini. Nafurahi kwamba madhumuni ya msingi ya mikutano ya kila mwaka ni kufanya tathmini ya kazi zenu kwa mwaka uliopita na katika mkutano huu mnafanya tathmini ya mwaka 2009.
Mafanikio katika Kupambana na Rushwa
Ndugu Washiriki,
Ni ukweli ulio wazi kuwa, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, tumepata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya rushwa nchini. Napenda kuitumia fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa kazi nzuri mliyoifanya na mnayoendelea kuifanya. Natambua kwamba kazi muifanyayo ni kubwa na ngumu. Ni kazi inayohitaji ujasiri mkubwa na moyo wa kujitolea na kujituma. Na, ni kazi ambayo mtu ambaye hayuko tayari kukubali lawama haiwezi. Mtu anayetafuta kupendwa na TAKUKURU si mahali pake.
Nauelewa uzito na ugumu wa kazi yenu, kama ninavyoelewa mazingira yenu magumu ya kazi na vikwazo ambavyo mnakabiliana navyo katika kutimiza majukumu yenu. Ni jambo la faraja kubwa kwangu na kwa Watanzania wenzetu kwa ujumla kwamba mnaweza kuvikabili vikwazo hivyo kwa umahiri mkubwa.
Mkurugenzi Mkuu na Ndugu Washiriki,
Napenda kuwahakikishia kwamba nitaendelea kuwa mwenzenu kwa kila hali katika mapambano haya. Ahadi yangu kwenu siku ya leo ni kuendelea kuwaunga mkono kwa hali na mali ili muweze kutimiza ipasavyo wajibu wenu. Nitaendelea kuhakikisha, kwa kadri inavyowezekana, kwamba taasisi yenu inapata rasilimali za kutosha ili iwe na watumishi wa kutosha na wenye ujuzi pamoja na vitendea kazi vya kutosha.
Nafanya hivi kwa sababu kubwa mbili. Kwanza, kwamba naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa kuendelea kuwepo na kuendelea kukua kwa tatizo la rushwa nchini ni uporaji wa haki za raia na kikwazo kwa maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla. Lazima tufanye kila tuwezalo kupiga vita rushwa. Sababu ya pili ni kwamba kupambana na rushwa ndiyo maagizo ya Chama cha Mapinduzi tangu TANU na ni moja ya ahadi muhimu katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005.
Ndugu Mkurugenzi Mkuu na Ndugu Washiriki,
Mambo hayo mawili ndiyo yaliyoiongoza Serikali yetu kushiriki kwa ukamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Na ndiyo yanayoendelea kuiongoza mpaka mwisho wa kipindi chake Oktoba 2010. Iwapo tutachaguliwa tena yataongoza jitihada hizo katika miaka mitano ijayo.
Tumewekeza sana katika kujenga uwezo wa kiutendaji wa TAKUKURU. Tumetunga Sheria mpya, 2007 badala ya ile ya mwaka 1971. Kama mjuavyo, Sheria mpya inapanua dhana ya Taasisi kuwa pia ya kupambana na rushwa badala ya kuwa kuzuia pekee. Imetoa tafsiri pana zaidi ya makosa ya rushwa, hivyo basi makosa yamekuwa 24 badala ya 4 ya sheria ya mwaka 1971.
Sheria mpya imeongeza adhabu na kutoa mamlaka makubwa zaidi kwa Taasisi katika kupambana na rushwa. Taasisi yetu sasa ina uwezo wa kukamata na kushitaki kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Mashitaka. Watumishi wa Taasisi wamepatiwa kinga wakati wa kutimiza wajibu wao. Sheria hiyo imeleta mabadiliko makubwa na ya msingi ambayo yanaimarisha mapambano dhidi ya rushwa na uwezo wa TAKUKURU kushiriki, kuongoza na kuratibu mapambano haya.
Ndugu Washiriki,
Jambo la pili kubwa na la msingi ni lile la kuchukua hatua za makusudi za kuimarisha na kuijenga Taasisi yetu. TAKUKURU sasa imekuwa taasisi kubwa zaidi kwa maana ya kuwa na watumishi wengi zaidi na mtandao mpana wa ofisi nchini. Watumishi wengi wapya wameajiriwa na wengi wamepata mafunzo ndani na nje ya nchi. Hivi sasa Taasisi yetu hii ina ofisi katika Wilaya zote 116 na mikoa 24 ya Tanzania Bara. Taasisi sasa inayo magari mengi na vifaa vingi zaidi vya kisasa vya kufanyia kazi.
