Tuesday, August 3, 2010

WAGOMBEA UBUNGE UWT WALALAMIKA.

KUTOKA MUSOMA MKANI MARA

Baadhi ya wagombea Ubunge Viti Maalum kundi la Wanawake walioshindwa katika kura za maoni za kuwapata wagombea watano kwa kila Mkoa,Mkoa wa Mara kupitia Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) wameliomba Baraza Kuu la UWT Taifa kuwachunguza baadhi ya wagombea waliopita katika Kura za maoni kabla ya kupendekeza ya majina yatakayowasilishwa kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kutokana na ukiukwaji wa Kanuni.

Walisema kutokana na ukiukwaji huo,baadhi yao hawana sifa ya kuwa viongozi kwa kuwa si wanachama halali wa UWT kwani kifungu cha kanuni cha UWT kinasema Mwanachama atakayechukua fomu ya kugombea ni yule ambaye ni Mwanachama wa UWT kwa kipindi kisichopungua miaka Mitano.

Aidha walilamikia kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha ili kuhakikisha wanapitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa kinyume na Sheria ya Uchaguzi.

Wengine walivunja kanuni kwa kuwalaza wajumbe kwenye mahoteli siku moja kabla ya Uchaguzi.huku wakitaja Nyumba ya kulala wageni ya Toto’s ya Mjini Tarime kwa wajumbe wapatao 24 kabla ya Uchaguzi ,Mujungu Guest House ya Mjini Musoma.

Pia Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa Habari hii umeonyesha kuwa ni vigumu kutekeleza Sheria kutokana na mazoea ya wanachama ambao wengi wao bila kuwapatia fedha hawawezi kuchagua kiongozi wanayemwona ni bora, bali bora kiongozi.

Wagombea Ubunge kundi la wanawake waliopitishwa kuingia tano bora Mkoani Mara ni Gaudentia Kabaka,Rosemary kirigini, Aggnes Mathew,Kichena Chambiri na Nancy Msafiri ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mara.

No comments:

Post a Comment