Wednesday, September 21, 2011

WAKEKETAJI KUCHUKULIWA HATUA KALI

TARIME.

WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda ameliagiza jeshi la polisi kuwakamata na kuwafungulia mashitaka mangaliba wanaojihusisha na ukeketaji kwa wasichana.


Agizo hilo limetolewa juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Masanga Wilaya ya Tarime mara baada ya kufungua kituo cha Utamaduni wa kabila la wakurya na Jengo la kliniki ya Mama na Mtoto (RCH) alisema kuwa hakuna budi kuachana na tabia ya kuwakeketa wasichana,jambao ambalo ni hatari sana kwani wanapokuwa wanajifungua wanapata madhara kubwa ikiwa pamoja na mama kupoteza maisha.

“Najua mwezi Disemba mtafanya sherehe zenu hizo za ukeketaji kwa wanawake, nawaambia wazee wangu mlioko hapa mnanisikiliza msijaribu kabisa kufanya, vinginevyo mtajuta,RPC hakikisha unawakamata”. Alisema Waziri Pinda huku akionyesha sura ya kusikitishwa na kuwa mkali kwa jambo hili hatari kwa akina mama.


Aidha amemwagiza Waziri wa Elimu na mafunzo ya Ufundi,Dk. Shukuru Kawambwa kuweka mtaala wa kufundishia kuanzia darasa la kwanza ili wajue madhara yake sambamba na kutoa elimu kwa makabila ambayo yanaendelea kuwa na mila hiyo potofu kwa wanawake.


Akijibu hotuba ya Dk Emmanuel John juu ya kupata umeme wa gridi ya Taifa utakoagharimu kiasi cha Sh. Milioni 600 na kuwezesha huduma ya bure kwa wajawazito, watoto na wazee alisema serikali itafanya jitihada za kuhakikisha kuwa umeme unafika na huduma inapatikana kama inavyopatikana kwa hospitali za serikali.



Aidha amemwagiza Meneja wa Tanroad Mkoa wa Mara, Emmanuel Koroso kuhakikisha anatengeneza barabara hiyo yenye kilometa 30 kutoka kijiji cha Itiro hadi Masanga ambayo ni barabara inayoingia mpakani ambayo ni kitega uchumi kikubwa kwa Wilaya.

No comments:

Post a Comment