Pamoja na kusema hayo, natambua fika kwamba TAKUKURU bado ina mahitaji mengi ili kuiwezesha kutekeleza kwa ubora zaidi majukumu yake. Napenda kuwaahidi kuwa tutaendelea kuiboresha bajeti ya TAKUKURU mwaka hadi mwaka ili tuzidi kuimarisha na kujenga taasisi yetu. Dhamira hiyo tunayo na tuko tayari kuitimiza.
Ndugu Mkurugenzi Mkuu naNdugu Washiriki,
Nayasema yote haya kusisitiza ukweli kwamba vita dhidi ya rushwa haitafanikiwa nchini bila ya kuwa na Taasisi imara ya kuongoza na kuratibu mapambano haya. Taasisi hiyo si nyingine bali ni TAKUKURU. Maelekezo ya Rais pekee au kelele za wanasiasa au chuki za wananchi dhidi ya rushwa pekee havitoshi. Sharti pawepo na TAKUKURU iliyo imara kwa maana ya nguvu ya kisheria na uwezo wa kiutendaji. Hayo tumeyafanya vizuri katika miaka hii minne na, kama nilivyokwishasema, tutaendelea kufanya zaidi mwaka huu na miaka ijayo. Inshallah.
TAKUKURU na Vyombo Vingine
Ndugu Washiriki,
Pamoja na hayo, ili TAKUKURU ipate ufanisi katika utendaji wake wa kazi, haina budi ifanye kazi kwa ushirikiano wa karibu na baadhi ya vyombo vya Serikali, hasa zile taasisi zinazohusika na maswala ya sheria, utoaji wa haki na utawala bora. TAKUKURU haiwezi kufanikiwa katika shughuli zake kama haitakuwa na mahusiano mazuri na ushirikiano wa karibu na Idara ya Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG Chambers), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Tume ya Maadili, Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA)na taasisi nyinginezo. TAKUKURU inazihitaji taasisi hizi kama ambavyo kila moja ya taasisi hizi nazo zinaihitaji TAKUKURU kwa ukamilifu wa shughuli zake.
Tatizo la rushwa linahitaji ushirikiano wa vyombo vyote hivyo ndipo matunda tunayoyataka yanapoweza kupatikana. Kulaumiana miongoni mwa taasisi, kutegeana au kutoshirikiana ipasavyo ni mambo ambayo yatadhoofisha mapambano haya. Lazima mtafute njia za kushirikiana na kushauriana kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu washiriki,
Ninaposema haya au ninapotoa wito huu, naomba isieleweke kwamba hivi sasa hakuna ushirikiano au kuna kutokuelewana miongoni mwa taasisi zetu. La hasha, nataka kusisitiza haja na umuhimu wa mashirikiano kuimarishwa na kuboreshwa miongoni mwa taasisi zetu. Nimefurahi kwa mfano, kwamba TAKUKURU mmesaini makubaliano ya ushirikiano na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) katika kushughulikia masuala ya rushwa katika ununuzi wa bidhaaa na huduma serikalini.
Hii ni hatua kubwa na muhimu kabisa, kwani rushwa nyingi na hasa zile kubwa kubwa Serikalini zinahusiana na shughuli za ununuzi wa mahitaji ya serikali na mikataba mbalimbali ya huduma. Hatua hii pia itasaidia kuhakikisha kuwa fedha za umma zinadhibitiwa ipasavyo na kutumika kufanya kazi iliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi wapate maendeleo na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wa Taarifa za CAG kuhusu ukaguzi wa hesabu za Serikali nilikwishaelekeza siku za nyuma kuwa, mara wizi au ubadhirifu wa fedha na mali ya umma ukigundulika TAKUKURU iarifiwe ili ichukue hatua zipasazo. Kufanya hivyo hakuingilii mamlaka wala wajibu wa CAG wa kuwasilisha taarifa kwa Rais ili taarifa hiyo ipelekwe Bungeni kujadiliwa. Mimi naamini hiyo itakuwa bora zaidi kwani hata katika taarifa yake CAG anaweza kueleza kuwa wizi au ubadhirifu fulani uliogunduliwa, umeshatolewa taarifa kwa vyombo vya dola kwa hatua zipasazo za kisheria.
