Sunday, October 14, 2012

WILAYA MPYA YA RORYA WALILIA MAJI

RORYA.



MKUU wa Wilaya ya Rorya Elias Goroi imeomba Wizara ya Maji kupitia kwa Naibu Waziri,Bilinith Mahenge kuona  uwezekano wa kuipatia kipaumbele Wilaya hiyo kutokana na upya wa Wilaya hasa maeneo ya  Ingri juu na Komuge yalipo makao Makuu ya Wilaya.
  Alisema kuwa Wilaya mpya ya Rorya inayo changamoto kubwa ya ukosefu wa maji ambapo tayari Halmashauri imetuma maombi ya fedha Wizara ya maji kwa ajili ya miradi minane  ambapo bunge lilipitisha miradi mitano ambayo ni ya Michele, Ingri Juu, Garimori. Komuge na Masonga.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa sekta ya maji ina chanagamoto nyingi ikiwemo mwitikio duni wa uchangiaji huduma ya maji kwa watumiaji wa maji,uchakavu wa miundo mbinu ya maji unaotokana na na miradi mingi kupita umri (Design Period) na gharama kubwa za uendeshaji miradi ya skimu za pampu inayotumia Dizeli ama umeme .
Aliongeza kuwa  ukilinganisha na mapato yanayatokana na malipo ya maduhuri ya maji  inawalazimu kutumia fedha nyingi za matumizi ya kawaida na kusababisha miradi mingi kusimama kutokana na ukosefu wa fedha za kulipia huduma ya mafuta na umeme.
Aidha kati ya vijiji 80 vilivyo katika Wilaya ya Rorya, Vijiji 25 ndivyo vyenye  mifuko ya maji yenye thamani ya Sh.27,863,388,  visima 85 na Kati ya hivyo visima 60 vinafanya kazi, malambo 19 na mabwawa sita.
Naye Naibu Waziri alipotembelea ujenzi wa Bwawa la Nyambori lenye ukubwa wa mita za ujazo 236,910 lenye uwezo wa kuhudumia wakazi wapatao 3,785 alishangazwa na ujenzi huo ambapo kwa sasa bwawa hilo lina nyufa ambazo zinahatarisha kuwepo na uendelevu wa kudumu wa wananchi kupata huduma hiyo muhimu.
Pia alishangazwa na wananchi kuteka maji eneo la  kunyeshea mifugo ambapo wananchi hao  walilalamikia uongozi uliopo ambao unahifadhi funguo za bomba la wananchi hali ambayo ilimlazimu Naibu Waziri Mahenge kuagiza uongozi wa kijiji kumchagua mwanamke ambaye ndiye mwangaikaji wa kutafuta maji ili aweze kuwa na funguo hizo.
Wizara ya Maji ilikabidhi bwawa hilo kwa halmashauri  ambapo  ililikabidhi kwa halmashauri ya kijiji kwa ajili ya usimamizi na uendeshaji.
Aidha akiwa Wilayani Tarime  Naibu  waziri wa Maji, Dk.Eng. Binilith Mahenge aliagiza  Mamlaka ya Maji safi na Taka (MUWASA)  kuhakikisha inafatilia madeni ya wateja wake ili iweze kujiendesha yenyewe.
“Mimi nashangaa sana mnasubiri maagizo kutoka juu wakati mkijua kabisa kuwa hayo ndiyo majukumu yenu,angalieni wenzenu wa Tanesco wanavyojiendesha wenyewe bila hata kuambiwa wasubiri kukata umeme kwa fulani,kwa nini nyie mnashindwa kufanya hivyo”Aliuliza Mahenge.
Alisema suala la kupanda kwa gharama za umeme haliwezi kuepukika na kuhusu  suala la uchakavu wa miundombinu linawezekana pale tu watakapojua kujiendesha wenyewe na kuwataka kujifunza kuwekeza kwenye maji kwani ni mtaji usiohitaji gharama kubwa na ni zaidi ya Almasi.
Serikali imetoa kiasi cha Sh. B.17.3 ya uboreshaji wa maji Mjini Tarime ambapo Wilaya hiyo ina jumla ya visima 207 vilivofugwa pampu za mkono,miradi ya maji ya kusambaza na mabomba ipatayo mitano.



No comments:

Post a Comment