Monday, September 19, 2011

MTOTO WA MKULIMA AWASILI BUNDA ATOA SOLAR!

BUNDA.

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameweka jiwe la Msingi la Mradi wa maji wa Vijiji vya Mugeta na Nyang’aranga katika Wilaya ya Bunda utakaogharimu kiasi cha Sh.M. 270.

Akisoma hotuba kwa mgeni rasmi, Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bunda, Tanu Deule alisema kuwa uchimbaji wa kisima kirefu na ujenzi wa tanki maji lenye ujazo wa lita 100,000 kwenye nguzo urefu wa mita 10 tayari vimeishafanyika.

Mradi huo utahusisha uchimbaji wa kisima kirefu cha maji chenye uwezo wa kutoa maji lita 5,000 kwa saa, ujenzi wa bomba kuu la kupeleka maji kwenye tanki umbali wa kilomita 1,982, ujenzi wa mtandao wa mabomba km 31.158 ya kusambaza maji kwa watumiaji na ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji.

Alisema kuwa kazi ambazo mpaka sasa hazijafanyika ni pamoja na kununua mabomba na kuyalaza kwenye njia kuu na njia ya kusambaza maji kwa watumiaji,kuvuta umeme hadi kwenye kisima cha maji, kununua pampu na kuisimika na kujenga nyumba ya pampu ambavyo vyote zitaanza mara ya baada ya kupata mzabuni.

Aliongeza kuwa mpaka sasa zabuni imetangazwa ili kukamilisha kazii hizo na kwamba tathimini ya kumpata Mkandarasi mwenye sifa ya kufnaya kazi hizo imefanyika na mkandarasi huyo ataanza kazi mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.

Aidha mradi huo unajengwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japani kupitia mfuko wa ‘Tanzania/Japan Food Aid Counterpart Fund (FACF) ambao uko chini ya Wizara ya Kilimo na Chakula,ambapo serikali ya Japan (JFACF) itatoa Sh.M. 240, na seikali ya Tanzania kupitia halmashauri ya Wilaya itatoa Sh. M.23 na wananchi watachangia nguvu zao Sh. M.7.

Mpaka sasa halmashauri imekwisha pokea kutoka serikali ya Japan ni Sh M. 107 na jumla ya Sh. M 90.7 ambazo ni za ujenzi wa tanki la uchimbaji wa kisima.

Waziri Mkuu, amechangia umeme wa jua katika zahanati ya kijiji cha Sarawe Tarafa ya chamriho ambayo aliifungua mapema kabala ya kutoa hotuba yake.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ambapo leo atakuwa katika wilaya ya Serengeti ambapo ataweka jiwe la uzinduzi wa lambo la kijiji cha Nyamisingisi, kukagua lambo, josho, kituo cha kuchotea maji na kupandikiza samaki, pia atakagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la upasuaji na kukagua chanzo cha maji cha mji wa Mugumu (Bwawa la Manchira) na kupanda mti wa kumbukumbu.

No comments:

Post a Comment