Ndugu washiriki,
Nimepokea kwa faraja kubwa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu kuhusu kiasi kikubwa cha fedha za umma zilizookolewa na taasisi hii kila mwaka. Hongereni kwa kazi nzuri, tafadhali endeleeni kushirikiana na wadau mbalimbali ili muweze kupata mafanikio makubwa zaidi siku zijazo. Endeleeni na kazi ya uchunguzi na ukaguzi wa miradi na ya kufuatilia na kudhibiti matumizi ya fedha za serikali ili fedha kidogo tunazotoa ziweze kuwanufaisha walengwa. Fedha hizo ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa badala ya kutajirisha maofisa wa umma wachache.
Rushwa katika Siasa
Ndugu Washiriki,
Mwaka huu tumepiga hatua muhimu katika jitihada zetu za kupambana na rushwa katika uchaguzi hapa nchini. Ni ukweli ulio wazi kwamba rushwa katika chaguzi inaanza kuwa tatizo kubwa. Ni dhahiri kwamba tusipochukua hatua za dhati sasa, kutoa na kupokea rushwa au hata kuomba rushwa kunaweza kuwa ni utaratibu wa kawaida. Kama tutafikia hatua ambayo kufanya hayo itakuwa ndiyo utamaduni katika chaguzi zetu, taifa letu litakuwa limeangamia. Iwapo uongozi unaweza kununuliwa kama njugu au shati, hata mwendawazimu au mhalifu anaweza kuwa kiongozi ili mradi tu awe na pesa. Hiyo ni hatari kwa ustawi na usalama wa nchi yetu, kamwe tusikubali tufike huko.
Sheria ya matumizi ya fedha katika uchaguzi iliyopitishwa na Bunge katika kikao kilichopita ni jambo la kihistoria na ni hatua ya kimapinduzi. Ina nia ya kutuzuia tusifike pabaya, labda wenyewe tupuuze kuitekeleza. Inatuweka mahali pazuri pa kuanza mapambano na watu wanaotaka kupata uongozi kwa nguvu ya pesa. Pia inasaidia kuwabana watu wanaogeuza haki yao ya kupiga kura kuwa ni mradi au bidhaa ya kunufaika nayo kipesa kwa kuiuza. Sasa ole wao wahongaji, ole wao wahongwaji na ole wao wanaoomba kuhongwa.
Ndugu Mkurugenzi Mkuu, Ndugu Washiriki,
Nafarijika sana kwamba ahadi niliyoitoa tarehe 30 Desemba, 2005 wakati wa kuzindua Bunge letu hili, sasa imetimia. Ningependa kuona hakuna mtu yeyote anayejihusisha au kutuhumiwa kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi wakati wa mchakato wa uchaguzi ndani ya vyama na wakati wa uchaguzi wenyewe baina ya vyama, anaachwa bila kushughulikiwa. Ninyi katika TAKUKURU ndiyo mnaotazamiwa kufanya kazi ya kukazia utekelezaji wa sheria hii mpya. Napenda kuwahakikishieni, wana-TAKUKURU kwamba nitafanya kila liwezekanalo kuwawezesha ili muweze kufanikisha kazi ya kudhibiti rushwa katika chaguzi zetu nchini. Nataka tuanze na uchaguzi huu.
Anzeni sasa kujipanga kuifanya kazi hiyo kwani naambiwa wanunuaji wa uongozi wameshaanza. Sheria inaruhusu kudhibiti rushwa kabla na wakati wa kura ya maoni ndani ya vyama vya siasa na wakati wa uchaguzi. Nawaomba muanze kufuatilia na kuchukua hatua zipasazo. Na, ukweli ni kwamba rushwa kubwa ipo wakati wa kura za maoni katika vyama pengine hata kuliko wakati wa uchaguzi wenyewe.
Ndugu zangu,
Ningependa kuona kuwa wakati mimi na wenzangu, tutakapomaliza muda wetu wa uongozi, tuwe tumejenga misingi imara ya utawala bora, demokrasia, na maadili ya viongozi wa umma. Misingi ambayo itajikita katika sheria za nchi na baadaye kuwa utamaduni wa kudumu wa kuendesha shughuli za siasa katika nchi yetu.
Elimu kwa Umma na Wadau Wengine
Mheshimiwa Waziri na Ndugu Viongozi wa TAKUKURU,
Nimesema kule mwanzoni, kuwa mafanikio yetu katika vita hii yanategemea uimara na ubora wa TAKUKURU. Hichi ndicho chombo cha taifa kilicho mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa. Ndicho chenye dhamana ya kuwaongoza na kuratibu mapambano hayo. Nimeelezea kwa kiasi gani Serikali imechukua hatua za kujenga na kuimarisha TAKUKURU. Kazi bado inaendelea, hatua kubwa imefikiwa na mafanikio ya kutia moyo yamepatikana na yanaendelea kupatikana. Mkurugenzi Mkuu ameelezea kwa ufasaha mafanikio yaliyopatikana, si haja ya kuyarudia.
Nimeelezea pia kuhusu umuhimu wa TAKUKURU kushirikiana na taasisi nyingine ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na kazi za upelelezi, ukamataji na uendeshaji wa mashitaka mahakamani. Aidha, nilieleza kwamba wajibu wa ushirikiano unazihusu taasisi hizo pia, kwani nazo mafanikio yake yanategemea uhusiano mzuri na TAKUKURU na taasisi nyingine. Nimeeleza furaha yangu na kuridhishwa kwangu na ushirikiano uliopo na kutaka uendelee.
Ndugu Mkurugenzi Mkuu na Ndugu Viongozi wa TAKUKURU,
Mtakubaliana nami kwamba, pamoja na ubora na uimara wa TAKUKURU na hata kama kutakuwepo mashirikiano mazuri na taasisi nyingine za Serikali, ushirikiano mzuri na wadau wengine nao ukipatikana ndiyo ukamilifu wa juhudi hizi. Hapo ndipo TAKUKURU inapoweza kujihakikishia ushindi.
Mdau wa kwanza ni Wizara, Idara za Serikali na Mashirika ya Umma. Katika Serikali tunao Mkakati wa Taifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (NACSAP) ambao utekelezaji wake unahusisha kila Wizara, Idara za Serikali na Mashirika ya Umma. Kama kila mmoja wetu atatekeleza ipasavyo wajibu wake tutapata mafanikio makubwa katika kuzuia na kupambana na rushwa kwa upande wa watumishi wa umma.
Swali ambalo sote hatuna budi kujiuliza na kuulizana ni je, mipango ya kila Wizara, Idara ya Serikali na Mashirika ya Umma iko wapi na kama kweli inazingatiwa na kutekelezwa? Mimi sina hakika, sijui nyie wenzangu. Naona tu mmerudia sifa yetu ya kuwa nguvu ya soda.
Mheshimiwa Waziri, Ndugu Mkurugenzi Mkuu na Ndugu Washiriki,
Napenda kuitumia nafasi hii kuwakumbusha Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara za Serikali na Mashirika ya Umma kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha kuwa Mkakati wa Taifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika maeneo yao ya uongozi uko hai na unatekelezwa kama ilivyokusudiea. Wahakikishe kuwa watumishi wote chini yao wanaelimishwa vya kutosha na kuna ufuatiliaji wa dhati kuhakikisha rushwa inadhibitiwa.
Nakuomba, Waziri wa Utawala Bora na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU mtambue kuwa mnao wajibu maalum wa kuhakikisha kuwa mambo yanatekelezwa ipasavyo. Wizara na TAKUKURU muendelee kuelimisha na kuhamasisha watumishi wa umma wajiepushe na vitendo vya rushwa. Wanaokaidi wabanwe. Mabango yatengenezwe upya tena kwa wingi na kusambazwa kila ofisi.
Mheshimiwa Waziri na Mkurugenzi Mkuu,
Naomba pia, hata sekta binafsi wahusishwe kwani hata na wao wanahusika katika vitendo vya rushwa. Wapo Maofisa na Watendaji katika makampuni binafsi wanaojihusisha na vitendo vya kutoa, kudai, na kupokea rushwa. Wanafanya hivyo katika ajira, kutafuta masoko na kutafuta zabuni. Bahati mbaya sana hata waandishi wa habari nao hawako salama katika kadhia hii. Hivyo rushwa ipo kila mahali, sote tuhusike na kuhusishwa katika mapambano haya.
Wadau wengine muhimu katika mapambano haya ni umma wa wananchi wa Tanzania ambao ndiyo hasa wahanga wa vitendo vya rushwa. Wanaathiriwa moja kwa moja kwa kudaiwa rushwa au kupata huduma duni kwa sababu ya wahusika kupokea rushwa na kazi kufanywa kwa kiwango cha chini. Wananchi wanachukizwa sana na vitendo vya rushwa vya watumishi wa umma na hata wa sekta binafsi wanaomba usiku na mchana rushwa ifutike. Tuendelee kuwahamasisha wazidi kuchukia rushwa na hasa wawe tayari kutoa taarifa za vitendo vya rushwa bila ya woga. Tuwaelimishe kuwa watoa taarifa wanalindwa na sheria. Tukifanikiwa kwa hili vita hivi tutashinda kwani wao wanajua mengi. Endeleeni kuelimisha na kuhamasisha wanachi. Najua mnafanya hivyo sana lakini ongezeni bidii. Ombi langu kwenu ni kuwa muwe wepesi kuzifanyia kazi taarifa mnazopewa na wananchi. Mkifanya hivyo mnawatia moyo waweze kuwapeni taarifa nyingi zaidi.
Changamoto
Ndugu Washiriki,
Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu imeelezea changamoto mnazokabiliana nazo, lakini pia imeelezea hatua mnazochukua kukabiliana na kila changamoto. Jambo hili limenifurahisha sana, kwani kuna baadhi ya sehemu huwa naalikwa halafu kwenye maelezo au risala ya wenyeji wangu, ninaorodheshewa changamoto tu, ili nizijibu mimi. Hakuna maelezo toka kwa wenyewe kuelezea hatua wanazochukua. Mbaya zaidi ni pale anayekueleza ndiye kiongozi mnadhimu wa eneo hilo. Anaona yeye hahusiki kutafuta ufumbuzi isipokuwa kuna mtu mwingine ambaye ni mimi Rais. Nimefurahi kwamba ninyi mnajua uzito wa kazi yenu, mnajua nini mfanye ili mfanikiwe. Mnajua yaliyo kwenye uwezo wenu na yale ambayo yako nje ya uwezo wenu. Nawaahidi yaliyoko nje ya uwezo wenu nitawasaidia, mimi, kufanya au kuwafikishia wahusika.
Chuo cha TAKUKURU
Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
Sina budi nikushukuru wewe, Mkurugenzi Mkuu na viongozi wenzako, kwa uamuzi wenu wa kujenga Chuo cha TAKUKURU. Hiki kitakuwa ni chuo cha kwanza cha aina yake nchini na huenda katika Afrika. Kitasaidia sana katika kuwaongezea elimu na maarifa maafisa wenu hivyo kuwajenga kwa ubora na weledi. Naomba mhakikishe kuwa Chuo hicho kinatoa elimu ya kiwango cha juu katika shughuli za kuzuia na kupambana na rushwa. Mitaala iwe ya viwango vya kimataifa ili Chuo kitoe maofisa walio bora na wenye sifa zinazovuka mipaka ya nchi yetu. Mkifanya hivyo, Chuo kinaweza hata kutumiwa na nchi jirani au hata na nchi nyingine Barani Afrika. Niko tayari kuwasaidia kwa hali na mali katika kufanikisha dhamira yenu njema.
Msichoke kufundisha watu wenu na kuwapa fursa ya kujifunza. Hii itawahakikishia kuwa watumishi wa TAKUKURU wana viwango vya juu ya uweledi unaothibitishwa na utendaji kazi wao wa hali ya juu. Watakuwa wapelelezi wazuri na waendesha mashtaka mahiri. Aidha, hiyo itawafanya muepuke aibu ya kupeleka kesi mahakamani kushindwa.
Mwisho
Mhe. Waziri, Ndugu Mkurugenzi Mkuu, Ndugu Washiriki,
Napenda nimalize kwa kuwakumbusha kwamba, mmepewa dhamana kubwa na taifa letu pamoja na umma wa Watanzania. Sisi sote tunawategemea nyinyi. Tuko pamoja nanyi na tuko nyuma yenu. La msingi, ni kama nilivyosema awali msimuonee haya mtu ambaye ni mhalifu na msimuonee mtu ambaye hana makosa. Tendeni haki kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni. Matunda ya kazi yenu yataonekana.
Vilevile, katika kutekeleza majukumu yenu ya kupambana na rushwa, lazima TAKUKURU yenyewe kama chombo kiwe na watumishi waadilifu na waaminifu. Kamwe msiruhusu kuwepo na chembe hata moja ya kutiliwa mashaka kuhusu uadilifu wenu. Hivyo basi, kazi ya kuhakikisha watumishi wenu ni waadilifu iwe ya kudumu. Msioneane muhali katika hilo. Heshima ya TAKUKURU mbele ya umma wa Watanzania inategemea uadilifu na weledi wa watumishi wake.
Baada ya kusema maneno yangu haya mengi, niruhusuni sasa kutamka rasmi kwamba Mkutano wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU umefunguliwa rasmi. Nawatakieni majadiliano mema.
Asanteni sana kwa kunisikiliza!